Adeladius Makwega-MOROGORO

Kwa wale wasomaji wa matini zangu nawakumbusha kuwa mwishoni mwa Februari 2022 niliwasimulia juu ya basi la abiria lilivyoharibika na kukutana na mama yule aliyenisimulia juu ya Khanga ya Dharura ya bintiye ambaye anaitumia kukalia chini darasani.

Mwishoni mwa juma hili nilijaribu kupita eneo hili na kupepesa macho lakini sikuweza kumona mama huyu. Nilisogea kando, nilikutana na jamaa ambaye alikuwa anachoma mahindi, nilitoa Tsh 500/- na kupatiwa hindi la kuchoma.

Nilitafuna hindi hilo taratibu, huku nikipiga soga na ndugu hawa, nilijulishwa kuwa eneo hilo linafahamika kama Mkundi Sheli. Niliuliza kuwa hapo pana shule ngapi za Sekondari za Umma? Nilijibiwa kuwa zipo mbili, Shule ya Sekondari KINGO na nyingine ni shule ye Sekondari MKUNDI.

Nikiwa hapo nilibaini kuwa kata hii inaitwa kata ya MKUNDI, KINGO ni kata nyengine ya Wilaya ya Morogoro ambapo walijenga shule yao eneo hilo kwa kuwa katani kwao walikosa maeneo katika ule mpango wa kila kata shule ya sekondari ulioanzishwa na kusimamiwa kwa karibu mno na Mjomba Jakaya Kikwete.

Nikiwa hapa nilitumia kama dakika kumi na tano kutafakari kujua hali ya shule hii ya Kingo, niliamua kununua mahindi mengine matano ambayo hayajachomwa yakiwa mabichi kwa shilingi Tsh 2500/-Kitendo hicho kilimroga jamaa huyu, kweli niliamini kuwa fedha ni uchawi wa Kizungu.

“KILA MTU ANANUNULIKA, SHIDA NI DAU TU.”

Niliyakumbuka maneno haya ambayo niliambiwa na rafiki yangu mmoja mwaka 2011.

Nilimuuliza huyu jamaa, nia yangu ya kutaka kumuhamishia binti yangu shuleni ya sekondari KINGO lakini je wana walimu wa kutosha? Je wana madawati?

Ndugu huyu akasema kaka hilo dogo sana, kuna jamaa hapa AMEKWENDA KWA OMARI KIJANA akirudi tunalimaliza na majibu utapata. NiIimuuliza kwa hiyo Omari Kijana ni jina la nani?

“Hilo ni jina la eneo huko machakani.”

Jamaa huyu alinijibu. Mara muungwana huyu alirudi na alielezwa nia yangu, akajibu hilo dogo sana.

Muda huo wanafunzi walikuwa wakitoka shuleni, akamuita jina kijana mmoja akiwa na sare za shule huku akiwa na kundi la wenzake. Kwanza akawapa vipande vya mahindi akiwauliza.


“Eti mmeshapata madawati?”

“Ah kaka bado, hayapatikana hadi sasa, tunakaa chini.” Alijibiwa.

“Pale tuna mkondo A, B na C na kila mkondo tupo 100 huko C wanakaa chini kabisa na kuna vumbi kibao sisi C tunakuita KARIAKOO.” Alisema mwanafunzi huyu.

Kijana huyu alisema kwa utani kama hamna madawati basi mbebe vibao vya mbuzi na stuli kutoka nyumbani. Binafsi nikamjibu vitawachoma, vibao vya mbuzi ni kama kisu wasije kugombana wakachomana bure.

“Wenzetu wa shule ya MKUNDI wana majengo mazuri na wanayo madawati hadi kidato cha nne. Huku kidato cha pili, kidato cha tatu na cha nne hayatumiki maana ndiyo kwanza shule hii imeanza. “ Alidakia mwanafunzi mwingine.

“Kazi nyepesi kabisa, unayachukua madawati kadhaa ya shule ya MKUNDI unayapeleka pale shule ya KINGO mchezo unakwisha kabisa.”

Alisema muuza mahindi.

Binafsi niliwaaga na kuondoka zangu. Nikapanda Hiace huku natafakari mwenyewe.

”Mathalani binti aliyepevuka akiwa amekaa chini alafu mwalimu kauliza swali, binti kanyoosha mkono, mwalimu kamruhusu ajibu swali hilo, mpaka atakaposimama kama yupo kwenye dharura hali inakuwaje?”

Hiace hii ilikuwa inasonga mbele tu na mahindi yangu mabichi nikiyashika nganganga mkononi.

“Hata mwanafunzi wa kiume, kaptura yake ni ya zipu au vifungo kunyanyukanyanyuka kutoka chini kwenye sakafu hadi juu kujibu swali la mwalimu ni hatari sana kwa utu wake kifungo au zipu inaweza kukatika na duka likawawazi, hilo linaweza kumfedhehesha mwanafuzi wetu.”

Nikiwa nayawaza haya nilishukuru Mungu kupata jibu hilo.

Kwa hiyo Jumatatu nitakwenda Ofisini kwa Afisa Elimu wa Mkoa wa Morogoro na baadaye Afisa Elimu wa Halmashauri ya Morogoro kumuhamishia mwanangu shule ya MKUNDI.

Nilipata usingizi huku Hiace hii ikiendelea na safari.


makwadeladius@gmail.com

0717649257


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...