*Asisitiza wanawake kupewa kipaumbele

Na Mary Gwera, Mahakama
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu amekutana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kufanya naye mazungumzo ambapo ameiomba Mahakama nchini kuendelea kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki za wanawake katika suala la utoaji haki.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika tarehe 16, Novemba 2021 ofisini kwa Jaji Mkuu Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Bi. Pangestu alimweleza Jaji Mkuu kuwa, haki za wanawake ni muhimu kuzingatiwa kwa kuwa wengi wanateseka kwa kutojua haki zao.

“Ni muhimu kutoa kipaumbele kwa wanawake katika jamii ili waweze kutambua haki zao na taratibu mbalimbali za kisheria na jinsi ya kuzitumia kwa kuwa wengi wanateseka kwakuwa hawajui cha kufanya katika kutafuta haki zao,” alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha, Bi. Pangestu alitoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma zake kufuatia Mradi wa Uboreshaji wa huduma za Mahakama uliofadhiliwa na fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuendelea na uboreshaji wa huduma za Mahakama kuwafikia wananchi wengi.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mtendaji huyo alibainisha kuwa uwazi na uwajibikaji ni vitu muhimu vitakavyoiwezesha Mahakama kuendelea kuwa karibu na wananchi.

“Uwazi na uwajibikaji ni vitu muhimu katika utawala wa sheria, suala hili limekuwa tatizo katika nchi nyingi, ila nina uhakika mmepata uzoefu katika utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa huduma za Mahakama mmeweza kuwafikia wananchi hivyo ni muhimu kuendeleza vitu hivi ili Mahakama iendelee kuaminika kwa makundi yote ya jamii,” alisema Bi. Pangestu.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa kipaumbele na ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia Serikali ya Tanzania Mahakama ilipata fedha za mkopo kutoka benki hiyo zilizowezesha kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano 2015/2016-2019/2020 na kuomba kuendelea kutoa ushirikiano utakaowezesha utekelezaji wa Mpango wa pili wa uboreshaji wa huduma za Mahakama wa 2020/2021-2024/2025.

“Ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania umeleta faida kwa Mahakama ya Tanzania, ni Mahakama chache duniani zinazopata aina ya ushirikiano huo hivyo Mahakama ya Tanzania inakiri kutoangusha ushirikiano huu kwa kuendelea kuboresha huduma zake,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania imebadilika katika utoaji wake wa huduma katika maeneo ya uwajibikaji, uwazi, upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi, kubadilisha mitazamo na fikra hasi kwa Mahakama na kuwa na mifumo ya ufuatiliaji na uwajibishwaji.

Katika ziara yake fupi ndani ya Mahakama, Mkuu huyo wa Benki ya Dunia alipataa wasaa wa kutembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke (One stop centre for Probate and Family Matters), alipata maelezo ya huduma za Mahakama inayotembea ‘mobile court services’ na mwisho alipokea taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho wa huduma za Mahakama wa mwaka 2015/2016-2019/2020, iliyowasilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mhe. Zahra Maruma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu. Bi Pangestu alimtembelea Mhe. Jaji Mkuu tarehe 16 Novemba, 2021 ofisini kwake Mahakama ya Rufani, Dar es Salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza jambo na baadhi ya Viongozi wa Mahakama na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia walioambata na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia na sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu, wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Bi. Mara Warwick.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia na sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania, wa tatu kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu, wa tatu kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, aliyesimama nyuma ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na wa tatu kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia-Tanzania, Bi. Mara Warwick na Maafisa wengine kutoka Mahakama na Benki ya Dunia walioshiriki katika mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Juma na Mkurugenzi huyo.

Jaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mhe. Zahra Maruma (wa pili kulia) akitoa maelezo ya huduma zinazotolewa na Mahakama inayotembea 'mobile court services' wakati Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia, Bi. Pangestu (kushoto) alipotembelea Mahakama hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu akishuka kutoka kwenye Mahakama inayotembea, ameonyesha kufurahishwa na huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo.
Bi. Pangestu akifurahia Mahakama inayotembea.
Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta (kulia) akimueleza jambo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayeshughulikia Maendeleo ya Kisera na Ushirikiano, Bi. Mari Pangestu wakati Mkurugenzi huyo alipotembelea kituo hicho cha Mahakama kilichoanza kutoa huduma hivi karibuni.

Ukaguzi wa moja ya kumbi za Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke wakati Bi. Pangestu alipotembelea Mahakama hiyo.

Jaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mhe. Zahra Maruma akiwasilisha mada ya kwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia (hayupo katika picha)

Picha ya pamoja mbele ya jengo la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke wakati Bi. Pangestu alipotembelea Mahakama hiyo.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...