Na Muhidin Amri,Nyasa.


WAKALA wa Barabara nchini (Tanroads) imepiga hatua nyingine, baada ya kukamilisha ujenzi wa daraja la urefu wa mita 98 katika mto Ruhuhu linalounganisha wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma na Ludewa mkoa wa Njombe .

Baadhi ya wahandisi wa Tanroads kutoka mikoa mbalimbali nchini walioshiriki kujenga daraja hilo walisema, kukamilika kwa daraja hilo ambalo limejengwa kwa ubora wa hali ya juu na wahandisi wa Kitanzania ni mafanikio makubwa kwa Serikali ya awamu ya sita.

Mhandisi Mwandamizi wa Tanroads Makao makuu Secilia Kalangi alisema, daraja la Ruhuhu limejengwa kwa vyuma badala ya zege na wataalam wa Kitanzania kutoka mikoa 26 ya Tanzania kwa kushirikiana na wataalam wa Tanroads makao makuu.

Kalangi alisema, daraja limekamilika kwa asilimia mia moja na ameipongeza wakala wa Barabara nchini( Tanroads) kuwaamini waandisi wake ambao walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ujenzi wa mradi huo muhimu kwa uchumi unakamilika kwa wakati.

Kalangi ambaye alikuwa kiongozi wa Timu ya waandisi hao, ameishukuru Wizara ya Ujenzi kuwapa dhamana ya kutekeleza mradi huo mkubwa ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu na wananchi wa mikoa hiyo miwili.

Alisema, hatua ya serikali kuwatumia wahandisi wa ndani imesaidia kuokoa fedha nyingi kama ingewatumia wakandarasi wa nje,pia daraja hilo limetumika kama sehemu ya mafunzo kazini kwa waandisi wazalendo katika kujenga madaraja ya aina hiyo ambayo ni machache hapa nchini.

Aidha alisema, sehemu hiyo ilikuwa shida kupitika kutokana na kuwepo kwa wanyama wakali hasa mamba na viboko ambao walitishia na kupoteza maisha ya wananchi wengi walipotaka kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Ndiyo maana,serikali iliamua kujenga daraja kutokana na changamoto ya usafiri kati ya mkoa ya Ruvuma na Njombe na baada ya kukamilika limerudisha matumaini kwa wananchi wa mikoa hiyo ambao wameanza kufurahia matunda ya Serikali yao.

Mhandisi Vicent Shirima kutoka Tanroads mkoa wa Njombe, alitaja fursa zinazoweza kupatikana baada ya kukamilika kwa daraja ni pamoja na kusafirisha makaa ya mawe yanayochimbwa kwa wingi wilaya ya Ludewa kwenda Bandari ya Mtwara .

Shirima alitaja manufaa mengine ni kuwawezesha wakulima,wafanyabiashara na wananchi kusafirisha mazao na bidhaa zao kwenda katika mikoa mbalimbali nchini kutafuta masoko na amewataka kutumia daraja hilo kuongeza uzalishaji na kufanya biashara,badala ya kuacha fursa hiyo ikiwanufaisha watu kutoka nje ya mkoa huo.

Naye Mkuu wa kitengo cha mipango Tanroads mkoa wa Ruvuma Msama Msama alisema,daraja hilo linatimiza adhima ya Tanroads kuunganisha watu wa sehemu moja na nyingine, kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Nchi kwa ujumla.

Alisema,daraja la Ruhuhu limejengwa katika nguzo kuu nne zilizobebwa na msingi wenye nguzo nyingine ndogo(Piles)48 na umegharimu jumla ya Sh.8,976,808,037.64.

Kwa mujibu wa Msama, baada ya kukamilika kwa ujenzi huo kilichobaki ni wananchi wenyewe kutumia fursa hiyo kusafirisha bidhaa kwani limekuwa mkombozi mkubwa kwao.

Amewataka,wananchi wanaoishi vijiji jirani vya Lituhi kwa upande wa Nyasa na Kipingu Ludewa kulinda daraja hilo kwa kuwa ni mkombozi mkubwa kwao, hivyo lazima walilinde kwa gharama yoyote ili liwasaidie katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kutambua kuwa Serikali imetumia fedha nyingi.

Kwa upande wake Mhandisi Geroge Nyagaboma kutoka Kilimanjaro alisema,watatumia ujenzi wa daraja la Mto Ruhuhu kama sehemu ya mafunzo kazini kwa kujenga madaraja mengine hapa nchini kwa weledi mkubwa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kipingu kata ya Manda wilayani Ludewa Elasmus Mbeya,amefurahishwa na hatua ya Serikali kukamilisha mradi huo ambao umerahisisha mawasiliano kati ya mkoa wa Njombe na Ruvuma ambayo inategemeana katika mambo mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.


Daraja la Mto Ruhuhu  linalounganisha wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma na Ludewa mkoa wa Njombe lililojengwa na Wahandisi wa Tanroads kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara kama linavyoonekana baada ya kukamilika rasmi ambapo limeanza kutumika kwa ajili ya  shughuli mbalimbali za kiuchumi  kwa wananchi wa mikoa hiyo miwili.Baadhi ya Wahandisi  kutoka Wakala wa Barabara nchini(Tanroads) Secilia Kalangi,George Nyagaboma na Msama Msama wakiangalia sehemu ya daraja la mto Ruhuhu linalounganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma baada ya kumaliza kazi ya ujenzi wa Daraja hilo ambalo limegharimu zaidi ya Sh.bilioni 8.
Waandishi walioshiriki kujenga daraja la Mto Ruhuhu linalounganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma, kutoka  kushoto Vicent Shirima wa Tanroads mkoa wa Njombe,Mhandisi Mwandamizi Secilia Kalangi wa Makao makuu ya Tanroads,Msama Msama kutoka mkoa wa Ruvuma,na Geroge Nyagaboma kutoka mkoa wa Kilimanjaro  na Afisa Uhusiano wa Tanroads Lela Haji wakitembea juu ya daraja hilo baada ya kukamilika rasmi ujenzi wake na kuanza kutumika.
Kivuko cha Mv Ruhuhu kilichokuwa kikifanya kazi ya kusafirisha watu na mizigo katika Mto Ruhuhu kikiwa kimepaki baada ya kukamilika kwa Ujenzi wa Daraja katika mto huo.

Picha na Muhidin Amri

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...