MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha sekta ya Afya katika Mkoa huo ambapo Vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kwa asilimia 20 ndani ya mwaka mmoja.

Ditopile ameyasema hayo wakati akizungumzia mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ambapo ameeleza kuwa Mkoa wa Dodoma pekee ndani ya kipindi cha mwaka mmoja Vituo vya kutolea huduma vimeongezeka na kufikia 446 sawa na asilimia 20.

"Ujenzi wa Hospitali za Wilaya unaendelea katika Halmashauri nne ambazo hazikua na Hospitali. Zaidi ya Sh Bilioni 6.9 zimeshatolewa Kwa Halmashauri za Chemba, Bahi, Chamwino na Kondoa ambazo hazikua na Hospitali wakati Kongwa wamepatiwa Sh Bilioni 1.6 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa Hospitali yao.

Tunamshukuru Rais Samia kwa namna pia alivyotukumbuka Wanawake wa Mkoa wa Dodoma katika uongozi, tumeona amemteue Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara huku pia akimteua Dk Fatma Mganga kuwa RAS wetu, hii ni Imani kubwa ambayo Rais ameonesha kwetu," Amesema Ditopile.

Mbunge Ditopile pia amempongeza Rais Samia kwa azma yake nzuri ya kuwatambua wamachinga Nchini ambapo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa kuendesha zoezi la kuwapanga wafanyabiashara hao katika maeneo yaliyopangwa.

" Rais Samia ameonesha jinsi gani anathamini wamachinga, Katika Jiji letu la Dodoma tunamshukuru kwa kutupatia Sh Bilioni 7.5 ambazo zitasaidia kukamilisha ujenzi wa Soko hilo na kila mwaka Serikali kupitia Jiji la Dodoma itakusanya Sh Bilioni 1.1 kupitia wafanyabiashara wa soko hili la machinga," Amesema Ditopile.

Akizungumzia sekta ya Elimu, Ditopile amesema Mkoa wa Dodoma nao umenufaika na mgao wa fedha za UVIKO-19 ambazo Rais Samia alizipata.

"Kupitia fedha za UVIKO-19 Dodoma tumepata jumla ya Sh Bilioni 12 ambapo madarasa 601 yamejengwa bila kuchangisha wananchi jambo ambalo halijawahi kutokea. Wanafunzi wetu wameingia Shule Januari mwaka huu bila Mzazi yeyote kuchangishwa ujenzi wa madarasa au ununuzi wa madawati.

Rais Samia hakuishia hapo ametupatia fedha Sh Bilioni 3.5 kwa ajili ya kujenga Madarasa 175 ya Shule Shikizi katika Mkoa wetu, lakini pia ametupatia Sh Milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa Mabweni katika Shule Maalum," Amesema Ditopile.

Mbunge huyo amewaomba wananchi wa Mkoa wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuendelea kumuombea Rais Samia ili azidi kutekeleza majukumu yake ya kuijenga Tanzania na kuwaletea Maendeleo wananchi wake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...