* TANZANIA KUISAIDIA MSUMBIJI KUKOMESHA VITENDO VYA KIGAIDI*
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itandelea kuwa mstari wa mbele kuisaidia nchi ya Msumbiji katika kukabiliana na vitendo ya kigaidi katika nchi hiyo.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Machi 24, 2022) alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa kujadili usalama katika eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika hususan nchini Msumbiji na maeneo ya jirani (Aqaba Process), uliofanyika katika mji wa Aqaba uliopo nchini Jordan.
“Tanzania tutaendelea na ushiriki wetu wa kuisaidia Msumbiji kwa kiwango wanachohitaji, lengo ni kuhakikisha tunauondoa kabisa ugaidi nchini humo, tunapunguza hatari ya magaidi kuingia nchini Tanzania, pamoja na kuwasaidia kwa hali na mali wananchi wake kuendelea na shughuli zao”.
Amesema kuwa mkutano huo pia umepokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa Msumbiji na wadau wa Aqaba Process kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano na kuisaidia Msumbiji kukabiliana na changamoto za ugaidi.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Eneo linaloshambuliwa ni Kaskazini mwa Msumbiji ambalo ni Kusini mwa nchi yetu, hivyo ushiriki wetu umekuwa ni muhimu sana”.
Mkutano huo ambao umeitishwa na Mfalme Abdullah II wa Jordan, utakuwa wa tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 na huwakutanisha viongozi wakuu wa nchi za ukanda wa Mashariki ya Afrika kwa lengo la kujadili changamoto za ugaidi na namna ya kuudhibiti.
Baadhi ya viongozi walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mfalme Abdulla II wa Jordan katika mkutano wa kujadili usalama kwenye eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika hususan nchini Msumbiji na maeneo jirani uliofanyika Machi 24, 2022 kwenye mji wa Aqaba nchini Jordan. Katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Mbarouk Nassor Mbarouk.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi katika mkutano wa kujadili usalama kwenye eneo la Kusini Mashariki mwa Afrika hususan nchini Msumbiji na maeneo jirani uliofanyika Machi 24, 2022 kwenye mji wa Aqaba nchini Jordan. Katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Mbarouk Nassor Mbarouk.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...