Na Said Mwishehe,Michuzi TV
BOHARI ya Dawa( MSD) imesema ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa na vifaa tiba ikiwemo mipira ya mikono(Gloves) kilichopo Idofi -Makambako mkoani Njombe ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90 na uzalishaji wa majaribio tayari umeshaanza na kuonesha mafanikio makubwa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Erick Mapunda leo Machi 7,2022 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa( MSD) Meja Jenerali Gabriel Saul Mhidze (Dkt)
wakati ziara ya waandishi wa habari walipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya MSD kuelezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.
Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo wa ujenzi wa Viwanda vya dawa na vifaa tiba uliopo Idofi -Makambako amesema ulianza rasmi Oktoba 4,2020 kwa lengo la kuanzisha kiwanda cha mipira ya mikono( gloves) na hiyo ilitokana na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo wakati huo,kutokana na anga nyingi Duniani ambazo MSD inategemea kuagiza bidhaa hiyo zilikuwa zimefungwa.
"Ukubwa wa eneo la mradi ni ekari 38 ambazo zimetolewa na wanakijiji cha Idofi waliokuwa wanamiliki eneo hilo kwa ujumla ya fidia Sh.59,035,168.Ujenzi wa kiwanda Cha kuzalisha gloves ulianza rasmi Oktoba 2020 ukijumuisha jengo la kiwanda lenye ukubwa wa mita za mraba 3120,"ameeleza Mapunda na kufafanua ujenzi wa kiwanda hicho umekamilika kwa asilimia 90.
Akielezea zaidi kuhusu kiwanda hicho,Mapunda amesema kwa Sasa ufungaji wa eneo la usafi,vyoo vya ndani ya kiwanda pamoja na maeneo ya kubadilisha nguo unaendelea huku akifafanua ghala la kuhifadhi malighafi linaloendelea kujengwa lina ukubwa wa mita za mraba 1000 ambapo ujenzi wa ghala hilo ulianza rasmi Septemba 10,2021 na unatarajiwa kukamilika katika robo ya tatu ya mwaka 2022.
Kuhusu ujenzi wa majengo matatu ya Viwanda vya Tablets,Capsules na Syrup , Mapunda amesema ujenzi wa majengo ya viwanda vya dawa za vidonge,dawa za maji na vidonge vya rangi mbili unahusisha ujenzi wa majengo matatu yanayofanana kwa ukubwa wenye mita za mraba 900( urefu mita 50.8,upana mita 17.7 na kimo cha mita 7 kwa kila jengo.
"Kwa sasa ujenzi wa majengo yote matatu umekamilika kwa asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika katika robo ya tatu ya mwaka 2022.Upokeaji wa mitambo ya kuzalisha syrup( vimiminika,rangi mbili(capsule) na dawa umekamilika kwa asilimia 100,"amesema.
Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha Krimu , Mapunda amesema MSD imenunua mitambo ya kutengeneza na kufungasha dawa rojorojo ambayo imekwishawasili nchini katika eneo la mradi MSD keko Makao Makuu.Manunuzi ya mitambo na malighafi ya ujenzi wa kiwanda yamekamilika kwa asilimia 60." Uzalishaji wa bidhaa za afya utaanza kwa kila kiwanda pindi ujenzi wake unapokamilika."
Aidha Mapunda amesema faida za miradi ya dawa na vifaa tiba , amesema itaondoa changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini ambapo kwa sasa asilimia 90 zinatoka nje ya nchi . Dawa na vifaa tiba vitakavyozalishwa vitakidhi mahitaji ya wananchi na watapata bidhaa A afya kwa gharama nafuu.
Pia Serikali itaokoa fedha za uagizaji wa dawa na vifaa tiba vitakavyozalishwa Idofi na kwamba jumla ya Sh.bilioni 33 ambazo zitaokolewa kwa mwaka kwa dawa zitakazozalishwa kwenye kiwanda Cha Idofi na kuongeza faida nyingine miradi itazalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 200.
Kuhusu aina ya dawa na vifaa tiba vinazotarajiwa kuzalishwa kwenye viwanda vinavyojengwa eneo la Idofi ,Mapunda ameeleza kiwanda cha vifaa tiba kitazalisha Sugical& examination gloves ambapo kiwanda hicho kitazalisha gloves 20,000 kwa saa ambazo ni sawa na jozi 10,000 kwa saa.
Amesema viwanda vya vidonge na rangi mbili ambazo zitazalishwa 330,000 kwa saa na vidonge vya kawaida (capsules) ambavyo vitazalishwa 425,000 kwa saa .Dawa hizo ni Paracetamol,Amoxycillin,Arythomycin , Apiclox.
Wakati kiwanda cha dawa za maji( syrup) kitazalisha jumla ya 180 kwa saa .Dawa zifuatazo ni pamoja na Cough Syrup,Paracetamol syrup ,Cotrimozazole syrup na metronidazole syrup.
Akizungumzia sababu za kujengwa kwa kiwanda Cha Idofi, Mapunda amesema imetokana na hali ya hewa ya baridi ambayo huhitajika kuzalisha gloves , miundombinu ya usafiri wa barabara na reli inayopita karibu na mradi huo ambayo inatarajiwa kurahisisha Usafirishaji wa bidhaa ,gharama nafuu ya upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hivyo.
Kuhusu gharama za mradi amesema hadi kufikia Desemba 2021 gharama za miradi yote minne kwa maana ya ununuzi wa mitambo na ujenzi wa majengo na miundombinu mingine ya Viwanda ni jumla ya Sh.bilioni 17 .7 ambapo Sh. 15,562,566,917.50 zilitolewa na Hazina na sehemu inayobakia inatokana na mapato ya ndani ya MSD.
Akizungumzia changamoto amesema ni upatikanaji wa malighafi ya utomvu aina ya Latex na kwamba juhudi za kutafuta malighafi hiyo maeneo ya Tanzania Bara zinaendelea ,hata hivyo jitihadi zinaendelea kupatiwa mashamba ya miti aina ya rubber kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ."Mazungumzo yanaendelea kwani upatikanaji wa malighafi hiyo ndani ya nchi utapunguza gharama za kuagiza za kutoka nje ya nchi."
Changamoto nyingine ni kuchelewa kufika watalaam ambapo Mapunda ameeleza kutokana na janga la UVIKO 19 baadhi ya wataalam wa kufunga mitambo kutoka China wakichelewa kuwasili nchini hivyo kuathiri ukamilishaji wa ufungaji wa mitambo.
"Menejimenti ya MSD inatambua mchango kutoka Serikalini kuwezesha ujenzi wa viwanda vya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba unaofanywa na MSD.Tunatoa shukrani zetu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa ujenzi wa viwanda vya uzalishaji unaofanywa na MSD.''
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...