Na Said Mwishehe, Michuzi TV

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema kuwa litaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni mkakati wa kuendelea kupunguza ajali huku likielezea kwa sasa matukio ya ajali hizo yamepungua kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza baada ya kushuhudia wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio jijini Dar es Salaam wakitoa hukumu mbalimbali kwa madereva ambao wamevunja sheria za Usalama Barabarani kupitia 'Mahakama ya Watoto' Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa amesema elimu inayoendelea kutolewa inasaida kupungua matukio ya ajali barabarani,hivyo wataendelea kuitoa mara kwa mara.

Kamanda Mutafungwa ameongeza katika kutoa elimu hiyo ya usalama barabarani kwa ajili ya kuwajengea uelewa wa kuepuka ajali kwa kufuata sheria za Usalama barabarani Jeshi hilo limekuwa likishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa Shirika la Amend ambao wamekuja na ubunifu wa kuanzisha Makamma ya Watoto ambayo lengo lake ni kuendelea kutoa elimu hiyo ili kufika kwa jamii kubwa ya Watanzania.

"Ninachoweza kukieleza, ni kwamba matukio ya ajali za barabarani yamepungua kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na huko nyuma.Kuna sababu nyingi ambazo zimesababisha kupungua kwa ajali za barabarani lakini miongoni mwa sababu ni elimu inayoendelea kutolewa sambamba na kuwahamiza madereva wa magari,bajaji na bodaboda kuheshimu sheria.

Pia elimu hii inatolewa kwa watembea kwa migumuu na njia mbalimbali zinatumika kufikisha elimu hiyo,"amesema Kamanda Mutafungwa na kuongeza kwamba Mahakama ya Watoto imekuwa njia nyingine ya kuifikisha elimu hiyo na matarajio yao ni kuona inaendelea katika maeneo mengi zaidi kwani kwa mujibu wa Shirika la Amend ambao ndio wameratibu programu ya mahakama hiyo wanaeleza inafanyika katika shule nane za msingi ambazo ni za Serikali.

Akiizungumzia zaidi programu ya Mahakama ya Watoto iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia wanafunzi wa Shule za msingi,Kamanda Mutafungwa amesema itasaidia kufika elimu hiyo kwa wananchi wengi zaidi na kwa haraka zaidi.

"Kupitia Mahakama ya Watoto tumeona Watoto wetu( wanafunzi) ambavyo wanafahamu sheria za usalama barabarani na hata wakati wanaoendesha kesi dhidi ya madereva waliovunja sheria mbalimbali za barabarani unaona wanavyosikiliza na kutoa hukumu.

"Madereva wanakiri kuvunja sheria mbele ya wanafunzi, wanatoa ahadi ya kutorudia makosa na watakuwa mabalozi kwa kuwaambia madereva wengine waheshimu sheria,hakika Mahakama hii inafikisha elimu katika Mazingira rafiki na sisi Kikosi cha usalama barabarani tunaifurahia na kuwapongeza Amend kwa ubunifu huu,"amesema Kamanda Mutafungwa.

Awali Mkurugenzi wa Shirika la Amend Simon Kalolo amesema wao kama wadau wa usalama barabarani wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha usalama barabarani kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani.

"Katika kuendelea kutoa elimu tumeamua kuja na programu ya Mahakama ya Watoto na lengo kuhakikisha tunashirikiana na wenzetu Polisi kufikisha elimu hii.Programu ya Mahakama ya Watoto imezaa matunda na kwetu tunaona faraja namna wanafunzi walivyokuwa na uelewa mkubwa wa kusikiliza kesi za madereva wavunjifu wa sheria na hukumu zinavyotolewa.Madereva wanaulizwa maswali ya msingi na wanafunzi hawa,"amesema Kalolo.

Kwa upande wa wanafunzi walioko kwenye programu ya kutoa elimu ya Usalama Barabarani kupitia Mahakama ya Watoto wamesema wanalishukuru Jeshi la Polisi na Shirika la Amend kwa kuandaa programu hiyo na kuombe iwapo kuna uwezekano isambae kwenye shule zote nchini wakiamini itakwenda kusaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo nyingi zinazotokana na watumiaji wa barabara kutofuatwa sheria .

Kamanda wa Jeshi la Polisi ,Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa ( wa kwanza kushoto waliokaa) akiwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio jijini Dar es Salaam wakati wanafunzi hao wakisikiliza kesi za madereva waliovunja sheria za Usalama Barabarani kupitia programu ya Makakama ya Watoto yenye lengo la kutoa elimu ya usalama barabarani.Aliyekaa mbele ya Kamanda Mutafungwa na wanafunzi hao ni mmoja wa madereva ambaye alikamatwa na askari wa Usalama Barabarani kwa kosa la kutosimama kwenye kivuko cha waenda kwa miguu kilichopo eneo la shule hiyo juzi.

Mmoja ya madereva akisoma kiapo cha ahadi ya kutorudia kuvunja sheria za Usalama Barabarani baada ya kutakiwa kufanya hivyo wakati wa uendeshaji na kesi ya madereva waliokamatwa kwa kuvunja Sheria za Usalama Barabarani katika Mahakama ya Watoto.Mahakama hiyo imeendeshwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utoaji elimu kwa wananchi kuzingatia sheria ili kupunguza ajali .Wa kwanza kushoto aliyekaa na wanafunzi hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa ambaye alikuwa akifuatilia namna wanafunzi hao wanaovyosikiliza kesi na kutoa hukumu kwa madereva

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo( katikati) na Meneja Programu wa Shirika hilo Neema Swai( kushoto) baada ya kumalizika kwa Mahakama ya Watoto iliyokuwa inasikiliza kesi ya madereva waliovunja sheria za Usalama Barabarani.Mahakama hiyo imeendeshwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa Mahakama ya Watoto iliyokuwa ikiendshwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam iliyokuwa na lengo la kutoa elimu ya Usalama Barabarani kwa wananchi ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa na jeshi hilo kifikisha elimu hiyo kwa wananchi

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam ambao wapo kwenye Programu ya Makakama ya Watoto wakiwa makini kuangalia mmoja wa madereva akiandika kiapo cha kutorudia kuvunja Sheria ya Usalama Barabarani baada ya kukiri mbele ya Wanafunzi hao kuvunja sheria hizo baada ya kutosimama kwenye kivuko cha waenda kwa miguu kilichopo nje ya shule hiyo .Wa kwanza kushoto ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa akifuatilia uendeshaji kesi uliokuwa unafanywa na wanafunzi hao wakati Makakama ya Watoto ikiendelea

Mmoja ya madereva walikamatwa kwa kosa la kuvunja sheria ya Usalama Barabarani akisoma kiapo cha kutorudia tena kuvunja sheria hizo mbele ya Wanafunzi waliokuwa wanaoendesha Mahakama ya Watoto katika Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam.Wa kwanza kushoto aliyekaa kwa wanafunzi hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa akisikiliza mwenendo wa kesi katika Mahakama hiyo

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam ambao waliokuwa wakiendesha kesi katika Mahakama ya Watoto kwa kusikiliza na kutoa hukumu kwa madereva waliovunja sheria za Usalama Barabarani katika eneo la shule yao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na walimu wa Shule ya Msingi Olimpio mkoani Dar es Salaam , Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo ( wa pili kushoto),maofisa wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na wanafunzi wa Shule hiyo.


Kamanda wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Wilbroad Mutafungwa (katikati) akiwa na maofisa wa Jeshi hilo pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo ( wa tatu Kushoto) na Meneja Programu Neema Swai(wakwanza kushoto).




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...