Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla amesema kuwa katika kutekeleza zoezi la kuwapanga Wafanyabiashara wadogo maarufu Wamachinga, baadhi ya Wanasiasa walitaka kuvuruga zoezi hilo lililokuwa linatekelezwa sehemu mbalimbali za mkoa huo wa Dar es Salaam.
Makalla ameyasema hayo wakati akikabidhiwa mradi wa Soko wenye lengo la kuwawezesha Wafanyabiashara wadogo kujikwamua Kiuchumi, katika eneo la Kigogo, mradi unaotekelezwa na Kampuni ya Coca Cola Kwanza Ltd.
Makalla amedai baadhi ya Wanasiasa hao walitoa matamko ya kupotosha kuhusu zoezi hilo la kuwapanga Wamachinga katika maeneo yalipangwa na Serikali, amesema walitaka kutoa dosari ili kufanikisha azma yao ya kuzuia zoezi hilo lisitekelezwe kiufanisi na Mkoa wa Dar es Salaam.
“Sasa hivi hali imebadilika pale Kariakoo, watu walikuwa wanapata ajali kila siku, kutokana na uwepo wa njia ndogo, haswa wale wanaotumia njia za miguu. Leo tunazungumza eneo la Kariakoo ni salama watu wanapita bila tatizo lolote, mji wetu tumeupanga vizuri na safi”, amesema Makalla.
“Wafanyabiashara wadogo waliorudi kwenye maeneo waliyotolewa, niwaombe mrudi kwenye maeneo mliopangiwa kufanya biashara zenu, kwa sababu zoezi la kuwapanga ni endelevu kwa mkoa wote wa Dar es Salaam”, ameeleza Makalla.
Makalla ameishukuru Kampuni ya Coca Cola Kwanza kuwezesha mradi huo utakaokidhi idadi ya Wajasiriamali 100 kufanya biashara zao kwenye eneo hilo. Pia amewaasa watumiaji wa maeneo hayo kwa ajili ya biashara kuchangamkia fursa ya biashara kutokana na ufadhili wa Kampuni mbalimbali.
Pia Makalla ametoa siku saba kwa Wakandarasi wa mkoa wa Dar es Salaam kufika katika eneo hilo na kuboresha zaidi kutokana na nafasi kubwa ya kutosha kwa ajili ya Wafanyabiashara hao, amesema ataomba Mamlaka husika kuelekeza Mabasi ya abiria maarufu Daladala kutumia njia hiyo kama Kituo chao ili kuchangamsha eneo hilo kibiashara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...