Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 04 Novemba, 2021 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea Glasgow, Scotland alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26).
Katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Aidha, Mhe. Rais Samia
amefanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Tanzanite
linalojengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Samia amepokea
maelezo ya ujenzi wa daraja hilo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara
nchini TANROADS Mhandisi Rogatius Mativilla ambaye amesema ujenzi wa daraja
hilo umefikia asilimia 98.44.
Mhandisi Mativila amesema
daraja hilo litakapokamilika litapunguza msongamano wa magari, ajali bararani, litaboresha hali ya maisha
Jijini Dar es Salaam pamoja na
kupendezesha jiji la Dar es Salaam na kuwa sehemu moja wapo ya kivutio cha
utalii katika fukwe zilizopo karibu na daraja hilo.
Wakati
huohuo, Mhe. Rais Samia
amefanya ziara katika eneo la Coco Beach ili kuona agizo lake la kutaka
wafanyabiashara wadogowadogo kupangwa vizuri katika mazingira bora ya kufanya
biashara linavyoendelea kutekelezwa.
Aidha, Mhe. Rais amesema
ziara hiyo pia imemuwezesha kuona hali halisi ya athari za mabadiliko ya
tabianchi katika fukwe za Coco beach na kusema kuwa Serikali itaangalia upya
namna ya kuzuia athari hizo.
Mhe. Rais Samia amesema
kuwa Serikali itaendelea kuwajali wafanyabiashara wadogo wadogo na kutolea
mfano eneo hilo ambalo wafanyabiashara wakubwa walilitaka lakini Serikali ilikataa
kwa kujali maslahi ya wafanyabiashara wadogo ili waendelee kukuwa na kujipatia
kipato.
Pia, Mhe. Rais amesema
Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara
wadogo ambao itabidi kuzirejesha ili kuwezesha wengine kupata mikopo hiyo na kuendeleza
biashara zao.
Mhe. Rais Samia amesema
zoezi la lengo la kuwapanga wafanyabiashara wadogo wadogo mijini ni zuri ambalo
limelenga kuwaboreshea mazingira yao ya biashara, kuweka miji katika hali ya
usafi pamoja na kuimarisha usalama.
Vilevile Mhe. Rais Samia
ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango Pamoja na TAMISEMI kuanza mara moja ujenzi
wa Soko Kuu la Kariakoo kwasababu tayari Serikali imepata fedha kiasi cha zaidi
ya Sh. Bilioni 34 ambapo ujenzi huo utahusisha soko la zamani na kujenga
mengine mawili mapya ya kisasa mkabala na soko la zamani la Kariakoo na kujenga
soko jingine jipya katika eneo la Jangwani Jijini Dar es Salaam.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Tanzanite linaloendelea kujengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021. Kulia ni mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatius Mativila.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatius Mativila kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Tanzanite linaloendelea kujengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wafanyabiashara wadogowadogo katika eneo la Coco Beach Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na wafanyabiashara wadogowadogo katika eneo la Coco Beach Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohammed Gharib Bilal alipomtembelea kumjulia hali nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam leo tarehe 04 Novemba 2021.
Ujenzi wa Daraja jipya la Tanzanite (Tanzanite) lenye urefu wa mita 1030 limefikia asilimia 98.44 na linatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba 2021. PICHA NA IKULU
Mandhari ya eneo la fukwe la Coco Beach ambapo wafanyabiashara wamejengewa Vibanda vya biashara
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...