MKE wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, ameitaka jamii kuwaenzi waalimu kwani wanamchango mkubwa katika malezi ya watoto.
Mama Zainab ameyasema hayo kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wanafunzi wa Skuli ya Laureate waliofanya vizuri. Skuli hiyo ipo Chukwani, Wilaya ya Magharibi B, Unguja.
Mama Zainab amekumbusha jukumu muhimu la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuwa karibu na skuli za binafsi ili kuzisaidia kuinua viwango vya ufaulu kwenye mitihani ya taifa.
Kadhalika ameasa wazazi kote nchini kutoa ushirikiano kwa waalimu katika kuwapatia watoto elimu bora, kuwajenga kuwa na nidhamu, heshima na malezi yaliyotukuka.
“Tutakapokuwa na ushirikiano wa dhati na waalimu, tunachagiza kuwa na taifa lenye vijana waliojengwa kimaadili na kiutawala, sifa ambazo msingi wake hujengwa sasa," alisema.
Amesema njia mojawapo ya wazazi kuwa karibu ni kujitahidi kulipa ada za watoto wao kwa wakati pamoja na mara kwa mara kufuatilia maendeleo ya watoto wao maskulini.
"Mkiwa wazito wa kulipa ada mtakwamisha mipango ya skuli kuimarisha upatikanaji wa vitabu na kutengeneza miundombinu kwa ajili ya mazingira mazuri ya kufundishia," alisema.
Katika risala yao, uongozi wa Laureate umesema wingi wa kodi zinazolipwa serikalini ni moja ya mambo yanayozorotesha kasi ya maendeleo ya skuli hiyo, na akaiomba serikali kufikiria kupunguza kodi hizo ili kuzisaidia skuli binafsi kuongeza maslahi ya walimu ambao ni sehemu muhimu ya mafanikio yanayopatikana.
Kwa mujibu wa Mwalimu Asila Abdallah Nassor aliyesoma risala ya skuli mbele ya Mama Zainab, Laureate iliyoanzishwa mwaka 1996, kwa sasa inao wanafunzi 1,120 na inasifika kwa kutoa watoto wenye vipaji maalum kila mwaka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...