Na Amiri Kilagalila,Njombe


Mwenyekiti wa jumuiya  ya wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Njombe Bi, Scholastica Kevela amesema hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka viongozi wa dini kuzungumza na waumini wao kuhusu umuhimu wa chanjo ya Covid-19 ni jambo la kupongezwa kwa kuwa limelenga kulinda Afya za watanzania.

Akizungumzia suala hilo,kwa niaba ya UWT Njombe, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Scolastika Kevela alisema Rais Samia alishawahi kusema kuwa Tanzania haipaswi kujitenga dhidi ya juhudi zinazofanywa na Dunia nzima kupambana na ugonjwa huo.

Alisema hata alipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UN na kutoa hotuba ya kuvutia na yenye kuliheshimisha Taifa, Rais Samia pia hakuacha kugusia  pia suala la Covid-19,  kutokana na kutambua umuhimu wa kujilinda

"Rais  Samia hivi karibuni amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye makao makuu ya umoja huo jijini New York ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia mapambano ya ugonjwa huo, hilo ni suala ambalo viongozi wa dini wanapaswa kumuunga mkono" alisema Mama Kevela

Awali akihutubia Baraza la UN lenye makazi yake New York nchini Marekani ikiwa ni mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo  Machi mwaka huu, Rais Samia alimulika masuala mbalimbali kuanzia uchumi, siasa, tabianchi, COVID-19 na usawa wa jinsia. 

Hata hivyo kutokana na hotuba hiyo,   Mwenyekiti huyo wa UWT alisema hotuba ya Rais Samia iliwagusa siyo tu watanzania, bali watu wa mataifa mbalimbali  hasa kwa namna alivyogusia masuala muhimu yanayoendelea kigubika dunia na hasa namna alivyohimiza nguvu ya pamoja katika kuyatafutia majawabu masuala hayo.

"kauli yake ya kuitaka dunia kutoyaacha nyuma mataifa yanayoendelea katika vita ya kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona kwa kuwa inaweza kusababisha kurudi nyuma kwa maendeleo ya Dunia kwa kasi ya ajabu  iwapo kila nchi itajichukulia njia yake katika kulishughulikia janga hilo, imeionyesha dunia kweli Tanzania ipo mstari wa mbele katika kukabiliana na janga hilo" alisema Mama Kevela.

" Ukweli na hakika Rais Samia aliipangilia vizuri hotuba yake mbele ya Baraza hilo la Umoja wa Mataifa, ameanza na mguu sahihi ndani ya chombo hicho cha kimataifa hivyo kuonyesha ubora katika nafasi yake  kama kiongozi wetu katika Taifa hili" alisema Scolastika 

Mbali na hilo alisema hatua ya Rais Samia kugusia pia hatua anazochukua katika kumwezesha mwanamke kupanda katika ngazi mbalimbali za uongozi na hatimaye kufikia shabaha ya uwiano sawa na mwanamme ni jambo lililoonyesha dhamira yake ya dhati mbele  ya Baraza hilo la kutekeleza matakwa ya kufikia malengo ya mkutano wa Beijing uliotaka uwiano sawa wa 50/50 kati ya mwanamme na mwanamke. 

"Kwetu sisi wana Jumuiya ya UWT Mkoa wa Njombe amezidi kutufanya tuendelee kujivunua nafasi yake kama Rais wetu, mbali na mambo mengi na mazuri aliyoyafanya katika Taifa hili kwa kipindi kifupi tangu aapishwe amevuka na kwenda mipaka ya mbali kuionyesha Dunia kuwa Tanzania ni nchi ya namna gani" alisema Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono  Auction Mart

Aidha wao kama wana Jumuiya hiyo kutoka Njombe watasimama naye pamoja wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake na kusisitiza kuwa Mwaka 2025 watampa miaka mingine mitano ya kuliongoza Taifa kwa kaulimbiu yao ya 'Samia mitano tena'.

 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...