Wakati Tanzania inaadhimisha siku ya wanawake katika Sayansi leo, imeelezwa kuwa uwakilishi wao bado ni mdogo sana.
Wito huo umetolewa leo Februari 11, 2020 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Philbert Luhanga wakati wa kuadhimisha siku ya wanawake katika sayansi.
Kaimu Mkurugenzi huyo amesema wanawake huathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi ikilinganishwa na wanaume, kwa sababu katika hali ya uhaba wa maji, wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Dr Luhanga wabobezi wanawake katika fani ya Sayansi wanatakiwa kuwa wabunifu ili kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu wanawake ikiwemo matatizo ya maji yanatokana na mabadiliko ya tabia nchi.
"Sayansi ya ubunifu inapaswa kuwa msingi mkuu katika kutafuta suluhisho zinazowakabili umma wakiwemo wanawake," alisema.
Alisema sera ya mazingira iko mbioni kuanza kutumika ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi hasa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameleta athari kubwa.
Kwa upande wake, Ofisa Mtafiti Mwandamizi wa Costech, Dk Hulda Gideon alisema wakati Tanzania ikiungana na wanasayansi wengine kusherehekea wanawake katika masomo ya sayansi, idadi ya wanawake katika taaluma hiyo bado ni ndogo ili kuleta mabadiliko.
"Uwakilishi wa wanawake katika sayansi bado uko chini iwe kuanzia ngazi ya kufanya maamuzi, usimamizi hadi ngazi za chini," alisema.
Alibainisha kuwa Tanzania na dunia nzima haijanufaika na fursa ya ubunifu unaobuniwa na wanawake katika Sayansi kwasababu walio kwenye taaluma hiyo bado ni wachache.
Dr. Gideon alitoa wito kwa wananchi kuwahimiza watoto wa kike kutoka shule za chekechea na shule za msingi kuchukua masomo ya sayansi na hisabati ili kujenga msingi imara katika siku zijazo.
“Wahimize watoto wa kike kuanzia ngazi ya msingi kupenda masomo ya sayansi na hisabati na matokeo yake yataonekana siku za usoni.” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...