Na. Damian Kunambi, Njombe


Baraza la madiwani wilayani Ludewa mkoani Njombe limemtaka mkurugenzi wa halmashauri kuliandikia barua ya wito shirika la maendeleo ya Taifa (NDC) ili waweze kukutana na baraza hilo na kujadili juu ya uendeshwaji wa miradi mbalimbali ya makaa ya mawe pamoja na chuma.

Wakizungumza katika kikao cha baraza hilo cha robo ya nne ya mwaka 2021/2022 madiwani hao wamesema halmashauri inakosa mapato ya kutosha huku ikiwa na miradi mikubwa ya makaa ya mawe na chuma hivyo ni vyema NDC wakaachia baadhi ya maeneo ili wawekezaji na wachimbaji wadogo wadogo waweze kuifanyia kazi.

Hoja hiyo iliibuka baada ya mwenyekiti wa kamati ya Fedha, uongozi na mipango Leodga Mpambalioto kusoma taarifa ya fedha iliyoonyesha nia ya kamati hiyo ya kutaka shirika hilo kuitwa.

 Katika hoja hiyo diwani wa kata ya Ruhuhu Athanas Haule alisimama na kusema kuwa NDC wanarudisha nyuma maendeleo ya wilaya ya Ludewa kwani wanahodhi vitalu vya madini pasipo kuviendeleza hivyo ni vyema wafike katika baraza hilo na kutolea maelezo.

"Haiwezekani wilaya yetu iwe nyuma kwa maendeleo huku vyanzo vya mapato vikiwepo ni lazima NDC waje la sivyo tuwe na uwezo wa kuwanyang' anya hivyo vitalu", amesema Haule.
Wise Mgina ni mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na pia ni diwani wa kata ya Mundindi amesema wawekezeji wamekuwa wakija kwa lengo la kuwekeza lakini shirika hilo limekuwa likiweka vikwazo.

Amesema endapo NDC ingeachia baadhi ya maeneo hayo halmashauri ingepiga hatua kimaendeleo kwani wangekutana na wawekezaji wa ndani wanaoweza kufanya kazi kwa wakati wakiwemo wawekezaji wadogo wadogo na halmashauri hiyo ingeongeza mapato.

" Tunahangaika na fedha za maboresho mbalimbali kama madarasa, nyumba za watumishi, vituo vya afya na nyinginezo wakati tungekuwa na miradi hiyo tungeweza kuendesha halmashauri yetu kwa urahisi zaidi", Amesema Mgina.

Aidha kwa upande wa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias amesema halmashauri yake inaonekana haina mapato lakini inavyanzo vingi ambavyo havijaanza kukusanywa kama makaa ya mawe, chuma ambavyo vimekaa kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi.

Amesema tayari alishawaandikia barua ya kufika kwenye baraza hilo na aliendelea kuwasiliana nao wakaahidi kufika lakini mpaka siku moja kabla ya baraza aliendelea kufanya mawasiliano hayo na hakukuwa na mrejesho wowote.

Ameongeza kuwa atawaandikia tena barua sambamba na kumuomba mkuu wa wilaya Andrea Tsere ili aweze kuweka mkazo zaidi na waweze kufika.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa ambaye pia ni diwani wa kata ya Mundindi Wise Mgina akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2021/2022

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2021/2022

Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Ludewa wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao cha baraza hilo cha roba ya nne ya mwaka 2021/2022

Wakuu wa idara pamoja na wananchi wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...