MBUNGE Wa Kinondoni Abbas Tarimba amesema kuwa atatembelea shule za Kata ya Makumbusho na kuangalia namna bora ya kuwezesha kuweka mazingira bora ikiwemo ujenzi wa uzio pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa taulo za kike mashuleni ili kuwaweka salama zaidi watoto wa kike kwa kuhakikisha wanakuwa salama na wanahudhuria masomo yao wakati wote.
Tarimba ameeleza hayo wakati akijibu hoja ya Mkurugenzi wa shirika wa Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI,) Janeth Mawinza katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM,) Kata ya Makumbusho ambaye alieleza kuwa kumekuwa na changamoto ya uzio kwa shule za Sekondari katika Kata hiyo hali inayopelekea wanafunzi kutorokona na kujiingiza katika makundi yasiyofaa huku wanafunzi wa kike wakishindwa kuhudhuria vipindi kutokana na kukosa taulo za kike zitakazowasitiri wakiwa shuleni.
Akijibu hoja hiyo Tarimba amesema kuwa wanasimamia Maendeleo ya haraka katika jimbo hilo hasa katika uimarishaji wa sekta ya elimu na miundombinu ya barabara na maji na kuahidi kutembelea shule hizo ili aone afanya nini akiwa Mbunge pamoja na kuangalia namna ya kuwezesha upatikanaji wa taulo za kike kwa wanafunzi na kuwataka Madiwani kushirikiana na asasi za namna hiyo katika kutatua kero za wananchi.
Awali akitoa mada katika jukwaa hilo la Jumuiya ya Wazazi ya CCM Bi. Mawinza alieleza kuwa Shirika hilo linalofadhiliwa na Women Fund Tanzania (WFT) limejikita katika utetezi wa haki za wanawake na watoto na kutokana na umuhimu wa Jumuiya hiyo wameona ni vyema kushirikiana masuala mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia hasa ukatili wa kingono kwa watoto ili waweze kushirikiana kwa kuutokomeza kuanzia ngazi ya familia.
Amesema kuwa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliozinduliwa na Waziri Mkuu hali bado sio nzuri hasa kwa watoto ambapo tafiti zimeonesha kuwa kwa mwaka 2020/2021 watoto 6168 wamefanyiwa ukatili, kati yao watoto wa kike ni 5287, wavulana 881.
"Narudi kwenu tushirikiane katika hili, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jeshi la polisi kesi za ukatili zilizofanyiwa upelelezi ni 2368 kesi zilizofanyiwa maamuzi ni 88 hali bado mbaya.....Tukiwa Jumuiya ya wazazi tuone tuna safari ndefu kwa kuchukua hatua ya mabadiliko ya tabia....WAJIKI tumeanza kupitia kampeni ya Safari salama bila rushwa ya ngono iliyolenga kuvunja ukimya katika masula ya rushwa ya ngono na tunashirikiana kwa karibu na madereva bodaboda na daladala ambao wanatajwa sana katika vitendo hivi kwa kuwapa elimu itakayowasaidia wao na madereva wengine." Amesema.
Amesema kuwa Jumuiya hiyo ina nafasi kubwa ya kushiriki katika ustawi wa jamii ili kujenga jamii imara ya sasa na baadaye.
Amesema masuala hayo kwa sasa yanazungumzwa katika jamii ili kuongeza uelewa zaidi na kuvitaka vyombo vya habari kuangalia namna ya kuripoti matukio hayo zaidi.
"Tunabahati ya kuwa na WAJIKI wapo hapa muda mrefu tunawatambua na tunashirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kijinsia katika kata ya Makumbusho."
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi tawi la Mwinjuma Huba Simba akizungumza katika kikao hicho na kueleza kuwa wanashirikiana na WAJIKI katika kuhakikisha watoto wanasoma na wanahimiza wazazi kuwapeleka watoto mashuleni kupitia vikao vya mashina.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...