MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imetanabaisha mafanikio yaliyopatikana kwenye mamlaka hiyo kwa mwaka mmoja wa Madaraka ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza usanifu kwenye tabiri za hali ya hewa nchini.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa Mwaka mmoja wa Rais Samia umeleta mabadiliko chanya kwa kuboresha miundombinu , kuongeza usahihi wa utoaji wa taarifa za tabiri mbalimbali, kuboresha mazingira ya kazi, utekelezaji wa sharia, na kukubalika kimataifa.

Mamlaka hiyo inafafanua namna Rais Samia alivyoboresha miundombinu kwa muda wa mwaka mmoja kwa ununuzi wa Rada mbili (2) za hali ya hewa ambapo TMA inakwenda kukamilisha malengo yake ya muda mrefu ya kupata rada saba ambapo rada mbili zinazotarajiwa kufungwa Kigoma na Mbeya zinaundwa nchini Marekani.

Mamlaka imefanikiwa kununua kompyuta ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuchambua taarifa za hali ya hewa (Computer Cluster) na hivyo kuipa Mamlaka uwezo wa kutoa utabiri maalum kwa maeneo madogomadogo na katika kipindi hicho Mamlaka imeanza kutoa utabiri wa msimu katika ngazi ya Wilaya kwa wilaya zote nchini.

Mamlaka imeendelea na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya hali ya hewa ikiwemo mitambo sita (6) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika (mobile Automatic Weather Stations), vifaa 15 vya kupima mgandamizo wa hali ya hewa na mitambo minne (4) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe.

Aidha Mamlaka inaeleza kuwa imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kukarabati vituo vitatu (3) vya hali ya hewa vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, na Tabora, pamoja na Chuo pekee cha Hali ya Hewa cha Taifa kilichoko Kigoma. Aidha, Mamlaka imeendelea na ujenzi wa kituo cha kufanya uangazi katika uwanja wa ndege wa Dodoma.

Mamlaka pia imeanza awamu ya pili ya ukarabati wa vituo vinne (4) vya hali ya hewa vilivyopo Shinyanga, Mpanda, Mahenge na Songea. Maboresho hayo yanaenda sambamba na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Mamlaka kupitia mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi.

TMA sasa inauhakika wa utabiri wake kwa kuwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa vimeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 93 ambapo kiwango kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ni asilimia 70. Ongezeko hili la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini.

Aidha, Mamlaka imeendelea kutoa utabiri wa msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa usahihi na ubora hivyo kuchangia kupunguza athari kwa watu na mali zao. Mfano: mnamo mwezi Oktoba 2021 Mamlaka ilitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli kuwa chini ya wastani hivyo kupelekea mamlaka mbalimbali kufanya maamuzi stahiki na kusaidia kuepusha madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea.

Kutokana na kujengewa uwezo na serikali katika nyanja za miundombinu, teknolojia na wataalam, Mamlaka imeanza kutoa utabiri wa msimu kwa ngazi ya wilaya ambao umekuwa na mwitikio mkubwa na watumiaji wengi.

Imeelezwa kuwa Kutokana na mamlaka kuwa na uhakika wa taarifa za tabiri zake imeendelea kukidhi Viwango vya Ubora vya Kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga na hivyo anga la Tanzania kuendelea kuaminika kuwa salama.

Katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ilifanyiwa ukaguzi mwezi Desemba 2021 na Kampuni ya Certech kutoka Canada na kwa mara ya kwanza hakukuwa na mapungufu yoyote na hivyo huduma za hali ya hewa kuonekana kuwa bora zaidi, hali iliyopelekea Mamlaka kuendelea kumiliki cheti cha ubora (ISO 9001:2015).

Katika kipindi cha mwaka mmoja cha Uongozi wa Rais Samia, pamoja na changamoto za UVIKO-19, TMA imefanikiwa kutekeleza vyema jukumu lake la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa. Ambapo wataalamu mbalimbali wa Mamlaka wameendelea kutekeleza majukumu yao katika Vikosikazi mbalimbali vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambavyo wameteuliwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Agnes Kijazi ametekeleza majukumu yake ya Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO na Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa Meteorological Association of Southern Africa (MASA). Hili lisingewezekana kama si juhudi za Mhe. Rais kuiwezesha TMA katika kipindi hicho kigumu cha UVIKO-19.

Katika Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi The twenty sixth session of the United Nations Framework Convention on Climate Change: Conference of the Parties (UNFCCC-COP26), uliofanyika Glasgow, Uingereza mwezi Novemba 2021, Tanzania kupitia Dkt. Ladislaus Changa ilipata heshima ya kuwa mwenyekiti kuongoza vikao vya majadiliano yaliyohusu masuala ya Utafiti na Uangazi wa hali ya hewa (Research and Systematic Observation). Fursa kama hii haijawahi kutokea na imetokea katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia alihudhuria Mkutano huo.

Aidha, Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea kuwa mfano mzuri katika utekelezaji wa programu mbalimbali za ushirikiano wa masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa, hatua ambayo imeifanya Tanzania kuaminiwa na kutumiwa katika kuzisaidia nchi nyingine katika maeneo mbalimbali ya kitaalamu ya kuboresha huduma za hali ya hewa.

Kwa mfano katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Tanzania kupitia TMA imezisaidia nchi za Uganda (katika masuala ya menejimenti ya taasisi ya hali ya hewa), Malawi (katika eneo la matumizi ya vifaa vya kisasa vya hali ya hewa, hususan rada za hali ya hewa), Zambia, Msumbiji, Rwanda, Burundi, na Ethiopia (katika eneo la utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa lengo la kuepusha maafa kwa kutumia mfumo wa WMO wa Common Alerting Protocol (CAP).

TMA imesema kuwa Kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya mwaka 2019 zimekamilika katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na hivyo kuimarisha shughuli za udhibiti, uratibu na utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini pamoja na kupatikana kwa vyanzo vipya vya mapato. Ukusanyaji wa mapato utaiwezesha Mamlaka kujiendesha yenyewe na hivyo kupunguza gharama kubwa za uendeshaji kutoka serikalini sambamba na kuendeleza uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Hata hivyo Mamlaka hiyo imeendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya tafiti mbalimbali katika masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, jumla ya machapisho ya utafiti manne (4) yaliandaliwa na kuchapishwa katika majarida ya kimataifa ya sayansi. Wataalamu watano (5) kutoka Zanzibar walishiriki katika tafiti hizo. Tafiti hizi zimechangia katika kuboresha huduma zinanzotolewa na Mamlaka.

Aidha, Mamlaka imekuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Masuala ya Usimamizi wa Ukanda wa Pwani na Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi kwa Zanzibar (Technical Committee of Integrated Coastal Zone Management issues and Climate Change matters for Zanzibar ICZM) pamoja na kufanikiwa kuwa mjumbe kwenye kamati ya Soil and Air Quality Technical Committee ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (Zanzibar Bureau of Standards- ZBS) na Kamati ya Tume ya Mipango Zanzibar ya kujadili mwenendo wa uchumi Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...