Na John Walter-Manyara
Dunia ikiwa katika mapambano dhidi ya Ukatili wa kijinsia, klabu ya waandisi wa habari ya mkoani Manyara imeendelea kupaza sauti wakionesha kutofurahishwa na ukatili wanaofanyiwa Wanawake na wasichana huku wakiiomba serikali kufuata sheria pale mtuhumiwa anapo kamatwa na kufikishwa mahakamani, kwa makosa ya ukatili dhidi ya watoto wa kike.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Riroda wilayani Babati wanasema awali walikuwa hawajui pa kuelekea baada ya kukumbana na vitendo vya kikatili wakiamini kuwa kupitia vikao vya kifamilia ndo ilikuwa suluhisho la mwisho, ila baada ya kupatiwa elimu ya uzazi na namna ya kupinga vitendo vya Ukatili wanajua ni wapi wanapaswa kuelekea kutoa taarifa.
Mmoja wa wanufaika katika mradi huo ni Maria Nicodemus ambaye alitelekezewa watoto watatu, anasema tangu apate elimu kutoka kwa Klabu ya waandishi wa Habari Manyara kupitia wataalamu kwenye mradi wa haki ya afya ya uzazi unaofadhiliwa na taasisi ya Women Fund Tanzania Trust (WFT) ameona mwanga kwani mume wake ameanza kutoa matumizi kwa watoto mara baada ya kumripoti kwenye dawati la jinsia wilayani humo.
Awali Maria alisema alikuwa akikosa furaha ya maisha kutokana na mume wake ambaye walishaachana lakini kutokan n elimu kwa sasa anaendelea na shughuli zake zaa kiujasiriamali ili aweze kujikimu yeye na watoto wake.
"Kwa sasa mume wangu japo hatujarudiana huwa nawasiliana nae ila anajaribu angalau kidogo lakini bado haeleweki, kunifuatilia ndo kitu ambacho amekipunguza,hajionyeshi sana" alisema Maria
Mkazi mingine wa Riroda Salome Benedict anasema huduma za ustawi wa Jamii zikisogezwa karibu itawasaidia wengi kueleza madhila wanayoyapitia katika familia zao na kwenye jamii.
Anasema wapo watu katika maeneo yao hufanyiwa vitendo vya kikatili lakini hawana namna ya kuripoti na kuishia kubaki na makovu na maumivu moyoni.
Afisa Ustawi wa jamii Halmashauri ya wilaya ya Babati Mathias Focus amesema ofisi yake inafanya kila njia kuwasikiliza wahanga wa matukio ya ukatilo katika maeneo yao kwa kutumia viongozi wa vijiji na kata na wakati mwingine yeye mwenyewe hulazimika kufika katika maeneo husika.
Focus amewataka wananchi waripoti katika ngazi ya kijiji au kata pindi wanapokuwa na dukuduku ili hatua zichukuliwe kwa wahusika na kukomesha Ukatili.
Amesema serikali imepunguza changamoto hiyo kwa kuanzisha mabaraza ya wazee na kamati mbalimbali ambazo wakiwemo wataalamu wa afya ambao wamefundishwa mbinu za kutoa taarifa za Vitendo vya kikatili vinavyotokea katika maeneo yao.
Katibu wa Klabu ya waandishi mkoa wa Manyara Jaliwason Jasson amesema lengo lao kuu ni walengwa wa mradi huo waweze kufanyia kazi elimu wanayopatiwa na wataalamu kwa kutumia uzazi wa mpango na kuripoti ukatili wanaofanyiwa.
Jasson wanaishukuru serikali kwa namna ambavyo wanaonyesha ushirikiano katika vita hivyo kwa kuwapatia wataalamu wa afya na wa ustawi katika kufikisha elimu kwa kundi hilo walilolilenga.
Kwa upande mwingine ameishukuru WFT kwa kuwezesha kutoa fedha za kufadhili mradi huo huku wakiwaomba waendelee kuwawezesha zaidi hata pindi mradi huo utakapokamilika kwa kuwa elimu haina mwisho.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...