Na John Walter-Hanang
WAZIRI Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye ametahadharisha tabia ya wanasiasa kutumia kipindi cha siasa Wilayani Hanang kuingilia na kuharibu mshikamano uliopo kati ya wananchi na serikali hali inayopelekea kukwamisha maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujitoa kwa michango mbalimbali inayoanzishwa na serikali.

Sumaye ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa wiki ya maendeleo ya wilaya ya Hanang ambayo imehusisha wadau mbalimbali ikiwa na lengo ya kuchangisha pesa na vifaa vingine vitakavyowezesha kuifanyia ukarabati hospitali ya wilaya ya Hanang (TUMAINI) na Miundombinu mingine.

Amesema kuwa wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakiingilia na kukwamisha mipango mbalimbali ya serikali na kurudisha nyuma muamko wa wananchi kujitoa kuchangia shughuli za maendeleo yao.

Sumaye amesifu jitihada za mkuu wa wilaya hiyo katika kuanzisha wiki hiyo ya Maendeleo ambayo imeonesha muitikio mkubwa kwa makundi mbalimbali ya watu kujitokeza kutoa michango yao ya fedha na vifaa wakiwemo wafugaji, wafanyabiashara,taasisi za Kidini na mashirika binafsi.

Katika kuunga mkono juhudi za mkuu wa wilaya, Waziri mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye ambaye ndiye mbunge wa kwanza wa jimbo la Hanang ameahidi kutoa shilingi Milioni tano ili kuikarabati Hospitali ya Tumaini ambayo ina miaka Zaidi ya ishirini na haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Mkuu wa wilaya ya Hanang Janeth Mayanja akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki hiyo ya maendeleo amesema mpaka sasa tayari ameshapokea mifuko ya Saruji Zaidi ya 1000.

Mayanja amesema alichojifunza ni kwamba wilaya ya Hanang ni wilaya ambayo Mungu alipanga yeye akafanye kazi kwa kuwa wamempokea vizuri na kumpa ushirikiano katika kila jambo hivyo ameahidi kuendelea kuwatumikia kwa nguvu zake zote.

Mbali na hayo mkuu wa wilaya amesema ataendelea kufanya ziara katika kata na vijiji vya wilaya hiyo kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ili wananchi waendelee na shughuli za maendeleo na sio malumbano.

“Mimi nina utaratibu linalowezekana nitakwambia linawezekana na lisilowezekana nitakwambia haliwezekani ili kuwapunguzia usumbufu wananchi kutembea ofisi za Umma”alisisitiza Mayanja

Wiki ya maendeleo wilayani Hanang imeanza novemba 1,2021 ikifunguliwa na Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na itahitimishwa Novemba 5 na mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...