JUMLA ya wanawake 35 wamepewa tuzo ya umahiri kwenye biashara zilizotolewa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) .
Walikabidhiwa tuzo hizo jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, kwenye hafla iliyofanyika ukumbi wa Mlimani City.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dk. Gwajima alisema wanawake wanaweza kufanya mambo makubwa kwenye jamii na aliwataka wanaume kuwapa nafasi ya kwenda kufanyabiashara.
Alikipongeza chama cha wafanyabiashara wanawake (TWCC), kwa kuandaa tuzo hizo na aliwataka mwakani waongeze idadi ya tuzo hizo hata zifikia 150 ili kuendelea kuwapa moyo wanawake kuendelea kufanya vizuri kwenye biashara.
“Hizi ni tuzo muhimu sana kwa wanawake na nawashukuru wafadhili wa tuzo hizi na nawapa changamoto TWCC ongezeni idadi ya tuzo hizi hata zifikie 100 na hii itasaidia kuwapa moyo wanawake kwamba wanaweza kufanya mambo makubwa,” alisema
Alisema ni muhimu wanawake wakafanyabiashara na kuinua kipato cha familia badala ya kumwachia mzigo baba peke yake kwani hali hiyo inaweza kumsababishia msongo wa mawazo na kusababisha apate maradhi au kifo cha mapema.
Alisema kuna fursa nyingi za mikopo ya riba nafuu ambayo imekuwa ikitangazwa na serikali na taasisi nyingi za fedha hivyo ni wajibu wa wanawake kuzifuatilia na kuzichangamkia kila zinapotokea.
Mtendaji Mkuu wa (TWCC), Mwajuma Hamza alisema kulikuwa na majaji watano Kutoka taasisi mbalimbali ambao walichuja majina ya wafanyabiashara hao kwenye sekta 16 zilizokuwa zikishindaniwa.
Alisema tuzo hizo zilitolewa baada ya maonyesho ya wiki moja ya wajasiriamali wanawake wajasiriamali yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Alisema baadhi ya vigezo walivyoangalia ni uendelevu wa biashara husika ili wasimpe mtu tuzo na biashara yake ikafa na waliangalia pia mikakati ya biashara husika.
Alisema kigezo kingine ni biashara iwe imerasimishwa na iwe na nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na umiliki wa biashara husika.
Mbali na GIZ wafadhili wengine ni Trade Mark East Africa, CRDB, NMB, NBC,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...