Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ripoti hiyo (kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage na kushoto ni Mwenyekiti wa bodi HakiElimu Japhet Makongo.
*Serikali yawapongeza kwa ushiriki wao katika kukuza na kuendeleza sekta ya Elimu
SERIKALI imepokea ripoti ya Utafiti unaohusu Sera na Utekelezaji wa Elimu ya Afya ya Uzazi katika Shule za Msingi na Sekondari Tanzania Bara uliofanywa na watafiti wabobezi kutoka shirika la HakiElimu na kueleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau hao katika kuhakikisha mtoto wa kitanzania anapata elimu bora.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka amesema wakiwa wasiamamizi wa sera na mikakati wanahitaji tafiti za namna hiyo zinazosaidia kuinua zaidi sekta Elimu.
''Wadau wa HakiElimu wamekuwa mstari wa mbele katika kusaidia ukuaji na uendelezaji wa sekta hii muhimu na kupitia utafiti huu uliofanywa na wataalam wabobezi utatusaidia kuona mbali zaidi na kuboresha zaidi.'' Amesema.
Kuhusiana na somo la Afya ya Uzazi mashuleni Sedoyeka amesema ni suala muhimu kwa kundi la vijana balehe.
''Somo hili ni muhimu sana kwa vijana wa kundi la balehe hasa kwa vijana wakike ambapo kumekuwa na changamoto kubwa pindi wanapoingia katika siku zao za hedhi wakiwa darasani na namna ya ufuatiliaji wao wa masomo...kukosekana kwa elimu hii kunaathiri uelewa na ufaulu wao kutokana na baadhi wa yao kushindwa kuhudhuria masomo yao wanapokuwa hedhi.'' Amesema.
Prof. Sedoyeka amesema, tafiti zinaeleza kuwa wanafunzi wanapopata elimu ya Afya ya Uzazi pekee wanaongeza siku za kukaa darasani jambo ambalo Wizara inalipa umuhimu katika kuboresha zaidi kwa kushirikiana na wadau.
''Suala la wototo wetu kuingia katika mahusiano huangaliwa zaidi mara baada ya matokeo kutokea kama kupata ujauzito na magonjwa.....kupata elimu ya kutochanganya elimu na mapenzi itawaweka huru na tafiti inaonesha elimu hii inatolewa tunachoangalia sasa ni kuboresha katika utolewaji wake kiundani na kwa umri upi.'' Amesema.
Akizungumzia kuhusu utafiti huo Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt. John Kalage amesema HakiElimu inatambua mchango wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na mchakato wa kupitia na kuboresha Sera na Mitaala zinaashiria nia thabiti inayolenga kufanikisha azma ya ya kuwa na Elimu bora kwa wote.
''Lengo ya utafiiti huu lililenga kuchunguzakuchunguza zingatiaji wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki katika mfumo wa Elimu ya msingi na sekondari Tanzania Bara kwa kuangalia uwepo wa sera, sheria na miongozo mahususi ya Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki za Jinsia, maudhui ya mtaala wa Elimu, ufundishaji na mchango wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki za Jinsia katika kuboresha upatikanaji wa Elimu kwa wasichana.'' Amesema.
Dkt. Kalage amesema jitihada hizo zilizofanywa na HakiElimu na kutoa taarifa hiyo ya utafiti kuhusu 'Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki' katika shule za msingi na sekondari Tanzania Bara ni jitihada za kutatua changamoto katika sekta hiyo muhimu na kuhakikisha mtoto wa kitanzania anapata elimu bora.
Amesema miongoni mwa changamoto zinazohitaji ushirikiano wa pamoja ili kuzitatua na kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu;
''Takwimu za elimu za kitaifa za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, National Basic Education Statistics in Tanzania (BEST,) ZA mwaka 2021 zinaonesha jumla ya wanafunzi 198,620 (wakiwemo wakiume 115,519 na wakike 83,801) wa shule za msingi na 113,484 (wakiume 57,544 na wakike 55,940) wa shule za sekondari waliacha masomo yao kwa mwaka 2020 kwa sababu mbalimbali ikiwemo vifo, makosa ya kinidhamu, mimba na utoro.......Kwa changamoto ya mdondoko kutokana na ujauzito mwaka 2020 watoto wakike 989 wa shule za msingi waliacha shule kwa kupata mimba na 4543 wa Sekondari waliacha shule kutokana na ujauzito kwa mwaka huo.'' Amesema Kalage.
Amesema utafiti huo uliofanywa kwa Mikoa ya Dodoma, Mara, Arusha, Rukwa na Lindi umezingatia kanuni za utafiti na changamoto kadhaa zilijitokeza ikiwemo kiwango kidogo cha asilimia 15 ya wanafunzi walioridhika na utoshelevu wa maudhui ya Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki pamoja na asilimia 93.3 ya walimu waliohojiwa walisema maudhui ya Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki hayajitoshelezi na asilimia 33.3 kusema maudhui hayo hayafai kufundishwa kwa wanafunzi.
''Changamoto tulizokutana nazo ni pamoja na mitazamo hasi ya juu ya elimu hii wengi wanahofia vijana kujihusisha na tabia mbaya, walimu kuona aibu kwa baadhi ya mada, walimu kuwatenganisha wavulana na wasichana kwenye madarasa tofauti pamoja na matumizi ya lugha ya kiingereza katika ufundishaji hizi ni baadhi ya changamoto nina imani matokeo ya utafiti huu yatatumika katika kuboresha zaidi na kuleta matokeo chanya katika jamii yetu tukianza na watoto kwani tuna methali yetu inasema 'Samaki Mkunje Angali Mbichi'.'' Amesema.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau wa elimu, wabunge, walimu, wanafunzi, wadau wa maendeleo na asasi za kiraia.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka akimkabidhi nakala ya ripoti ya utafiti kuhusu Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki kwa shule za Msingi na Sekondari kwa mwakilishi wa Asasi ya Kiraia ya Karibu Tanzania (KTO,) Utafiti huo umefanywa na shirika la Haki Elimu umependeza Wizara husika na wadau wengine kushirikiana katika kuingiza Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki za Jinsia katika mfumo na taratibu za sekta ya Elimu.
Baadhi ya wanafunzi wakipokea nakala za ripoti ya utafiti kuhusu Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki kwa shule za Msingi na Sekondari.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti kuhusu Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki kwa shule za Msingi na Sekondari Tanzania Bara na kueleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau hao katika kuboresha sekta ya elimu, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalage akizungumza wakati wa uzinduzi huo na kueleza kuwa mapitio na kuboresha sera na mitaala zinaashiria nia thabiti ya kufanikisha azma ya kuwa na Elimu bora kwa wote, Leo jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakifuatilia uzinduzi huo.
Mawasilisho yakiendelea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...