Na. Damian Kunambi, Njombe
Kutokana na mvua kuchelewa kunyesha katika maeneo mengi hapa nchini wakulima wilayani Ludewa mkoani Njombe, wameingiwa na hofu ya upungufu wa chakula kwa mwaka huu kwani wanalazimika kutumia mbegu za kisasa badala ya mbegu za kienyeji ili ziweze kustawi kwa muda mfupi.
Wakizungumza na Michuzi TV wakulima hao wamesema kuwa wakulima wengi wa hali ya chini wamezoea kupanda mahindi waliyovuna mwaka uliopita ambayo ustawi wake huchukua muda mrefu na huitaji maji mengi lakini kwa sasa kutokana na mvua kuwa chache wanalazimika kutumia mbegu za kisasa ambazo huuzwa kilo mbili elfu 12,000 hadi 13,500 kitu ambacho hawawezi kumudu gharama hizo.
Titus Haule ni miongoni mwa wakulima hao amedai kuwa wakulima hutumia mbegu za kienyeji kwakuwa hawana uwezo wa kununua mbegu za kisasa lakini kwa mwaka huu watu hao wa hali ya chini wapo katika wakati mgumu zaidi juu ya zao hilo kwani inawalazimu kubahatisha kwa kupanda mbegu hizo hizo za zamani kitu ambacho ni ngumu kuleta matokeo mazuri.
"Mwaka huu ni mgumu sana kwetu sisi wakulima wa hali ya chini maana tunaingia hofu ya kukumbwa na janga la njaa hivyo tunaiomba serikali itupunguzie bei ya mbegu ya kisasa ili hata sisi wananchi wa hali ya chini tuweze kumudu gharama hizo", amesema Haule.
Naye Maria Kayombo amesema wamezoea katika miaka mingine mwezi huu wa kwanza huwa ni mwezi wa kupalilia lakini mwaka huu umekuwa tofauti badala ya kupalilia wao wanapanda.
Amesema mabadiliko haya yana matokeo mabaya zaidi kwani kilimo kimekuwa na gharama kubwa zaidi kuanzia kwenye mbolea ambayo hununua shilingi 120,000 kwa mfuko mmoja wa kilo hamsini halafu baada ya mavuno wanauza mahindi elfu 4000 kwa debe moja.
"Tunaomba serikali itusaidie kutupunguzia gharama ya pembejeo maana zipo juu kuliko gharama ya mazao tunayo yauza, mpaka sasa mahindi bado tunayo ndani kwakuwa soko halieleweki na hatujui ni lini soko litakuwa zuri, kwakweli sisi wakulima wa hali ya chini tunateseka sana!", Amesema Bi. Kayombo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...