Makamu wa Kwanza wa rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, akizungumza na Kamati ya Kidumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia masuala ya Ukimwi, Dawa za kulevya, Kifua Kikuu na maradhi yaasiyoambukiza huko ofisini kwake Migombani leo. Kulia kwa Mhe. Makamu ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Hassan Taufiq, Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Asia Msangi na Dk. Stev Kiruswa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati. Kushoto kwa Mhe, Makamu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Dk. Saada Mkuya Saluma na Mbunge wa Mtambwe Khalifa Mohammed Issa.
(Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar)
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema ni muhimu kwa Taasisi na Mamlaka zote zenye jukumu la kupambana na dawa za kulevya Tanzania kujifunza na kutambua ujanza na mbinu tofauti zinazotumiwa na wahalifu hao ikiwa ni njia muhimu ya kushinda vita hivyo kwa pamoja.
Mhe. Othman ameyasema hayo leo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar aliposalimiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Mungano wa Tanzania inayoshughulikia Ukimwi, Kifua Kikuu, Madawa ya kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza inayotembelea Zanzibar kwa ziara ya kimafunzo hapa Zanzibar.
Mhe. Makamu amesema wahalifu wa madawa za kulevya wamekuwa wakitumia mbinu na ujanja mkubwa, hivyo ni vyema taasisi hizo kutambua hilo na kufanya kazi kwa pamoja na karibu zaidi kati ya pande mbili hizo ili kushinda vita dhidi ya tatizo hilo nchini.
Aidha Mhe. Othman amefahamisha kwamba katika kupambana na tatizo hilo, kuna haja ya kuukata mzizi wa tatizo hilo kwa kuwepo sheria zinazotenganisha kati ya usafirishaji na utumiaji wa madawa ya kulevya kama mbinu mbadala naya pamoja kupambamba na kushinda vita hivyo.
Amesema kuwepo kwa sheria za namna hiyo ni mbinu bora za kudhibiti uhalifu huo ikiwa ni pamoja na kuwa na nyenzo za kukata na kuzuia uwezo, mali na fedha za wahalifu hao wanazopata kwa mapato ya biashara hiyo haramu .
Amefahamisha kwamba wakati umefika sasa nchini Tanzania kuwa sheria na mbinu mbadala za pamoja zitakazosaidia vyema kudhibiti mali na uwezo wa wahalifu hao ili uhalifu hao usiweze kuendelea hasa katika kusafirisha, kuingiza na kuwepo matumzi ya madawa hayo nchini.
Amesema mashirikiano makubwa dhidi ya tatizo hilo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ni muhimu na yanahitajika sana na ni vyema kuachana na utaratibu wa kila upande kushikilia shieria yake pekee kwa kuwa jambo hilo linahitaji kufanyanyiwa kazi kwa pamoja miongoni mwa mamlaka zenye jukumu sambamba na kujengwa na kubadilishana uwezo na utaalamu juu ya jambo hilo.
Akizungumzia suala la ugonjwa wa kisukari Mhe. Othman, amesema kuwa ni maradhi yanayoongezeka sana nchini na kunahaja ya kuongezwa elimu miongoni mwa jamii hasa katika suala la matumizi ya vyakula, kuacha mazoea ya kula sukari, mafuta, uwanga kwa wingi bila mpangilio wa lishe bora.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge inayoshughulikia Ukimwi, Kifuaa Kikuu, dawa za kulevya na magonjwa yasiyoambukiza Mhe. Fatma Hassan Taufik, amesema Kamati yake imejifunza na imevutiwa sana na juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kupambana na tatizo hilo Zanzibar.
Amesema kituo cha kurekebisha tabia kwa waathirika wa dawa za kulevya kilichopo Kidimni wilaya ya Kati Ungujanj kinafanya kazi kubwa kutokana na program zake zilizopo na kwamba itasaidia sana kuwajengea uwezo waathrika wa dawa za kulevya kwa kuwa na mipango bora itakayosaidia sana waathrika kuwa na shughuli za kufanya na kuondokana na tatizo hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar leo tarehe 16/11/2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...