Na Mwandishi Wetu.

MAANDALIZI ya mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon ambazo zinatimiza miaka 20 tangu kanzishwa kwake, yamefikia hatua nzuri huku waandaaji wakitoa wito kwa washiriki kutoka Kanda ya Kaskazini wajisajili mapema kuepuka usumbufu dakika za mwisho.

Wito huo umetolewa kutokana na uzoefu wa miaka ya mnyuma ambapo washiriki kutoka kanda hiyo ya kaslkazini ambayo ndio mwenyeji wa mbio hizo,  wamekuwa wakisubiri hadi dakika za mwisho ili wajisajili jambo ambalo huwaacha baadhi na masikitiko baada ya kukuta namba zote zimeshauzwa.

“Tunatoa wito kwa washiriki kutoka Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara kujisajili kwa njia ya mtandao kupitia Tovuti yetu Au kwa njia ya Tigopesa kwa kupiga *149*20#,” alisema Aggrey Marealle ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Executive Solutions, waratibu wa mbio hizo kitaifa.

Alisema mbio hizo za mwakani zinategemewa kuwa kubwa zaidi kwa sababu itakuwa ni mwaka wa 20 tangu kuanzishwa kwake kwa hivyo washiriki wana kila sababu ya kujisajili na kuhakikisha wanathibitisha ushiriki wao kwa kujisajili.

“Huwa inasikitisha sana kuona washiriki kutoka Moshi au Arusha wanakosa namba wakati wanatokea katika kanda mwenyeji wa mbio hizi. Namba zikishaisha usajili huwa unafungwa. Kwa kawaida hakuna namba zinazouzwa katika vituo vya kutolea namba isipokuwa tu kwa mbio za KM 5 kama zitakuwa zimebakia,” alisema.

Alisema kujisajili ni rahisi mno na kwa sasa kuna punguzo la bei la asilimia 20 lakini ifikapo Januari 7, 2022 bei zitapanda kwani hakutakuwa na punguzo tena.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa mbio hizo, Bw. John Bayo alisema washiriki wote wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager 42km , Tigo 21km na Grand Malt 5km waanze mazoezi mapema ili wajiandae na mbio hizi za 20 za Kilimanjaro Marathon ambazo ni za kihistoria.

“Tunataka mbio hizi ziwe za ushindani zaidi na ziache kumbukumbu ya aina yake miongoni mwa washiriki kwa hivyo maandalizi ni muhimu sana. Ni matumaini yetu kuwa zawadi nyingi zitabaki hapa nyumbani safari hii. Kama waandaaji tutafanya sehemu yetu  na tunatoa wito kwa washiriki wafuate maelekezo ili kufanya mbio za mwakani ziwe za kufana zaidi kwani tunatarajia washiriki kutoka nchi zaidi ya 55 na umati unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi kuliko miaka ya nyuma,” alisema.

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania Bw. Jackson Ndaweka alisema wameridhishwa na maandalizi hadi sasa kwani wamekuwa wakipokea taarifa kutoka kwa waandaaji wa Kilimanjaro Marathon.

“Hili ndio tukio kubwa kabisa la riadha nchini ambalo huwaleta pamoja zaidi ya washiriki 12,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa maana hiyo tunashirikiana na waandaaji kwa karibu kuhakikisha mbio hizi zinafanikiwa na zinaweka riadha ya Tanzania katika kiwango cha kimataifa. Wanariadha wa hapa nchini hujipatia kipato kwa kushiriki mbio hizi lakini pia huwandaa vizuri katika mashindano ya nje ya nchi.Mbio hizi pia zinachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la nchi kwa sababu ya watalii ambao hutembelea vivutio mbalimbali,” alisema.  

Alisema RT pia imefarajika kusikia kuhusu maonesho yaliyoandaliwa na wandaaji wa Kilimanjaro Marathon kama sehemu ya madhimisho ya miaka 20 ya mbio hizo. “Maonesho hayo yatatoa fursa nzuri kwa wadhamini kujitangaza vizuri na pia wananchi watapata maelezo mengi kuhusu Kili Marathon na riadha kwa ujumla. Tutakuwepo kutoa mchango wetu katika suala hili,” alisema.

Wadhamini wa Kilimanjaro Marathon  2022 ni Kilimanjaro Premium Lager- 42km, Tigo- 21km, Grand Malt -5km wadhamini wa meza za maji ni Absa, Unilever, TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, na wasambazaji maalumu Kilimanjaro Leather Industries Company Limited, GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel na CMC Automobiles.

Mbio za mwakani zitafanyika katika Chuo Kikuu Cha Ushirika Moshi Februari 27, 2022.

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon huandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa kitaifa na kampuni ya Executive Solutions Limited.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...