NA WU, NAPOLI ITALY.
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Watanzania nchini Italy, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, jumamosi ya tarehe 26/03/2022 amekutana na Watanzania wanaoishi Napoli na vitongoji vya Mkoa wa Campania Nchini hapa.
Mhe. Mahmoud Thabit Kombo tangu amefika nchini Italy miezi takriban mitano sasa, mbali na majukumu yake makubwa ya kitaifa lakini pia amekua akiendelea kukutana na Watanzania wanaoishi Italy, kwa dhamira kubwa ya kuwatambua, kuwasikiliza changamoto zao pamoja na kuwapa taarifa mbalimbali zinazohusu fursa za Diaspora zinazopatikana nyumbani Tanzania.
Mkutano wa Watanzania Napoli umepata muitikio mkubwa baada ya muda mrefu wa janga la Uviko lililosababisha kuzuiliwa shughuli zote za mikusanyiko.
Watanzania wa Napoli katika risala yao iliyo sheheni mambo mengi, historia, mafanikio pamoja na changamoto zao, walimpongeza na kumshukuru Balozi kwa kuonyesha kuwajali Watanzania wote wanaoishi nchini Italy
Ambapo ameendelea kusisitiza uimara wa jumuiya zao zinazo waunganisha pamoja, sambamba na kuchagua viongozi wenye sifa na mvuto unaoweza kuwakusanya watu pamoja.
Mhe. Balozi amewahakikishi kama mlezi wa jumuiya zote za Watanzania Italy kuwa pamoja nao kwenye kila jambo lenye tija kwao na kwa taifa.
Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewahakikishia Watanzania kuwa milango ya ubalozi iko wazi kwa yeyote mwenye kuhitaji huduma za uwekezaji Tanzania na kutilia mkazo suala zima la Diplomasia ya Uchumi ambayo yeye kwake ni moja ya kipaumbele cha majukumu yake.
Balozi Mhe. Kombo amebainisha hayo baada ya wakati wa maswali na mijadala wadau walisema kuwa wapo Wataliani ambao wameonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika sekta za afya na wanahitaji kupata maelezo zaidi na taratibu za kisheria za nchi katika uwekezaji huo.
Balozi alipata nafasi pia ya kuulizwa maswali mbalimbali ambayo yote aliyapatia majawabu lakini pia alipokea mapendekezo na ushauri uliotolewa na wadau wa Diaspora.
Balozi pia aliendelea kusisitiza kwa Watanzania wote kuendelea kulinda heshima ya nchi yetu huku ugenini na kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu popote walipo.
Mwisho wa risala ya Watanzania nao walimpongeza Mh Balozi kwa kuteuliwa na kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kuwa balozi nchini Italy,
vilevile walimshukuru kwa kutenga muda wake na kukubali mualiko wa mkutano.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...