*Tiketi za kieletroniki kuanza kutumika
Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
WAKALA wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) umesema kuwa kazi kubwa ya wakala sio kufikiria kusafirisha watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine bali ni kuangalia namna ya kumuweze mtu kusafiri kwa kwenda kuzalisha kwa kukuza uchumi wa nchi.
Hayo ameyasema Mtendaji Mkuu wa DART Dk.Edwin Mhede wakati akifungua Kikao cha Wahariri na Waandishi habari kuhusiana na mikakati ya DART katika utoaji wa huduma ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Mhede amesema utoaji wa huduma za usafiri ulianza mwaka 1947 hivyo katika mabadiliko na hadi kufika kwa DART ni mwendelezo wa kufanya huduma hiyo kwenda kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Mhede amesema kuwa kuna miradi ya awamu sita ambapo jiji la Dar es Salaam wananchi watapata huduma kupitia wakala huo pamoja na kujengwa kwa majengo ya kisasa katika vituo kwa kutoa huduma mbalimbali.
Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Dart, Ng’wanashigi Gagaga amesema wameanzisha mfumo mpya wa ukataji wa tiketi wa kielektroniki ili kuhakikisha inazuia upotevu wa mapato.
Gagaga amesema, mfumo uliokuwapo haukuwa vizuri na Serikali kuamua kuuondoa na kuanzisha mfumo wake mwenyewe “ambao hautakuwa na gharama kubwa kwani ukiwa na gharama kubwa anayekuja kuumia ni mwananchi.
“Mfumo wa kutaka tiketi umeanza kufanya kazi kwa tiketi hizi za utambuzi wa QR Code na unafanya kazi ambapo kati ya vituo 33 vituo 20 tayari vimeanza kutumia huu mfumo. Lakini unaweza kutumia kupitia simu za mkononi na au kununua kadi maalum,” amesema Gagaga.
Amesema mfumo uliokuwapo, lakini waliokuwa wakitoa huduma eneo la tiketi za kielektroniki ilikuwa Kampuni ya Maxmalipo iliyoacha zaidi ya miaka ya miaka miwili iliyopita.
"Tumekusudia kufunga mfumo maalum wenye uwezo wa kuangalia mabasi yapishane kwa muda gani “na katikati ya mwaka huu, tunaweza kuwa tumekamilisha kwani hatuutengenezi sisi bali tunaununua na tuko hatua za mwisho za manunuzi.”amesema Gagaga.
Naye Kaimu Mkurgenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Dart, Mhandisi Ahmed Wamala amesema, mradi umegawanyika katika awamu sita ambapo awamu ya kwanza yenye kilomita 20.9 imekwisha kujengwa na kutumika kutoka Kivukoni kwenda Kimara na kutoka Magomeni kwenda Morocco na Fire kwenda Kariakoo.
Wamala amesema, awamu ya pili kutoka katikati ya Jiji kwenda Mbagala Rangi tatu na kutoka JKT Mugulani kuja kukutana na Magomeni ujenzi wake unaendelea ambao uliwekwa katika mafungu mawili.
Ametaja mafungu hayo ni ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ambapo mkandarasi amefikia asilimia 45 na pili ni miundombinu ya majengo ikiwemo depo umekamilika kwa asilimia 100.
Wamala ametaja awamu ya tatu itahususisha barabara za kutoka mjini kwenda Gongolamboto kupitia Uwanja wa Ndege, “usanifu umekwisha kamilika, tumefanya mchakato wa kumpata mjenzi na tumepata kibali kutoka Benki ya Dunia kumwajili mkandarasi na wakati wowote tutaanza ujenzi.
Awamu ya nne ameitaja ni barabara ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia Maktaba kwenda Tegeta hadi Dawasa eneo la Boko na kwenda Ubungo katika daraja la Kijazi. Usanifu umekwisha kufanyika na mtaalamu elekezi amekwisha kuleta nayaraka na kuzipitia na kabla yam waka huu kuisha ujenzi utakuwa umekwenda.
Wamala ametaja awamu ya tano zinahusisha barabara za Mandela pale Ubungo kwenye daraja la Kijazi kwenda Kigamboni katika daraja la Nyerere “halafu tuna barabara mpya tunaitengeneza kutoka Tabata Segerea inakwenda mpaka ‘round about’ ya Kigogo, tayari usanifu umefanyika na serikali inaendelea kufanya majadiliano na wafadhili na kama majadiliano yatakwenda vizuri, Aprili 2022 tunaweza kuwa tumefanya mkataba.”
Awamu ya sita inahusisha barabara ya Mwai Kibaki kutoka Moroco inakwenda kuungana na barabara ya Ali Hassan pale Lugalo.
“Kuutakuwa na upanuzi wa barabara kutoka Kimara kwenda Kibaha kwa kuweka njia na vituo maalum na tutakuwa na upanuzi wa Mbagala Rangi tatu kwenda vikindu na tukikamilisha yote haya tutakuwa na kilomita 154.4,” amesema Wamala.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji wa Dar), Mhandisi Fanuel Kalugendo amesema, ili kubaini mabasi mabovu wanashirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kuwa inayafanyia ukaguzi na kutoa ushauri ili kuhakikisha wanakuwa na mabasi bora kwa matumizi.
Amesema, kwa kawaida asilimia 90 ya mabasi yawe barabarani na asilimia 10 yanakuwa matengenezo na kwa kipindi hiki wana magari 210 na yanayopaswa kuwa barabarani zaidi ya 190, “lakini ifahamike hatutoi mabasi yote kwenda barabarani kwani mengine lazima yaende matengenezo.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...