MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) umetoa wito kwa Wanachama na Wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa ya huduma ya kuwawezesha kumiliki nyumba kwa kulipa kidogokidogo na hivyo kuboresha maisha yao.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa Mfuko huo, Beatrice Musa-Lupi aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wakati wa ufunguzi rasmi wa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Novemba 10, 2021 ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Anayeshughulikia masuala ya Fedha na Mipango) Mhe. Jamal Kassim.
Akifafanua kuhusu umiliki huo Lupi alisema PSSSF na Benki ya Azania wanayo makubaliano yanayowawezesha wananchama na wananchi kukopa kutoka benki hiyo kupitia mikopo ya makazi yaani (Mortgage loan) ili kununua nyumba na viwanja vinavyomilikiwa na PSSSF kama vile nyumba za makazi za Buyuni jijini Dar es Salaam.
“Tunashirikiana na wenzetu wa benki ya Azania, mwanachama na asiye mwanachama anakaribishwa kwenye banda letu hapa Mnazi Mmoja atakutana na maafisa wa Mfuko ambao wako tayari kutoa huduma na kuwapa elimu kuhusu majukumu ya Mfuko lakini pia elimu ya fedha kuhusu jinsi Mwanachama au Mwananchi atakavyoweza kununua nyumba hizo kupitia mkopo kutoka benki ya Azania kwa masharti nafuu.” Alifafanua Mkurugenzi huyo wa fedha wa PSSSF.
Kama ambavyo kauli mbiu ya Wiki hiyo inavyosema “Boresha Maisha Kupitia Elimu ya Fedha, PSSSF ni miongoni mwa taasisi za fedha iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa na jukumu la Hifadhi ya Jamii.
“Hifadhi ya Jamii ina majukumu mengi ikiwemo Kusajili Wanachama, Kukusanya Michango, Kuwekeza kwa mujibu wa Sheria lakini pia kulipa Mafao mbalimbali kwa Wanachama na kwa kupitia uwekezaji tunaamini elimu tunayoitoa hapa itawawezesha wanachama na wanachi kutambua fursa zilizopo na hivyo kuboresha maisha yao binafsi na hivyo kuchangia pato la taifa.” Alisema


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...