WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema serikali itahakikisha inapunguza matukio ya ukatili kwa watoto wa kike ambayo kwa sasa takwimu zinaonesha hufanyika kwa asilimia 70.

Amesema  kwa kushirikiana na wadau wake wote itaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua zenye kuhamasisha kuzuia na kushughulikia aina zote za ukatili ili kuhakikisha jamii ya kitanzania inafurahia haki ya kuishi.

Waziri Gwajima ametoa kauli hiyo leo wakati alipofanya ziara katika makao ya watoto na makazi ya wazee katika kituo cha  'Home Of Love and Joy' kilichopo Hombolo Jijini Dodoma ili kujionea namna wanavyoishi na kutambua mahitaji yao

Waziri Gwajima alikuwa ameongozana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mwanaidi Ally Khamis, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk.Zainabu Chaula na Amon Mpanju na wataalamu wa Wizara hiyo.

Waziri Gwajima amesema kuwa, watoto wanapokuwa wanaishi kwenye mazingira hatarishi pamoja na changamoto nyingi pia wanakutana na ukatili mkubwa katika mazingira tofauti tofauti.

Aidha, ukatili wa majumbani ni sababu mojawapo inayowafanya watoto wakimbilie mitaani na matokeo yake wanakutana na aina zingine za ukatili na mazingira hatari zaidi

"Takwimu zinaonesha waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa upande wa watoto  wa kike ni asilimia  70 pamoja na serikali na wadau wake kuendelea kupambana kuzuia ukatili pia inatoa huduma kwa wahanga wa ukatili ikiwemo huduma ya kisheria ambapo kwa mwaka 2020/21 mashauri 3889 yamepelekwa Mahakamani na 1,504 yametolewa hukumu na mengine kazi inaendelea,”amesema

Waziri amebainisha kuwa ukiacha ukatili kwa watoto hata watu wazima wanafanyiwa ukatili ambapo wanawake wanatengeneza asilimia  96 ya wanaoathirika.

“Kwa ujumla wake ukatili kwa mtu yeyote haukubaliki, hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wake wote itaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua zenye kuhamasisha kuzuia na kushughulikia aina zote za ukatili ili kuhakikisha jamii ya kitanzania inafurahia haki ya kuishi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Dk.Zainabu Chaula amesema huo ni mwendelezo ziara ya kutembelea vituo vya kulelea watoto na wazee ambapo walianza Januari 17 mwaka huu Kikombo na Kijiji cha Matumaini.

Naye,Naibu Waziri Mwanaidi ally Hamis amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameona umuhimu wa kuanzisha Wizara hiyo kwa kuwa ni eneo pana hivyo wameunda timu ya kutembelea vituo mbalimbali ambavyo vinalea wazee na watoto lengo ni kujua kwa undani changamoto ambazo wanakutana nazo ili waweze kuzitatua.

“Upendo unahitajika sana ndio maana Mwalimu Nyerere na Karume waliona umuhimu wa kuanzisha vituo hivi.Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa sasa hawana kazi sasa kazi imeanza Rais anataka kuona tunafanya kazi kutembea na kuona uhalisia,”amesema.

Kwa upande wake,Sister wa makao ya watoto na makazi ya wazee  cha  Home Of Love and Joy,Sister Radience MC amesema lengo la kuanzishwa kituo hicho ni bila kubagua dini wala ukabila ambapo walengwa hupatiwa huduma zote bure.

Amesema wanakabiliwa na changamoto za gharama kubwa za uendeshaji wa kituo malipo kwa ajili ya umeme na wale ambao wanaumwa hivyo wameomba wapatiwe Solar pamoja na bima ya afya.


"Kituo chetu kilianza muda mrefu kidogo ambapo hadi sasa tunawatoto 23  na wazee 54 ambao wanalelewa na kituo chetu na kupatiwa mahitaji muhimu ikiwemo maradho, chakula na vingine"alisema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akizungumza na watoto waliopo katika kituo cha Makao ya Watoto na Makazi ya Wazee kilichopo Hombolo jijini Dodoma.
Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ally Khamis akizungumza na Wazee na Watoto waliopo katika kituo cha Wazee na Watoto Hombolo jijini Dodoma leo katika ziara ya Waziri, Dk Dorothy Gwajima.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju akitoa neno lake katika ziara ya Waziri Dk Dorothy Gwajima katika kituo cha Malezi ya Watoto na Makazi ya Wazee kilichopo Hombolo jijini Dodoma.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...