Na Mwandishi Wetu
Viongozi wa
kiimani waliopo kanda ya ziwa katika mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara wanaounda
jukwaa la kiimani kanda ya ziwa wamependekeza sheria zinazohusika na
kulisimamia baraza la kata zirekebishwe ili kuruhusu mabadiliko ikiwemo
kuondolewa kwa jukumu la kufanya maamuzi badala yake liishie kuwa chombo cha
usuluhishi.
Pendekezo hilo
limesomwa na Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa hili Sheikh Haruna Kichwabuta ambaye
ni shekh wa Mkoa wa Kagera alipokuwa anasoma taarifa iliyoandaliwa na Jukwaa
hilo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, William Lukuvi
walipokutana nae na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara ya Ardhi zilizopo
Mtumba Jijini Dodoma tarehe 03 Novemba mwaka huu.
Jukwaa La
Kiimani Kanda ya Ziwa baada ya kujadiliana limebainisha changamoto mbalimbali
zinazosababishwa na mabaraza haya ya kata ambayo ni pamoja na miingiliano ya kimamlaka
katika maamuzi, uelewa duni wa wajumbe juu ya masuala ya kisheria, upendeleo,
ukata, rushwa, siasa, sintofahamu juu ya usimamizi na uwajibikaji pamoja na
ukosefu wa ulinganifu wa kijinsia kwa wajumbe.
“Sheria ya
mabaraza ya kata inataja wajumbe wasiwe wanasheria na pia wajumbe hawatakiwi
kuwa watu wenye elimu kubwa wakati wanashughulikia maswala ya kisheria yenye
kuhitajiwatu wenye ufahamu wa kutosha kuzitafsiri sheria hizo na hivyo
kupelekea makosa yanayosababisha watu kupoeza haki zao” Alisema Shekh
Kichwabuta.
Kwa upande wake
Askofu Abednego Keshomshahara wa Kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania Jimbo
la Kaskazini Magharibi Bukoba alisema wamelazimika kujadili changamoto hizi
kwani hadi hivi sasa braza la kata linasimamiwa na mamlaka tofautitofauti na
hivyo kupelekea hali ya kutoeleweka nani ni msimamizi na pia anayepaswa
kuwajibika kwani katika maswala ya jinai baraza linasimamiwa na mahakama ya
mwanzo ila kwenye migogoro ya ardhi mabaraza yamekuwa yakisimamiwa na mabaraza
ya ardhi na nyumba ya wilaya.
Akipokea taarifa
ya mapendekezo ya Jukwaa hilo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.
William Lukuvi amesema changamoto hiyo serikali inaitambua na tayari muundo
unaandaliwa utakaowawezesha Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya
kuajiriwa kwa masharti ya kudumu mara baada ya kukamilika kwa miongozo na
taratibu za Utumishi wa Umma.
Aidha Mhe.
Lukuvi aliongeza kuwa hatua hiyo inatokana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kufanya marekebisho ya Sheria ambayo ilikuwa inaelekeza Wenyeviti hao
kuajiriwa kwa mkataba wa miaka mitatu.
‘‘Marekebisho
hayo yalifanyika ili kuondoa changamoto za mlundikano wa mashauri katika
Mabaraza ya Ardhi wakati wa kusubiri Mwenyekiti mwingine ateuliwe, na hayo
mambo ya rushwa yamejitokeza zaidi pale ambapo mwenyekiti hana uhakika wa
kubaki katika nafasi yake mara muda wake unapokwisha’’ alisema Mhe. Lukuvi.
Akielezea katika
mtazamo wa kisheria baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo cha
sheria Wizara ya Ardhi Michael Luena alisema ile dhana ya wajumbe kutokuwa
wanasheria ilitokana na kwamba wale walikuwa wanashauri kutokana na mila na
desturi za eneo husika, ila kutokana na kuendelea kukua kwa jamii, zimeibuka
hoja ambazo zinahitaji utaalamu wa sheria ambazo ni muhimu kuingizwa katika
maboresho ya kisheria kwani yapo upande wa kisheria.
Akiwashukuru
wawakilishi wa Jukwaa la kiimani Kanda ya Ziwa waliofika wizarani, Msajili wa
Mabaraza ya ardhi Stella Chaggi alisema baada ya kupata ujio wa jukwaa hili
wizara ililazimika kuwaalika na wadau wengine kutoka Wizara Sheria ya Katiba na
Tamisemi katika kuhakikisha makubaliano haya yanafanyiwa kazi katika sekta zote
husika.
Jukwaa hili limeundwa kwa ajili ya kuzishughulikia changamoto zilizopo kwenye jamii kwa kuzijadili pamoja na kutoa mapendekezo kwa Serikali. Kikao hiko kilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka TAMISEMI pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria ambapo Viongozi hao wa Jukwaa la Kiimani Kanda ya Ziwa waliwakabidhi taarifa yao iliyoonyosha changamoto na mapendekezo, yote hayo ikiwa ni jitihada za kuboresha utendaji kazi hasa katika ngazi ya Mabaraza ya Kata
Mhe. William Lukuvi akipokea taarifa ya changamoto na mapendekezo katika Mabaraza ya Kata kutoka kwa Mwenyekiti Mwenza Jukwaa la Kiimani Kanda ya Ziwa Sheikh Haruna Kichwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Jukwaa la Kiimani Kanda ya Ziwa, baadhi ya viongozi wa Wizara Ardhi pamoja na wawakilishi kutoka TAMISEMI na Wizara ya Sheria na Katiba
Askofu Dkt. Abednego Keshomshahara wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Jimbo la Kaskazini – Magharibi Bukoba akiwasilisha mapendekezo ya Jukwaa la Kiimani Kanda ya Ziwa katika kuboresha utendaji kazi wa Mabaraza ya Kata mbele ya Mhe. William Lukuvi
Mhe. William Lukuvi akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti Mwenza Jukwaa la Kiimani Kanda ya Ziwa Sheikh Haruna Kichwa akitoa ufafanuzi juu ya utendaji kazi wa Jukwaa hilo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...