Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema ofisi yake itaendeleza uhusiano mzuri baina yake na mahakama zote jijini humo ili kudumisha utawala wa sheria na kuwatendea haki wananchi.

Malima amesema hayo leo Jumanne Februari 2, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria jijini Tanga na kuongeza kuwa hayo yote yanawezekana kila mtu akitambua nafasi yake na kuheshimu nafasi ya mwenzake.

Aidha, Malima ambaye alikuwa mgeni maalumu katika maadhimisho hayo amewapongeza watumishi wa mahakama wakiwamo majaji na mahakimu huju akiwataka kutenda haki hususani kwa wasiokuwa na kipato.

"Binafsi nawapongeza kwa hatua mliyoanza kuchukua ya maboresho ya mahakama kuwa ya kimtandao, hii itasaidia kuleta ufanisi na kuweka uwazi lakini pia kuokoa muda na haki ikapatikana ni jambo zuri.

"Lakini kuna jambo ambalo huwa linaniumiza sana ndani ya nafsi yangu hili la upatikanaji wa haki kwa wale wenye uwezo mdogo wa kipato, nawaomba mfumo huu utusaidie watendewe haki," amesema Malima.

Pamoja na mambo mengine, Malima amezungumzia utawala wa sheria akitolea mfano wa watu kujichukulia sheria mkononi katika mapigano ya wakulima na wafugaji wilayani Kilindi mkoani Tanga, yaliyosababisha mauaji ya watu saba.


"Utawala wa sheria ni watu kutojichukulia sheria mkononi na kutofanya mambo yasiyo na maslahi kwa wananchi. Kuna watu wanabaka watoto... tuwaache watoto wawe watoto na sheria iwalinde, Tanga ninayoongoza mimi hakuna nafasi hiyo," amesema.

Awali, Jaji Mkuu wa Mkuu Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Latifa Mansour alisema katika wiki ya sheria ambayo kilele chake kimefikia leo mambo mbalimbali yamefanyika ikiwamo kutoa elimu ya sheria kwa wadau na wananchi magerezani, mashuleni na kwenye viwanja vya wazi huku akisema wananchi wote ni wanasheria.

"Kuna wanasheria na wasomi wa sheria, mtu yeyote anayekubali kufuata na kutii sheria ni mwanasheria," amesema.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...