Mlezi wa kituo cha kulea watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu cha St Antony Mfaranyaki kilichopo kata ya Mfaranyaki katika Manispaa ya Songea Judith Mwageni kushoto, akipokea zawadi ya Mbuzi kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Songea Livini Lyakinana, wakati baadhi ya watumishi wa Mahakama walipotembelea kituo hicho jana kwa ajili ya kuwaona na kuwapa zawadi watoto wanaoishi katika kituo hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea Livini Lyakinana kulia akimpa zawadi ya mafuta ya kupikia mlezi wa kituo cha kulea watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu cha St Antony Mfaranyaki kilichopo katika Manispaa ya Songea Juditth Mwageni kwa ajili ya watoto wanaoishi katika kituo hicho ambapo watumishi wa Mahakama kanda ya Songea walitembelea kituo hicho kwa ajili ya kwenda kuwaona na kutoa msaada wa vitu mbalimbali,kushoto ni Afisa Tehama wa Mahakama Kuuu kanda ya Songea Catherine Francis.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu mkazi Songea Livini Lyakinana kulia, akimpa mfuko wa unga wa sembe uliotolewa na Mahakama Kuu kanda ya Songea mlezi wa kituo cha kulea watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu cha St Antony Mfaranyaki Sister Judith Mwageni kwa ajili ya watoto wanaoishi katika kituo hicho.

Na Muhidin Amri, Songea
KATIKA kuhadhimisha wiki ya sheria nchini,Mahakama Kuu kanda ya Songea imetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa kituo cha kulea watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu cha St Antony Mfaranyaki kilichopo kata ya Mfaranyaki Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Misaada iliyotolewa kwa watoto hao ni Mbuzi,mafuta ya kula,mchele,unga wa mahindi,ngano na sabuni kwa ajili ya kuwapa faraja watoto hao wakati huu ambao Mahakama inaendelea na maadhimisho ya wiki ya sheria kuelekea kilele cha siku ya sheria nchini.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea Sekela Moshi Hakimu Mkazi Lilian Haule alisema, mahakama kama taasisi ya umma imekuwa ikisaidia jamii hususani watu wenye uhitaji maalum kwa lengo la kuwapa matumaini.

Alisema,wamekwenda katika kituo hicho kwa ajili ya kuwaona watoto wanaolelewa katika kituo hicho kwa kuwa ni sehemu ya watu ambao wanawahudumia mara kwa mara na wanaguswa moja kwa moja na kazi zinazofanywa na mahakama nchini.

Alisema,wapo watoto wa mitaani wanaishi kwa wazazi wao na wanaweza kwenda katika mabanda au mahakamani kwa ajili ya kupata elimu ya sheri na haki mbalimbali,lakini watoto wanaoishi kwenye vituo mbalimbali ni vigumu kujua wako wapi na wanafanya nini.

Kwa hiyo,wamekwenda kuwatembelea kwa lengo la kuwaona na kuwatia moyo kwani wao kama watoto bado wana haki ya kupata mahitaji yote ya msingi kama ilivyo kwa watoto wengine katika jamii.

“mahali ulipo hapakufanyi uwe mtu fulani,bali unakuwa mtu fulani kwa vile unataka kuwa hivyo, pamoja na watoto hawa kuwa katika maeneo hayo lakini miongoni mwao wanaweza kupatikana majaji, wanasheria,mahakimu na watumishi wa taasisi na idara mbalimbali za umma”alisema Hakimu Haule.

Aidha amewasihi watoto hao kutokata tamaa, kwa sababu kuishi mahali hapo sio mwisho wao na haki mojawapo ya mtoto ni kuishi na wazazi au walezi kama ilivyo kwa watoto wa kituo hicho ambao wanapata haki zote ikiwamo chakula,mavazi na kwenda shule.

Amewataka kusoma kwa bidii na kutoogopa kujieleza au kuuliza maswali kwa walimu wao ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao na wakati wote wamshirikishe Mungu katika safari yao ya masomo, kwani hiyo ndiyo fursa pekee katika maisha yao.

Kwa upande wake Mama mlezi wa kituo hicho Judith Mwageni alisema, kituo hicho kimeanza mwaka 2010 na kina watoto 59 kati yao 34 wanaishi kituoni hapo na wengine wanaishi kwenye shule za bweni zilizopo ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma.

Alisema,changamoto zinazowakabili kwa sasa ni ugumu wa uendeshaji wa kituo hicho kwa kuwa sehemu kubwa wanategemea wafadhili wa nje ambao kutokana na janga la ugonjwa wa Corona hawafiki nchini na wengine wamefariki.

Alisema, mahitaji makubwa kwa watoto wa kituo hicho ni chakula,mafuta ya kula na kupaka,sabuni,sale na vifaa vya shule na mahitaji mengine muhimu ya watoto na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia.

Mmoja wa watoto wa kituo hicho Rahabu Mkondya,ameishukuru Mahakama kuu kanda ya Songea kwa msaada huo ambao unakwenda kupunguza baadhi changamoto zilizopo katika kituo hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...