NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA


WAKATI serikali ikikuna kicha kusaka mwarobaini wa kukomesha mauaji, watu 9 mkoani Mwanza wanashikiliwa na na jeshi la polisi, wakihusishwa na matukio tofauti ya mauaji ya watu wawili katika wilaya za Sengerema na Nyamagana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Ramadhan Ng'anzi,leo akizungumza na waandishi wa habari,alisema katika tukio la kwanza wanawashikilia watu wanne wanaodaiwa kumwua dereva taxi Respikius Anastaz (55), mkazi wa Isamilo jijini Mwanza.

Alisema marehemu huyo huyo aliuawa, Januari 26, mwaka huu, majira ya 4:00 katika Kijiji cha Kasungamile,Wilaya ya Sengerema,ambapo mwili wake uligunduliwa na polisi waliokuwa doria usiku baada ya kulikuta gari lake likiwa limeegeshwa katikati ya barabara.

Ng’anzi alisema marehemu Anastaz alikodiwa na mtuhumiwa Sylivester Renatus akiwa na mkewe Elizabeth Jackson kutoka eneo la Buzuruga Mwanza kwenda Sengerema,walipofika maeneo ya msituni katika Kijiji cha Kasungamile walitekeleza unyama huo.

Alieleza kuwa baada ya kufanya mauaji hayo inadaiwa watuhumiwa walikwenda kwa mganga wa kienyeji aitwaye Ryabakamba Sekelwa ambaye amekamatwa pamoja na mumewe ili wakasafishwe.

Kwa mujibu wa Ng’anzi mauaji hayo yalifanyika ndani ya gari namba T.143 DHV,aina ya IST lililokuwa likiendeshwa na marehemu Anastaz,ambapo kabla watuhumiwa walimkaba kisha walitumia kamba ya manila kumnyonga,wamlichoma visu shingoni,pia walimtoboa macho na kumkata sehemu za siri.


Alisema baada ya kubaini mauaji hayo walifuatilia na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa pamoja na mganga wa kienyeji na kueleza chanzo cha tukio hilo ni kupora gari .


Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi gari limepatikana likiwa limefungwa namba bandia mbele na nyuma ( T 620 CGN) na eneo la tukio kulipatikana visu viwili,panga,nyundo na simu mbili aina ya TECNO moja kubwa na nyingine ndogo pamoja na kamba moja.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Robert Daud(42),mume wa mganga wa kienyeji,Sylivester Renetus (30),Ryabakamba Sekelwa (30) ambaye ni mganga wa kienyeji na Elizabeth Jackson (23), wote wakazi wa Katunguru wilayani Sengerema.


Katika tukio hilo la pili lilitokea Januari 29,mwaka huu,majira ya saa 1:30, huko mtaa wa Ng’washi,Kata ya Buhongwa,Wilaya ya Nyamagana,Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt.Augustine (SAUT),Mwanza,Nicholus Telesphory (25),mkazi wa Malimbe,anadaiwa kuuawa na kundi la wahalifu kwa kupigwa mawe na fimbo sehemu mbalimbali mwilini mwake na kusababisha kifo chake.

Alisema marehemu huyo aliuawa na watuhumiwa hao wakimtuhumu kuiba televisheni ambapo alifariki dunia baadaye wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza,Sekou Toure.

Ng’anzi alisema upelelezi wa uliofanywa na polisi uliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa watano wanaodaiwa kuhusika kwenye tukio hilo na kuwataja kuwa ni Thobias Lucas au Joseph (25),mkazi wa Nyanembe,Alex Madoshi almaarufu Junior (20),Yusuph Mwandesha(25) na Nyanda Madirisha (19),wote wakazi wa Ng’washi,Samwel Masalu au George (25),mkazi wa Lwanhima na waendesha bajaji.

Kamanda huyo wa polisi alisema chanzo cha tukio hilo ni watuhumiwa kujichukulia sheria mkononi ambapo polisi wanakamilisha upelelezi wa mashauri hayo ya mauaji ili kuwafikisha watuhumiwa wote mahakamani hatua kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.Aidha Ng’anzi alitoa onyo kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuwania mali waache mara moja kwani ni kosa kisheria, wakibainika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...