NA MWANDISHI WETU, KIBITI

MKUU wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge amewaagiza viongozi wa Serikali ngazi zote mkoani humo kuhakikisha wanafuatilia watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule na wale waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wa 2022 wanaripoti katika shule walizopangiwa  kwakuwa Serikali tayari imejenga miundombinu ya kutosha kwa ajili ya masomo.

Mhe. Kunenge aliyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Vyumba vya Madarasa ya Samia katika wilaya za Mkuranga na Kibiti  chini ya mradi wa Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii wa 5141TCRP ambapo hadi sasa umefikia asilimia 99.9%.

Mradi huo unatekelezwa baada ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupokea mkopo wa Shilingi Trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kukabiliana na athari zilizotokana na ugonjwa wa Uviko 19.

”Suala la shule halina hiari, mzazi atakayeshindwa kumpeleka mtoto shule achukuliwa hatua za kisheria, viongozi wa eneo lile watakaoshindwa kuhamasisha uandikishaji wa watoto kujiunga darasa la kwanza na wale wanaopashwa kujiunga kidato cha kwanza nao wachukuliwe hatua kwa sababu watakuwa hawatoshi.” Alisema RC Kunenge

RC Kunenge alisisitiza “Tutakapobaini kuna eneo mtoto haende shule viongozi wa Serikali wa eneo lile hawatoshi kwasababu wameshindwa kutekeleza majukumu yao …..….Haiwezekani Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, afanye jitihada kubwa kama hizi halafu sisi wasaidizi wake tusitekeleze maana yake tutakuwa tunamuhujumu na anayemuhujumu hatakiwi kuwa miongoni mwetu.” Alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

Aidha wananchi wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada ya kutafuta fedha na kuzielekeza katika miradi ya Kijamii ikiwemo Elimu na Afya.

“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa madarasa haya na ofisi ya walimu kama unavyoyaona, kwakweli tunayo furaha kubwa.” A;isema Bw. Hamza Bakar kutoka kitongoji cha Matatu.

RC Kunenge alisema Mkoa wa Pwani ulipata mgao wa Shilingi Bilioni 13.39 na kati ya hizo Bilioni 10.9 zimetumika kujenga vyumba vya madarasa ya shule za sekondari na shule shikizi 535.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...