Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha .


Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amefunga kikao kazi cha Majaji Wafawidhi mwishoni mwa wiki iliyopita tarehe 11 Februari, 2022 huku akitoa rai kwa Majaji hao kutekeleza na kueneza mazuri yote waliyoyapata katika kikao hicho ili kuboresha zaidi huduma ya upatikanaji haki kwa wananchi.

Akizungumza na Waheshimiwa Majaji Wafawidhi katika Ukumbi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliopo jijini Arusha, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa ili kwenda pamoja ni vyema kuwashirikisha Watumishi wa Mahakama wa ngazi mbalimbali pamoja na Wadau ili kuimba wimbo mmoja wa kuboresha huduma za Mahakama.

“Sisi ni kama Mabalozi na pia ni wawakilishi wa wale ambao tunaowaongoza, hayo mazuri ambayo tumeyapata hapa tuhakikishe tunayafikisha kwa njia mbalimbali na mimi naamini baada ya ninyi kupitia tanuri ya mkutano huu mtakuwa ni viongozi bora kuliko mlivyokuwa kabla ya kuanza kwa mkutano kwa sababu mmepata mada mbalimbali zenye manufaa makubwa katika utendaji kazi,” alisema Jaji Mkuu.

Aliongeza kwa kuwataka Majaji hao kuwa na desturi ya kujisomea zaidi kwakuwa dunia ya sasa ina mambo mengi ya kimaboresho hivyo kujisomea kutawezesha kupata taarifa nyingi zaidi ambazo zitakuwa za manufaa katika uboreshaji wa huduma za kimahakama.

Naye, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewasisitiza Majaji hao kuzingatia masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya mfumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa kuratibu mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS II).

“Wahe. Majaji tunakwenda kwenye Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’, safari imeanza na sio jukumu la Mhe. Jaji Mkuu pekee, Majaji Wafawidhi ndio wasimamizi wa kuwezesha hili, hivyo tusilege kutumia mifumo iliyopo ili kufikia azma yetu,” amesema Mhe. Siyani.

Amesisitiza pia kuhusu matumizi ya teknolojia katika kusikiliza mashauri hususani matumizi ya ‘Video Conference’ ambapo amesema kila mmoja ahakikishe kuwa teknolojia inatumika kwa kiasi kikubwa kwakuwa ni suala linalowezekana hivyo linahitaji uamuzi na utayari wa wote.

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Siyani amewakumbusha Wahe. Majaji Wafawidhi kusimamia vyema utendaji kazi wa Mahakama za chini ambazo ni Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu Mkazi kwenye kuongeza kasi ya uondoshaji wa mashauri.

“Tusimamie vyema Mahakama za Mwanzo na zote zilizopo chini yenu ili kasi ya uondoshaji wa mashauri iendelee, Mahakama hizo ndio zinazojenga taswira ya Mahakama kulingana na ukweli kwamba zinapokea idadi kubwa ya mashauri,” alisisitiza Jaji Kiongozi.

Katika siku ya pili ya Kikao kazi hicho Mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo; mada ya Hali ya Mashauri na Mikakati yake iliyowasilishwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma ambapo katika mada yake aliainisha mafanikio kadhaa ikiwemo kukamilika kwa uandaaji wa Taarifa ya Utendaji Kazi za Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2021 ‘Comprehensive Performance Report of the Judicial Functions 2021’.

Mada zingine ni hali ya mlundikano na Mikakati ya Kanda/Divisheni kuondoa mlundikano iliyowasilishwa na Majaji Wafawidhi, Dhana ya Vituo Jumuishi, ukaguzi wa Mahakama na nyingine.

Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho kilichoanza tarehe 10 Februari, 2022 ni Mahakama kufanya mawasiliano na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) na vyuo vingine vinavyotoa mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu ili kuanzisha Mitaala ya mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu kielektroniki ili iendane na mabadiliko/uboreshaji wa matumizi ya TEHAMA yanayoendelea mahakamani na katika sekta nyingine.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Wahe. Majaji Wafawidhi (hawapo katika picha) wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha Majaji hao kilichoanza tarehe 10 Februari, 2022 katika Ukumbi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha.





Waheshimiwa Majaji Wafawidhi kutoka Kanda na Divisheni za Mahakama Kuu wakimsikiliza kwa makini Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma alipokuwa akitoa nasaha zake wakati wa kufunga kikao kazi cha siku mbili cha Majaji hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza na Wahe. Majaji katika hafla ya kufunga kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika tarehe 10 na 11 Februari, 2022 katika Ukumbi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwasilisha mada ya Hali ya Mashauri na Mikakati yake, katika mada hiyo Msajili Mkuu aliainisha mafanikio kadhaa ikiwemo kukamilika kwa uandaaji wa Taarifa ya Utendaji Kazi za Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2021 ‘Comprehensive Performance Report of the Judicial Functions 2021’.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mshauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akiwaonyesha Majaji Wafawidhi (hawao katika picha) moja ya nakala ya kitabu cha Taarifa ya Utendaji Kazi za Mahakama ya Tanzania kwa mwaka 2021 ‘Comprehensive Performance Report of the Judicial Functions 2021’.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akiwasilisha Mada ya Dhana ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki ‘IJCs’ ili kuwapa uelewa zaidi Majaji Wafawidhi kuhusu uendeshaji wa Vituo hivyo vilivyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 06 Oktoba, 2021. Kwa sasa Vituo hivyo vipo Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Arusha, Mwanza, Dodoma na Morogoro.


Mwezeshaji kutoka ‘ESAMI’, Bw. Andrew Msami akitoa mada katika kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibraahim Hamis Juma kwa kushiriki pamoja nao katika kipindi chote cha kikao chao. Mhe. Jaji Mruma alitoa neno la shukrani kwa niaba ya Majaji wenzake walioshiriki katika kikao hicho. (Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...