Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), iliandaa Kongamano la Fursa za Uwekezaji na Biashara lililofanyika katika ofisi za Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali katika sekta za kilimo, ufugaji, teknolojia, upatikanaji wa mitaji na masoko.
Akizungumza wakati wa kufungua Kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa (ESRF) Dkt. Tausi Kida alisema, wataalam mbalimbali watawasilisha mada katika fursa ambazo zimefanyiwa tafiti za kina na Taasisi hiyo ambapo mada hizo zimegawanyika katika maeneo makuu manne ambayo ni: (1)Fursa zilizopo katika sekta mbalimbali katika mikoa hapa nchini, (2)Fursa katika Teknolojia, (3)Fursa ya upatikanaji wa masoko pamoja na (4) Namna ya kupata mitaji.
Dkt. Tausi alifafanua kwamba, fursa zitakazozungumziwa katika kongamano hili zitajikita katika sekta mbali mbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, madini, viwanda, usafirishaji, ujenzi, afya na elimu. Aidha, alisema kuwa kutakuwa na mawasilisho yatakayojikita kwenye fursa mbalimbali katika kilimo biashara (Agribusiness) kama vile Kilimo cha mbogamboga bila kutumia udongo (Hydroponic vegetable), Kilimo cha malisho ya mifugo bila kutumia udongo(Hydroponic fodder), kilimo katika shamba kitalu (Green House), ufugaji wa samaki katika vizimba (cage) katika mabwawa (ponds), katika matanki (RAS), ufugaji wa kisasa wa nyuki ikiambatana na shuhuda kutoka kwa wadau mbalimbali wanaofanya Kilimo Biashara kwa tija.
Kwa upande wa upatikanaji wa mitaji, Dkt. Kida alisema kuwa, wafanyabiashara wengi pamoja na wakulima wanapata changamoto kwenye upatikanaji wa mitaji ambapo wengi hawajui namna ya kuweza kupata mitaji au uelewa wa namna ya kupata mitaji, hivyo basi tutakuwa na wataalamu kutoka mabenki na huduma nyingine za utoaji wa mitaji ya kuleta maendeleo kwa watu na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kukua kwa sekta ya teknolojia duniani, sekta zote za maendeleo zinahitaji matumizi ya teknolojia ili kufanya shughuli zake kwa uharaka, uhakika na ufanisi mkubwa ambao utaleta tija. Kwa kuliona hilo tumewaalika wataalamu ambao leo hii watatoa mada juu ya matumizi ya teknolojia na jinsi teknolojia inavyotumika katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Lakini pia tutakuwa na shuhuda mbalimbali za matumizi ya teknolojia kutoka kwa wadau wanaofanya vyema katika shughuli zao, alisema Dkt. Kida.
Aidha, Dkt. Kida alisisitiza kuwa, Fursa zilizopo hapa nchini ni nyingi sana kwani kila mkoa wa Tanzania una fusra zake na hasa kwenye kilimo, ufugaji, madini na sekta nyingine, hivyo amewaasa vijana kuchangamkia fursa hizo ili kujikwamua kiuchumi.
Akitoa neno kwa niaba ya Wizara ya Kilimo, Kaimu Mkurugenzi wa Kilimo upande wa Sera na Mipango ndugu Gungu Mibavu, alisema serikali iko bega kwa bega na wadau wote wa Kilimo kwa kuimarisha shughuli za ugani pamoja na kupunguza ama kuondoa kodi na tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kero kwa wadau wa Kilimo.
Akizungumzia
fursa mbalimbali katika upatikanaji wa masoko ya kuuza bidhaa, mwakilishi wa TANTRADE
Bw. John Fwalo alisema, Taasisi yao imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa
wazalishaji wa bidhaa hapa nchini katika kuwatafutia masoko ya uhakika ndani na
nje ya nchi. Bw. Fwalo alitoa wito kuwa, TANTRADE wapo kuwasaidia wote ambao
watahitaji msaada wao katika upatikanaji wa masoko.
Aidha, mwakilishi wa taasisi ya PASS Bw. Hamisi Mmomi alisema, PASS hutoa
mikopo kwa wateja ambao wanazo dhamana na endepo mteja ana dhamana ya kiasi
kidogo wao wako tayari kumdhamini ili aweze kukopesheka.
Wadau walioshiriki kwenye kongamano hilo ni Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Aquaculture Association of Tanzania, Big Fish, Agriculture Media Ltd, Green Fish Investment, Nyanzobe Ltd, IMADS, Tanganyika Apicultural Ltd, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO), Multics Company, Kampuni ya Ramani, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), CRDB, TADB, SELF, PASS Trust na pamoja na wadau wengine mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...