Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema katika kipindi Cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita kuwa madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan sekta ya afya imepewa umuhimu mkubwa na limefikiwa kwa kiwango kikubwa kama ambavyo Ilani ya CCM imeahidi

Akizungumza ikiwaimebaki siku moja Rais Samia kutimiza mwaka mmoja ambazo ni sawa na siku 365 akiwa madarakani,Chongolo amesema Chama chao kimeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Ilani na katika sekta ya afya kumeimarishwa na lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi.

"Hospitali za rufaa za mikoa 19 ziko katika hatua mbalimbali za kukamilisha ujenzi na ukarabati wake. Kuna miradi ipatayo 127 ya ujenzi wa hospitali inaendelea katika halmashauri za wilaya nchini, halikadhalika kuna ujenzi wa vituo vya afya vipatavyo 233 katika tarafa 207, vyote hivi vina uwezo wa kufanya upasuaji, vikiwa na majengo ya OPD, Maabara na vichomea taka.

"Bila kusahau ujenzi wa zahanati zipatazo 564 katika halmashauri mbalimbali nchini ambao uko katika hatua za kukamilika.Katika eneo la upatikanaji wa dawa ili kuondokana na malalamiko ya wananchi, mbali ya Serikali kutumia takriban Shilingi bilioni 333 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendenashi, inajenga viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba katika eneo la Idofi, Halmashauri ya Makambako, mkoani Njombe kwa lengo la kupunguza ununuzi wa dawa kutoka nje ya nchi,"amesema Chongolo.

Ameongeza hatua hiyo itasaidia kuimarisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kununulia dawa nje ya nchi na hivyo fedha itakayookolewa itaelekezwa katika mipango mingine ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Aidha Chongolo amesema katika sekta ya maji Ilani ya CCM katika ukurasa wa 147 – 150, inatamka kuwa uimarishaji wa huduma ya maji ni mojawapo ya agenda za kudumu za CCM tangu tulipopata uhuru, kwa sababu wanatambua maji ni msingi wa uhai wa binadamu na injini ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani uhakika wa upatikanaji wake, yakiwa safi na salama, huchangia katika kuzuia magonjwa, na hivyo kuimarisha afya na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

"Mwaka 2020 kupitia Ilani ya Uchaguzi, tumewaahidi wananchi kuwa tutaielekeza Serikali kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na usalama wa maji na huduma hiyo iwafikie zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini ifikapo mwaka 2025. Kazi kubwa inaendelea kufanywa nchi nzima, ikiwemo ile ya ujenzi wa miradi mikubwa ya maji nchi nzima,"amesema.

Kuhusu mindombinu ya usafirishaji na uchukuzi – barabara, reli, anga na majini amesema katika ibara ya 55 hadi ya 96, Chama Cha Mapinduzi kiliweka ahadi kwa wananchi kuhusu namna kitakavyoboresha na kufungua mazingira ya ustawi wa wananchi kuendeleza uzalishaji kwa ajili ya kuongeza kipato na fursa mbalimbali za shughuli za kiuchumi, kupitia sekta za ujenzi wa miundombinu, uchukuzi na mawasiliano.

Amesema a katika mwaka huu mmoja, eneo hili nalo limefanyiwa kazi kwa kiwango ambacho CCM inaridhika nacho. Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la kisasa la Tanzanite jijini Dar es Salaam sambamba na barabara unganishi zenye urefu wa km 5.2 kwa jumla ya Tsh. 243 bilioni.

Pia ujenzi wa miradi mikubwa ya Daraja la Magufuli lililoko Kigongo-Busisi, Mwanza, Daraja la Mto Wami, mkoani Pwani, unaendelea katika hatua mbalimbali, ambapo Busisi ujenzi uko asilimia 40 na Wami ujenzi uko asilimia 75 na wakandarasi wako kazini.

"Tunapozungumza hapa ukanda wa magharibi mwa nchi yetu unazidi kuunganishwa na kufunguliwa fursa mbalimbali baada ya kukamilika kwa Barabara ya Katavi – Tabora huku Barabara ya Kakonko hadi Kasulu ujenzi wake ukiendelea kwa kiwango cha lami.

" Ni hivi karibuni tu Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje yenye urefu wa kilometa 112.3 katika Jiji la Dodoma. Kwa upande wa usafiri wa anga, miradi ya ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri na usafirishaji imefanyika na mingine inaendelea katika hatua za utekelezaji katika mikoa mbalimbali nchini mfano;

"Kiwanja cha Ndege cha Songea (asilimia 95), Mtwara (asilimia 85), Iringa (asilimia 33.42), Musoma (asilimia 04), pamoja na ujenzi wa jengo la abiria katika kiwanja cha ndege cha Songwe (asilimia 81)."

Kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato Mkoani Dodoma , Chongolo amesema ulipaji fidia umekamilika kwa asilimia 98, mkataba wa awamu ya kwanza wa ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege umesainiwa tayari na mkandarasi amekabidhiwa eneo la mradi mapema mwaka huu.

Ameongeza mwaka huu mmoja pia wameshuhudia ujenzi na ukarabati wa bandari za TPA na zingine ndogo ndogo, huku tukijionea mafanikio ya ukarabati wa Bandari ya Mtwara katika kurahisisha uchukuzi na usafirishaji na kuifungua mikoa ya Kusini.

Pia ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea vizuri ambapo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi huo kipande cha kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora chenye urefu wa Kilometa 368 katika kipande cha tatu cha mradi huo (Lot III), alisisitiza kuwa lazima utatekelezwa hadi kumalizika kwa namna yoyote ile.

"Chini ya usimamizi na uongozi wake, Mheshimiwa Rais amesaidia kuwepo kwa mazungumzo kati ya nchi nne, Tanzania, Congo DRC, Burundi na Rwanda, ili kushirikiana kufikisha SGR katika nchi hizo na kuunganisha sekta ya uchukuzi na usafirishaji, ambapo kwa upande wa Congo DRC itaunganishwa kwa kipande cha Kaliua, Mpanda kupitia Bandari za Karema na Kalemie.

" Burundi itaunganishwa kupitia Uvinza (Kigoma) hadi Musongati (Burundi) huku Rwanda ikiunganishwa kupitia Isaka (Shinyanga) hadi Kigali. Hakika kazi inaendelea. Aidha, kumekuwa na ukarabati na ujenzi wa meli na vivuko katika maeneo mbalimbali nchini ili kufanikisha usafiri na uchukuzi kupitia njia za majini.

Akizungumza eneo la nishati amesema kutokana na umuhimu wa kimkakati wa sekta ya nishati, kwenye Ilani ya 2020 – 2025, CCM ilikusudia kuimarisha zaidi eneo hilo, ili kuhakikisha nchi inazalisha umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda na hata soko la nje ya nchi yetu.

"Ni kutokana na maelekezo hayo Watanzania wameshuhudia katika mwaka huu mmoja, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais imechukua hatua madhubuti katika eneo hili pia, kuondoa changamoto ya umeme nchini kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme pamoja na kuongeza vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo ili kuhakikisha maeneo yote ya nchini yanapata umeme wa uhakika hususan maeneo ya vijijini.

"Kazi ya kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa, hasa katika mikoa minne iliyobakia ya Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa inaendelea. Maeneo hayo yatakuwa na umeme wa uhakika kutokana na mradi wa Rusumo unaotekelezwa kwa makubaliano ya kiserikali kati ya Tanzania, Rwanda na Burundi, kuzalisha megawati 80.

"Serikali pia imeendelea kuweka mkazo katika kusimamia ukamilishaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ambao utakapokamilika utazalisha megawati 2,115. Kupitia ziara za kimkakati za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nchi, Tanzania tumefanikiwa kusaini mikataba na hati za makubaliano ya ushirikiano katika kuendeleza miundombinu ya nishati.

"Ikiwemo ya kupokelea na kuhifadhia mafuta na gesi itakayojengwa hapa hapa nchini, huku ikilenga kuhudumia ukanda mzima wa Afrika Mashariki.Aidha, tumeona pia dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG), unaanza ili kupanua wigo wa uzalishaji wa nishati ya kutosha na uhakika,"amesema na kuongeza hadi sasa mradi huo umefikia katika hatua ya majadiliano ya kimkataba na wawekezaji. 



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...