*Wasema imekuwa mwiba wa maendeleo ya kidigitali Tanzania, waeleza  sekta ya habari ilivyoathirika
Na Mwandishi Wetu
WADAU
 wa sekta ya habari na hasa waliojikita katika kutoa  huduma za maudhui 
katika Tovuti, programu tumishi, mtandao wa YouTube na blogs 
wamelalamika kupungua kwa kasi kwa watumiaji wa huduma zao huku 
wakiiomba wizara na wadau husika kujadili na kulipatia mwarobaini suala 
hili.
Kupungua kwa watumiaji hao kunatokana na kupanda maradufu 
kwa bei za vifurushi vya interneti nchini, huku GB 1 ya Data ikipatikana
 kwa zaidi ya dola 1.3 ambapo kumesababisha kupungua kwa kasi idadi ya 
watumiaji wa internet nchini, hivyo kuathiri taasisi, mashirika na 
watumiaji binafsi wa interneti ambao hutumia huduma hiyo katika majukumu
 mbalimbali pamoja na burudani.
Taarifa iliyoandaliwa na 
baadhi ya watoa maudhui, waandishi wa habari za mtandaoni na watumiaji 
wa mitandao Tanzania wamesema  kutokana na bei hizo kutokuwa rafiki kwa 
watumiaji wa huduma hiyo hasa mwananchi wa kawaida Taasisi na tasnia 
mbalimbali zimetajwa kuathirika kwa namna moja au nyingine.
Wamesema 
 kuwa ili  kuendesha mitandao ya kijamii inatakiwa kutumia bando kila 
wakati ili kuendelea kuuhabarisha umma kuhusu habari na matukio 
mbalimbali hivyo gharama kubwa za vifurushi zimekuwa kikwazo kwa 
bloggers & youtubers.
Kwa upande wa Wasanii na watoaji 
maudhui  ya burudani hasa kwa mtandao wa video wa YouTube nao wamedai 
idadi ya wanaofuatilia kazi zao kushuka kwa kasi kwa siku za karibuni, 
jambo ambalo wamedai kuathiri sana kipato chao. Vilevile mitandao 
mbalimbali ya takwimu inaonesha kushuka kwa watumiaji wa mtandao wa 
YouTube Tanzania kwa siku za karibuni.
Wakati kwa watumiaji 
binafsi wa internet nchini Tanzania nao wameonesha kukerwa na kupanda 
mara kwa mara kwa bei za vifurushi tena vinapandishwa kimya kimya licha 
ya mamlaka kusema gharama zimeshuka huku wakidai uishaji wa haraka 
kuliko kawaida wa vifurushi hivyo, vile vile  wanakumbusha ahadi za 
wadau na wizara kuahidi mara kadhaa kulishughulikia tatizo hilo na 
kubakia ahadi hewa. 
Pamoja na hayo, bei hizi ambazo zimetajwa 
kutokuwa rafiki kwa watumiaji  huenda zikazidi kuathiri  mfumo mzima wa 
maendeleo ya kidigitali hasa kwa mashirika, taasisi, na makampuni kama 
vile huduma za kibenki za kidigitali, huduma za afya, elimu, na dini 
zinazopatikana kwa njia za kidigitali pamoja na tasnia ya michezo ya 
bahati nasibu ya mtandaoni. 
Pamoja na hayo wamedai hali hiyo 
imeathiri haki ya  kupata taarifa huku wakifafanua kila mtu ana haki ya 
kupata taarifa, kwa miaka ya karibuni kutokana na ukuaji wa maendeleo ya
 teknolojia ya habari na mawasiliano hata Serikali imekuwa ikitoa 
taarifa zake kwa idara mbalimbali kwenda kwa wananchi kwa njia ya 
mitandao.
Hiyo inahusisha hata Matangazo ya moja kwa moja ya 
Uapisho wa viongozi, uzinduzi wa miradi na hotuba za viongozi kwa 
wananchi ambao wapo maeneo tofauti tofauti. Kwa mujibu wa wadau hao 
wamesema hapo awali ilikuwa rahisi mtu kufatilia mubashara matangazo ya 
matukio ya kitaifa kupitia mtandaoni.
Lakini  hivi sasa wananchi 
wengi wanapata shida kuangalia hadi mwisho matangazo hayo kwani 
maranyingi kabla tukio halijaisha kifurushi cha data kinakuwa 
kimeshaisha, hivyo athari hizi si tu kwetu wananchi ila hata kwa watoa 
taarifa wakiwemo viongozi wa Serikali.
Na hivyo ujumbe uliokusudiwa kuwasilishwa kwetu wananchi unakuwa umekwamishwa na gharama za vifurushi vya data.
Kutokana
 na hali hiyo wadau mbalimbali wanaishauri  wizara husika, pamoja na 
kampuni za simu nchini yanayotoa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo 
kuangalia upya na kwa umakini jambo hili kwa maendeleo na tija ya nchi.
Wamesema
 wanafahamu Vifurushi vya Data ni Ofa za kampuni ya simu katika kufanya 
ushindani wa kibiashara, lakini licha ya ofa basi wanashauri ziwe zenye 
kuleta unafuu kwa mwananchi kwani kukiwa na huduma hizo nzuri, hata 
matumizi ya mawasiliano kwa njia ya simu yataongezeka na kutaongeza 
mapato kwa Serikali kwa njia ya kodi na tozo zilizopo hivi sasa.
Home
HABARI
 WADAU WATOA OMBI KWA WIZARA,KAMPUNI ZA SIMU KUANGALIA NAMNA YA KUPUNGUZA BEI KUBWA KATIKA VIFURUSHI VYA DATA 
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...