TAASISI inayojishughulisha na utoaji elimu ya usafi na utunzaji wa mazingira ya 'Environmental Conservartion Community of Tanzania(ECCT) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa hotuba nzuri kuhusu hali ya mabadiliko ya Tabia nchi (COP) aliyoitoa mbele ya mkutano wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukizungumzia kuhusu suala hilo.
Katika hotuba yake hiyo iliyojaa hisia na umakini mkubwa imetafsiriwa na magwiji wa diplomasia kuwa ililenga kuyabeba mataifa yote ya Afrika huku akiongea kwa ujasiri mkubwa akitumia nafasi hiyo kuziasa nchi tajiri ambazo nyingi zinaongoza kwa kuchafua hali ya hewa ziwajibike zaidi katika vita hiyo.
Akizungumzia hatua hiyo Mkurugenzi wa ECCT Lucky Michael alisema hotuba ya Rais Samia siyo tu imeibeba Tanzania bali Bara zima la Afrika na kutokana na changamoto mbalimbali za mabadiliko ya tabia nchi inazozikabili nchi hizo.
"Tunapenda kumpongeza Rais Samia kwa kuonyesha uongozi thabiti na kuwa mstari wa mbele Kwenye jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, sauti yake katika mkutano wa COP26 sio tu imehimiza mataifa yaliyoendelea kutoa fedha na teknolojia kwa ajili ya utekelezaji wa mipango himili ya mabadiliko ya tabianchi, bali imetoa hamasa na hari kwa mataifa yote yanayoendelea kuendeleza jitihada katika vita hii ya mabadiliko ya tabia nchi" alisema Lucky.
Alisema kutokana na hilo wao kama taasisi, mashirika mengine yasiyo ya kiserikali na jamii yaliyojikita kwenye masuala ya mazingira, kwenye mabadiliko ya tabianchi kutumia fursa hiyo kuandaa miradi na programu mbalimbali zitakazotoa majawabu katika kukabiliana mabadiliko haya ya tabianchi.
"Rais Samia, hakupepesa macho, zaidi alisisitiza kuwa nchi tajiri sasa ziwajibike zaidi kwa kufadhili miradi ya kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi katika nchi zinazoendelea akimaanisha nchi zetu za Afrika, hivyo ni vyema nasi kwa nafasi yetu kama wadau kutumia fursa hiyo kuandaa miradi mbalimbali" alisema Lucky.
Alisema hotuba ya Rais Samia Ilikuwa ya kipekee sana katika kupaza sauti za mataifa yanayoendelea katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hasa alipoyataka mataifa hayo tajiri Duniani kutekeleza maazimio ya mkataba wa Paris ulizungumzia suala la mabadiliko ya tabia nchi.
"Raisi Samia ametaja vipaumbele vya Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi ambavyo ni pamoja na kupunguza makali ya mabadiliko ya tabianchi, kuhimili mabadiliko hayo sambamba na uchangiaji wa fedha kulingana na kiwango cha changamoto zilizoko hivi sasa, kwa hili anastahili pongezi kubwa" aliongeza Lucky.
Aidha alisisitiza kuwa hatua ya Rais Samia kugusia hali ya chafuzi wa hali ya hewa ambao sasa unatishia kutokea kwa milipuko ya magonjwa, ukame, njaa na mafuriko, unaochangiwa sana na nchi tajiri tokana na kuwa na viwanda vingi vikubwa vinavyozalisha hewa chafu ni jambo la kijasiri kwa kuwa limenga kutatua changamoto zilizopo katika nchi hizo.
Aidha alisema ni dhahiri kuwa Rais Samia alikuwa anaweka msingi wa ushirikiano wote wa kimataifa kuhusu mabadiliko hayo ya tabianchi kwa nchi za Afrika na hiyo ni kwa sababu COP26 ndicho chombo kikuu cha kufanya maamuzi cha kutekeleza Mkataba na vyombo vya ufuatiliaji katika masuala ya hali ya hewa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...