Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema kuwa asilimia 10 ya fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 zimeelekezwa katika miradi ya Maji.
Asilimia hizo 10 ni sawa na kiasi cha Sh Bilioni 139.4 ya fedha hizo zilizotolewa na IMF kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati akizungumza na wandishi wa habari kuelezea namna ambavyo miradi ya maji itanufaika na mgawanyo huo wa fedha za IMF.
Aweso amesema kiasi cha Sh Bilioni 104.2 zitaelekezwa katika eneo la kwanza la utekelezaji wa miradi 218 ya Maji, ambapo miradi 46 itatekelezwa mijini na mingine 172 ikitekelezwa vijijini.
" Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia kwa kutambua umuhimu wa Maji katika kuchochea ustawi wa jamii yetu katika maendeleo ya uchumi wa jamii yetu umeonelea kuelekeza kiasi hicho cha Sh Bilioni 104 kwa ajili ya miradi hiyo 218 mijini na vijijini.
Wote ni mashahidi namna Rais wetu amekua Balozi wa kuhakikisha anamtua Ndoo Mama hivyo niwahakikishie watanzania kwamba fedha hizi zitatumika ipasavyo katika kutekeleza miradi hiyo ya Maji Nchini," Amesema Waziri Aweso.
Amesema Serikali haitomvumilia mtu yeyote ambaye atajaribu kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo huku akiwataka viongozi wote wa wizara yake na Idara zilizo chini yake kuwa wakali kwenye usimamizi wa fedha hizo.
" Fedha hizi pia tumepanga kuhakikisha zinaelekezwa kwenye Kila Jimbo Nchini kwani tunatambua kuwa hakuna eneo lolote ambalo halikuathirika na ugonjwa wa Corona, hivyo tumepanga Kila Jimbo kuelekeza mradi unaogharimu Sh Milioni 500.
Lakini kama Wizara tumepanga pia kununua seti 25 ya mitambo ya kuchimba visima ambapo kila Mkoa utapata mtambo mmoja, lengo letu ni kukabiliana na uhaba wa vitendea kazi," Amesema Aweso.
Waziri Aweso amesema kuwa kiasi cha Sh Bilioni 17.6 zimeelekezwa katika kununua mitambo Mitano ya ujenzi ya ujenzi wa mabwawa na seti nne za vifaa vya kisasa vya utafiti wa Maji chini ya ardhi.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza na wandishi wa habari Ofisini kwake jijini Dodoma kuelezea mikakati ya wizara yake katika utekelezaji wa fedha za IMF kiasi cha Sh Bilioni 139.Sehemu ya wandishi wa habari na Watendaji wa Wizara ya Maji wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika mkutano wake na wanahabari jijini Dodoma.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisisitiza jambo mbele ya wandishi wa habari Ofisini kwake jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...