WATOTO wa kike nchini wametakiwa kuwa makini katika matumizi ya mitandao ya kijami kwa kuitumia kwa usahihi ikiwemo kujifunza na kujipatia manufaa yao ya kila siku.
Pia wazazi na Walezi wameaswa kuwalinda watoto hususani wa kike ikiwemo kuwasimamia katika matumizi ya mitandao hiyo ili kuweza kuwaepusha na madhara yanayoweza kuwasababisha kupata vitendo vya ukatili wa kimtandao.
Naibu waziri wa maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Mwanaidi Ally Hamisi, amesema hayo leo Oktoba 11, 2021 Jjini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Duniani, yaliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN-Women) yanayoadhimishwa Octoba 11 ya kila mwaka.
Amesema kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa la teknolojia duniani, kumekuwepo na matumizi yasiyokuwa sahihi ya mtandao na vitu vya kielektroniki ambavyo huchangia katika unyanyasaji na ukatili kwa watoto na vijana balehe
"Kumekuwepo na matumizi yasiyosahihi ya Mtandao pamoja na vifaa vya Kidigitali ambavyo vimekuwa vikichangia katika unyanyasaji wa ukatili kwa vijana na watoto wa kike.
Amesema, kauli mbiu ya mwaka huu inayosema 'Kizazi cha Kidigitali Kizazi chetu' ina kumbusha na kuimiza jamii kuwa dunia inapitia Mapinduzi makubwa ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano ambayo inawezesha na kutoa fursa mbalimbali za maendeleo na ustawi wa Kizazi kilichopo ambapo nusu ya watumiaji wake ni watoto pamoja na vijana.
Pia amebainisha kuwa, kuwa tafiti za awali nchini zinaonyesha, takriban watoto watano kati ya kumi wa shule za sekondari za mjini wanamiliki simu, nane kati ya kumi hutumia simu nyumbani na watano kati ya kumi wako mitandaoni huku utafiti unaonyesha ukatili wa mitandao hufanywa na watoto na watu wazima wasiowafahamu.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN-Women) Hodan Addou amesema ni muhimu wadau kwa pamoja kushirikiana kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi vitendo vya ukatili wa mitandaoni na kuhakikisha wanaitumia vizuri kwa mustakabari wa maisha yao ya badae
Naye, Sebastiani Kitiku, Mkurugenzi kutoka idara ya watoto Wizara ya afya amewataka watoto kuwa makini katika matumizi ya mitandao ikiwezekana kushirikiana mzazi au mlezi kunapoonyesha dalili za udhalilishaji wa kimtandao.
Pia Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Taifa , Nancy Aloyce ameiomba Serikali kuboresha huduma za Kidigitali ili mtoto wa kike aweze kushiriki kikamilifu kujifunza sambamba na kutoa elimu ya madhara ya kimtandao ili kuweza kuepukana na ukatili wa mitandaoni.
"Tunaiomba serikali itoe adhabu kali kwa watu wanaoshiriki kudhalilisha watoto wa kike kupitia mitandao"amesema
Aloyce amewaomba Wazazi na Walezi kutokufumbia macho vitendo vya ukatili na badala yake watoe taarifa kwa Mamlaka zinazohusika ili kuwaokoa watoto wa kike.
Kwa upande wao baadhi ya Watoto wa kike tuliozungumza nao wamewashauri wenzao kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya kusoma na kujifunza mambo mbalimbali.
Diana Christopher na Right Yohana ni wasichana ambao wako shule za msingi jijini Mwanza wameweza kubuni application ambazo zinasaidia wasichana kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia huku mwingine akitengeneza ya Daktari kiganjani mwako ili kuweza kupata taarifa za hospitalini kwa ujumla wamewashauri wenzao kuwa makini na mitandao.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiangalia baadhi ya shughuli zinazofanywa na vikundi vya wasichana katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike yaliyofanyika Jijini dar es salaam Leo tarehe 11/10/2021.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watoto Nancy Kasebo akipokea cheti cha umahiri katika uongozi wa Baraza la Taifa la watoto Tanzania, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike yaliyofanyika Jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya mtoto Sebastian Kitiku akizungumza na washiriki wa maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike Jijini Dar es salaam Leo tarehe 11/10/2021.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake (UN-Women) Hodan Addou akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya mtoto wa kike duniani iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake, (UN Women) Jijini Dar es Salaam. Siku ya mtoto wa kike duniani huadhimishwa Kitaifa Oktoba 11 ya kila mwaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...