Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha akionyesha baadhi ya takwimu zilizokuwa kwenye ripoti hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam wakati akizindua ripoti ya matokeo ya utafiti wao kwa kipindi cha mwaka mwaka 2021.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikizidi kupambana katika kukabiliana na suala la kulinda mazingira hususan kuzuia matumizi ya plastiki, lakini imebainika kuwa kuna kampuni kubwa 10 ambazo ni vinara zinazoendelea kuzalisha bidhaa hizo.
Hayo yamebainishwa na Taasisi ya Nipe Fagio ambayo imekuwa ikifanya kazi za kusafisha maeneo ya fukwe na kutembelea maeneo ya jamii kuanzia mwaka 2018, 2019, 2020, na 2021, kwa ushirikiano na washiriki 32,151, Nipe Fagio ili kuangazia muundo wa taka nchini Tanzania.
Akizindua matokeo ya utafiti wao kwa kipindi cha mwaka mwaka 2021, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaa, Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha, amesema kupitia utafiti wao ambao waliufanya kwa muda wa miaka minne umeweza kuonyesha kuwa wazalishaji wa ndani ndio wanaoongoza kwa uchafuzi wa mazingira ambapo asilimia 75 ya taka zote zilizokaguliwa huku bidhaa za nje zikichukua asilimia 25.
“Uchambuzi wetu umebaini kuwa wachafuzi 10 wanaoongoza kwa uchafuzi wa plastiki nchini ni: Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL), Bakhresa food products limited, U Fresh food limited, Chemi & Cotex limited, Watercom limited, Unilever limited, The Coca-cola. kampuni, Tanzania distillers limited, SBC Tanzania limited na Tanzania Breweries Limited,” amesema Rocha.
Rocha amefafanua kuwa mwaka wa 2021, umekuwa mwaka muhimu zaidi wa kufanya mashirika yanayozalisha plastiki kuwajibika kwa mchango wao katika mabadiliko ya hali ya hewa wakati viongozi wa duniani na kwamba walikutana katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) kujadili jinsi ya kupunguza joto duniani. 1.5°C.
Na sasa, mnamo 2022, tulipata azimio la "Kukomesha Uchafuzi Utokanao na Plastiki: Kuelekea Azimio la kisheria la kimataifa” lililoidhinishwa katika mkutano wa UNEA 5.2 na kuchukuliwa kuwa ni makubaliano muhimu zaidi kuchukuliwa tangu makubaliano ya Paris. Azimio hili linalenga mzunguko mzima wa maisha ya plastiki, kutoka uzalishaji hadi utupaji, na inatambua umuhimu wa Waokota Taka na wafanyakazi wasio rasmi kwa kurejesha taka.
“Kwa mujibu wa uchambuzi wa taka na chapa tulioufanya katika kipindi cha miaka 4 kati ya 2018 na 2021, tuligundua kuwa kampuni za Mohammed Enterprises Tanzania Limited na Bakhresa Food Products Limited zimeongoza kwa kuwa wachafuzi wakubwa wa plastiki nchini Tanzania. Huku kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited ikiongoza kwa miaka 3 mfululizo,"alisema.
"Kuchambua takwimu tulizonazo mkononi, kwa hali ya kawaida haitoshi tu kutegemea juhudi za urejeshaji taka pekee ili kushughulikia uchafuzi wa mazingira na mgogoro wa hali ya hewa unaosababishwa na vifaa hivi vya plastiki vinavyotumika mara moja," ameongeza.
Rocha amepongeza juhudi za serikali katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira kutokana na bidhaa za plastiki lakini pia akahimiza kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kukomesha tatizo la matumizi hayo.
"Tunafahamu na tunathamini hatua ambazo serikali tayari imechukua kupunguza matumizi ya plastiki. Hasa kwa kupigwa marufuku kwa mifuko ya mboga ya plastiki na marufuku inayotarajiwa ya kanga laini za plastiki zinazofunika chupa za vinywaji vya plastiki na chupa,"ameongeza. Alisema kwamba hata hivyo wanaamini jitihada zaidi zinaweza kufanyika ili kumaliza tatizo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo, baada ya kutembelea maeneo zaidi ya 350,000 na kuchambua vipande vya taka, matokeo yanaonyesha kuwa kwa wastani, asilimia 64 ya taka kwenye mifuko ya sampuli iliyokaguliwa ni taka za plastiki.
Wanasema mbali na hili katika kipindi cha mwaka 2021 taka za plastiki zilichangia asilimia 76 ya taka zote zilizokusanywa, asilimia 42 zikiwa ni taka zitokanazo na makampuni mbali mbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...