Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo ameamua kuanza kutoa elimu na kuhamasisha zao la Mchikichi kwa njia ya Mikutano ya hadhara ya vijiji.
Tayari Dkt. Mkamilo amefanya Mikutano mikubwa ya hadhara katika vijiji vya Lugongoni, kata ya Itebula, tarafa ya Nguruka katika wilaya ya Uvinza. Kadhalika amefanya mkutano mkubwa katika kijiji cha kandaga, kata ya Kandaga wilaya ya Uvinza.
Hatua hiyo ya Mkurugenzi Mkuu imekuja baada ya kutembelea vijiji kadhaa na kulalamikiwa na wananchi wengi kuwa hawafahamu mbegu bora za Mchikichi aina ya Tenera.
Mikutano hiyo ambayo imeonesha kujaza watu wengi na kuwa na mafanikio makubwa imeandaliwa na viongozi wa vijiji husika kwa kushirikiana na TARI na kuhudhuliwa na wananchi wote wakiwemo wakulima.
Dkt. Mkamilo alifanikiwa kutembelea mashamba na vikundi mbali mbali vya wakulima pamoja na kupokea changamoto kutoka kwa wakulima na wananchi ambazo asingeweza kuzipata bila Mikutano hiyo ya hadhara. Changamoto hizo aliziwasilisha kwa uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa hatua zaidi.
Wakizungumzia changamoto, wakulima na wananchi wa vijiji hivyo wamemwambia Mkurugenzi Mkuu kuwa hawana mbegu bora za Mchikichi aina ya Tenera huku wengine wakidai kuwa wamesikia uwepo wa mbegu hizo lakini wameshindwa kuzifuata Halmashauri na TARI kihinga kutokana na umbali na gharama za usafirishaji.
‘Tunakushukuru sana Mkurugenzi Mkuu wa TARI kwa ujio wako hapa kijijini kwetu. Kwa kweli uhamasishaji ni mdogo sana. Wengi bado tunatumia mbegu za michikichi ya zamani, Viongozi wetu hawajawahi kufanya mkutano kama huu wa kuhamaisha zao hili,” alisema Abiudi Obeid kutoka kijiji cha Kandaga.
Aidha wakulima wengine wamedai kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maafisa ugani. Wakitolea mfano, wakulima wa kata ya itebula walidai kuwa katika tarafa yote ya Ngaruka kuna afisa ugani mmoja tu ambae hatoshi kutoa elimu ya Mchikichi kwa tarafa nzima. Mwenyekiti wa kikundi cha watendakazi cha Itebula Mwalimu mstaafu Goodluck Mzikayi aliiomba serikali kuhakikisha wananchi wanaletewa maafisa ugani katika vijiji vyao.
Aidha vijana walidai kuwa kikwazo chao kikubwa kinachowafanya wasilimezao hilo hawana ardh kubwa ya kuendesha kilimo hichoi na kwamba ardhi kubwa inamilikiwa na wazee ambao wameiacha na kuwa mapori, alisema Furaha Tofiki.
Wanakijiji hao waliomba Serikali iwapatie mikopo na mashine za kuchakata bidhaa za Michikichi ili wengi waweze kuingia katika Kilimo hicho huku wengine wakiomba uwepo wa masoko kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.
Katika majibu yake kwa wananchi Mkurugenzi Mkuu wa TARI amewahakikishia wananchi hao kuwa mbegu bora aina ya tenera zipo kwa wingi.
‘ TARI tutaanzisha vitalu vya michikichi katika vijiji hivi ili wale wasio na uwezo wa kufuata mbegu wilayani na kule TARI kihinga wapate hapa hapa" alisema Daktari Mkamilo.
Aidha, aliwaahidi wananchi kuendelea kutoa elimu kwa kuwa hilo ni jukumu la TARI na Halmashauri za Wilaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza Zainab Mbunda na Mkuu wa Wilaya hiyo Hanali Msabaha walisema Wilaya imejipanga kuendeleza zao hilo kwa kuanzisha vitalu zaidi na kwamba wananchi wanaohitaji watapata mbegu hizo.
Wilaya ya Uvinza Ina jumla ya vitalu 33 ambavyo vinamilikiwa na makundi mbalimbali ya wakulima, Taasisi za dini, Shule za msingi na sekondari ambapo mahitaji ya mbegu zilizootoshwa zilifikia zaidi ya 1,500,000.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo akizungumza na Wakazi wa Kigoma juu ya umuhimu wa kulima zao la mchikichi kwa kutumia mbegu bora
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...