MAKAMU Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuongeza kasi ya ubunifu ili kutoa huduma kwa kiwango cha kimataifa na kuhimili ushindani wa biashara ya fedha duniani.
Mhe. Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, jijini hapa alipokutana na uongozi wa PBZ, uliofika kujitambulisha na kushauriana naye juu masuala mbali mbali kuhusu maendeleo ya Benki hiyo.
Amesema hivi sasa hapa Zanzibar zipo Benki nyingi zinazofanya kazi ya utoaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wa ndani na wageni, jambo ambalo linaweza kuongeza kasi ya ushindani na kuwavutia wateja wengi zaidi pindipo kutakuwepo na ubunifu wenye ufanisi.
Aidha Mhe Makamu amesema kwamba pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na uongozi wa Benki hiyo kuimarisha huduma, lakini bado zipo changamoto mbali mbali zikiwemo za urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wateja wake pamoja na kuwepo mifumo ya kisheria ndani ya benki hiyo inayohitaji kufanyiwa marekebisho ili kwenda na wakati wa ushindani wa biashara hiyo.
Alishauri Uongozi wa PBZ kufanya marekebisho katika baadhi ya sheria ili kuimarisha taratibu zinazosimamia benki hiyo kwa nia ya kuweka mfumo bora zaidi wa utoaji wa huduma na kusaidia kuwavuta zaidi wateja wake kuendelea kuitumia Benki hiyo .
Ameutaka Uongozi wa Benki hiyo kuendelea kuitumia fursa ya Uzalendo wa Wananchi na Wafanyabiashara wa Zanzibar kuendelea kuipenda Benki yao kwa kupata huduma bora za Kibenki zitakazowaridhisha ili waendelee kuiamini kwamba ni benki bora.
Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Dk. Muhsin Suleiman Masoud, amesema kwamba pamoja na changamoto mbali mbali zilizopo katika Benki hiyo, lakini wamepokea ushauri huo na watajitahidi kuimarisha utoaji wa huduma bora ili kwenda na wakati na kuhimili ushindani.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema kwamba licha ya Benki hiyo kupitia katika kipindi kigumu, lakini bado ipo vizuri na inaendelea kuimarika na wateja wengi wanapenda kutumia huduma za Benki hiyo.
“Hivi karibuni Benki yetu itaendelea na zoezi la kufungua matawi mapya katika mikoa kadhaa ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kuongeza mawakala hadi 800 kutoka 200 waliopo sasa” Alieleza Dk. Muhsin.
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Dk. Muhusin Suleiman Masoud na kulia kwa Mkurugenzi ni Meneja wa Benki hiyo Said Ali Mwinyigogo. Mkurugenzi huyo na ujumbe wake ulifika Ofisini kwa makamu leo kujitambulisha na kushauriana kuhusu masuala mbali mbali ya Benki. ( Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar).
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman, akizungumza na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Dk. Muhusin Suleiman Masoud(kulia kwa makamu). Mkurugenzi huyo na ujumbe wake ulifika Ofisini kwa makamu leo kujitambulisha na kushauriana kuhusu masuala mbali mbali ya Benk hio.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...