Adeladius Makwega,DODOMA.

Kwa muda mrefu rafiki yangu anayefahamika kama Kassimu Awadhi ambaye tulijaliwa kusoma shule ya sekondari ya Tambaza kwa wakati tofauti aliniuliza habari za kabila la Wakimbu ambapo yeye ni kabila la upande mmoja wa mama yake mzazi. Ndugu yangu huyu alikuwa na kiu ya kujua angalau chembe ya utamaduni wake.

Ili kuipooza kiu hiyo ya kulifahamua kabila hili, mwanakwetu leo natembelea mbuga ya kabila hili kwa kiasi tu.

Kabila wa Wakimbu linapatikana katika mikoa kadhaa ya Tanzania, nayo ni Singida (Manyoni), Mbeya (Chunya), Songwe (Songwe) na Tabora (Tabora). Kama walivyo Wanyamwezi, Wakimbu ni kabila lenye machifu wengi. Huku ikiaminika kuwa walikuwa na machifu wanaowongoza katika koo 38.

Eneo la kabila hilli kwa kaskazini kuna Mito Wala, Midiho na Nyahua, mashariki kuna Mto Kisigo na Njombe. Kwa Magharibi kuna Mto Rukwa na Rungwa unaoelekeza maji yake kwa kaskazini ya Mto Ugalla. Hii ni kulingana na maandishi ya B. Mvellengi juu ya Wakimbu na Ushirikina.

Kwa ndugu hawa, ukilitazama eneo lao hilo la kijografia wapo jirani na makabila mengi lakini kwa karibu mno ni Wanyamwezi, huku lugha zao zikikaribiana mno.

Wakimbu wa Tabora wanatafautiana na Wakimbu wa Mbeya, Songwe na Singida kwa matamshi ya baadhi ya maneno lakini kwa hakika watu ni wale wale.

Wakimbu wa Tabora waliathirika mno na tabia za Wanyawezi wa Unyenyembe. Nako eneo la Kiwere na Kambi Katoto ambalo lipo huko Chunya, Wakimbu hawa pia wameathirika pia na Unyamwezi na ndiyo maana baadhi yao unaweza kusikia akakwambia kuwa mimi ni Mnyamwezi wa Chunya kumbe kiukweli ni Mkimbu.

Kabila la Wakimbu katika masuala ya utani pia wanao lakini si kwa kiasi kikubwa mno. Utani kwao wanaita LUPIGO. Kulingana na mila za Kikimbu mahusiano mema yalisisitizwa tangu enzi na kusaidiana katika shida mbalimbali kama vile ugonjwa na misiba.

Kusaidiana huko kwa Kikimbu kunaitwa BUSENGANYA ambapo kunajegwa katika utani na majirani zao wote wanaopakana na kuishi nao, hata kabla ya kuingia kwa wakoloni.

Lupigo unafanyika katika hatua tatu nazo ni kati ya ndugu wa familia moja, kati ya koo na koo na kati ya kabila zinazozungukana na kuishi na kushirikiana nao pamoja na hata makabila yaliyo mbali nao.

Kwa kulitazama kabila hili, jambo ambalo limebebwa mno ni namna linavyojihusisha na imani za Uganga na Ushirikina kama zilivo jamii nyingi za kiafrika,

Kumekuwa hakuna utafauti mkubwa baina ya Ushirikina na Uganga wa kienyeji, mambo haya yamekuwa yakihusianishwa kwa pamoja kwa muda mrefu mno. Huku Waganga wakidai kuwa wao wanatibu tu na kuzuia mabaya yasimkute binadamu.Kwa kabila hili ushirikina huo huitwa BULOGI.

Kuna kisa kimoja, inadaiwa kuwa watoto walikuwa wakicheza porini, wakiwa katika mchezo huo kwa furaha. Mtoto mmojawapo aligongwa na nyoka. Mtoto huyo alibebwa na kurudishwa nyumbani na kupatiwa matibabu. Mara baada ya mtoto kupona, wazazi wa mtoto huyo walikwenda kwa mganga kuuliza, je kwanini nyoka huyo alimgonga mtoto wao na si mtoto mwingine? Swali hilo lilipofika kwa mganga lilipata majibu.

Hoja ya kujiuliza, je wazazi hao hawakutambua kuwa mtoto wao kwa kucheza katika pori hilo alikuwa katika eneo hatarishi la kugongwa na nyoka? Hii inaonesha wazi juu ya Wakimbu na makabila mengi ya kiafrika kuwa na imani kubwa na ushirikina kwa kuwa ni utamaduni wetu.

Kwa jamii nyingi za kiafrika kila jambo ambalo linatokea huwa na mkono wa mtu na ndiyo maana hata mganga alipofuatwa kwa kisa hicho cha mtoto aliyegongwa na nyoka kwa hakika mbaya alipatikana. Katika hili mwanakwetu wewe fikiria matukio yoyote unayoyakumbuka hapo ulipo, utaambiwa hili kafanya yule na lile kafanya fulani. Muda mwingine hayo yanayodhaniwa huwa kweli mwanakwetu, narudia kusema huwa kweli mwanakwetu. Huo ndiyo utamaduni wetu.

Kulingana na Wakimbu suala la mtu kumloga mwenzake linaaminika kufanywa kwa sababu kadhaa; Wivu, ugomvi na kuna wakati mwingine huwa hakuna sababu yoyote ile ya msingi.

Kulingana na maandishi ya B. Mvellengi anasema wazi kuwa hili mtu kuwa mshirikina/mganga ana wajibu mkubwa kwanza wa kushirikiana kwa kipindi fulani na ndugu hao. Hapo hufanya kazi ya kuwa msaidizi wao.

“Mtu akishirikiana nao na yeye ndiyo hufundiswa taratibu kadhaa za mambo hayo kwa kina na yeye kuweza kufuzu mafunzo hayo na kukabidhiwa mikoba. Lakini wengine hukabidhiwa kwa kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine yaani kwa babu, baba na hadi kijukuu na kitukuu /Bibi, mama, shangazi/mama mdogo hadi kijukuu na mwanafunzi huyo anaitwa BUHEMBA/MUHEMBA.”

Katika hili pia kumekuwepo na mabingwa wa kuwatambua wachawi hao ambapo wao huwa na nguvu ya juu zaidi ya hao washirikina na ndugu hawa huwa na uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali, Wakimbu humuita KAMCHAPE.

Neno Kamchape linatokana na neno la Kiswahili CHAPA hapo kwanza inaondolewa irabu A mwisho wa neno hilo na kunaongezewa silabi KA mwanzoni mwa mzizi wa kitenzi –CHAP- na kuongezwa Irabu E mwisho wa mzizi wa neno na kutokea neno jipya KAMCHAPE ilikuonesha tendo la kwenda kumuadhibu huyo mhusika.

Kamchape huifanya kazi hiyo huku akiwa na vifaa na dawa kadhaa na huku na yule anayedhaniwa kuwa mchawi anapolishwa dawa hizo kama ataendelea na ushirikina huo inaaminika kuwa anaweza kufa.

Katika hili kuna baadhi ya watu wanaamini pia ilisaidia baadhi ya watu kuwa wema, kwani waliogopa kutendeana mabaya na mtu anatambua kuwa nikimfanya mwezangu hivi anaweza akalogwa na kufariki au kujulikana ni mchawi.


Basi mwanakwetu hao ndiyo Wakimbu na Kamchape wao.

Kwa ndugu yangu Kassimu Awadhi na Wakimbu wote nasema kuwa wakati naandaa matini hii pia nilikumbushwa kuwa mna utani na Wazaramo.


Kwa leo naishia hapo, nakutakieni siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257 




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...