Mwenyekiti
wa Kikundi cha Kikoba cha Malkia Ladies Group, Charity Mwakalonge ( wa
pili kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salam leo
wakati akitangaza Uzinduzi pamoja na kongamano la kikundi hicho
utakaofanyika Jumamosi hii tarehe 20, 2021 katika ukumbi wa PTA
Sabasaba. Mkutano huo mkuu unategemea kupokea wanawake zaidi ya 6,000.
Kutoka Kushoto ni Mwanamuziki wa Muziki wa Dansi, Aneth Kushaba,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji, Chevawe Mberesero na Kaimu Mwenyekiti
Kamati ya Jamii, Husna Mkupete.
Kikundi
cha Kikoba cha Malkia Ladies Group kinawakaribisha wanawake wote popote
walipo kuhudhuria kwenye Tamasha kubwa la kikundi hicho chenye makazi
yake jijini Dar es Salaam. Mkutano huo mkuu utafanyika Jumamosi hii
tarehe 20, 2021 katika ukumbi wa PTA Sabasaba na unategemea kupokea
wanawake zaidi ya 6,000.
Hakuna
kiingilio bali mtu yeyote anakaribishwa. Labda mtajiuliza Malkia ladies
ni akina nani? Ni kikundi cha Kikoba kilichosajiliwa na Benki kuu ya
Tanzania chenye lengo la kuwasaidia wanawake wengine kupitia elimu ya
fedha yaani uwekaji wa akiba na pia uwekezaji kwa maendeleo yao wenyewe
na familia zao. Kwa sasa wajumbe wa Malkia ladies Group wapo 34 na
mzunguko wao wa fedha unafikia zaidi ya milioni 250 kwa mwaka, hii
imetokana na kikundi hiki kuwa na nidhamu ya uwekaji akiba na pia kuanza
kuwekeza kupitia fursa mbalimbali, sasa kina kuja na program maalumu ya
kusaidia wanawake wengine kuanzisha vikundi kama hivi na kuvikilea ili
kuja kuwa vikubwa na mwisho kuleta matokeo chanya ndani ya chama
chenyewe na taifa kwa ujumla.
Siku
ya Jumamosi tarehe 20, wanakaribishwa wanawake wengine wanaotaka
kujifunza namna bora ya kuanzisha vikundi na pia kujifunza namna ya
kuendeleza vikundi vyao ili vilete tija miongoni mwao. Siku hiyo
watazindua rasmi kikundi cha Malkia pamoja na uzinduzi wa kampuni ya
Bima (Insurance) ambayo itaanza kutoa huduma hivi karibuni, pamoja na
kuzindua Ramani ya Malkia women market Mall yenye maduka Zaidi ya 100
ili kuwapa wanawake sehemu ya kuuzia bidhaa zao, mwisho watazindua
Kitabu cha fursa 50 pamoja na Youtube Channel inayoitwa (Malkia Ladies
TV) ambayo itakuwa chachu ya akina mama kupata elimu ya masuala ya
vikundi na uwekezaji. Malengo yao ni kusaidia wanawake wenzao kupitia
Biashara kwani wanategemea kwa watakao hudhuria na kuanzisha kikundi
chao, watachagua vikundi vitatu kwa kuanzia ili tuvilee vifikie kiwango
kikubwa kuliko hata chao
Mgeni
rasmi wa uzinduzi huu ulio katika mfumo wa kongamano ni Mheshimiwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (mb) atakayeambatana na Mlezi wao Rais
mstaafu wa bunge la Africa Mh Getrude Mongella wanategemea kuwapokea
wanawake wote wanaotaka kupata elimu ya vikundi na pia wanaotaka
kuanzisha vikundi vyao waje wasikilize na wanaimani hawataondoka kama
walivyokuja, wataondoka na kitu kikubwa sana cha kujenga na kubadilisha
Maisha yao. Kauli mbiu ya Mkutano huo wa jumamosi ni “Mwanamke ni Nguzo
ya Uchumi, Amka Uwekeze.”
Wanawaomba
wanawake wenzao popote walipo, karibuni kwenye ukumbi wa PTA SabaSaba
jumamosi kuanzia saa mbili kamili asubuhi. Pia kutakuwa na burudani
mbalimbali kutoka kwa Msanii Peter Msechu, Aneth Kushaba na The Star
Band. Mada mbalimbali zitatolewa kutoka kwa watu maarufu kama Aunt
Sadaka atakayeteta na wanawake wote watakao hudhuria siku hiyo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...