Adeladius Makwega-Mbagala

Siku ya Machi 14, 2022 nilipata wasaa wa kumsoma Baba Askofu Emmaus Mwamakula katika matini iliyokuwa na aya karibu ya 16 juu ya mgogoro baina ya waliokuwa wanafunzi wa Azania na Tambaza kati ya mwaka 1993 na 1994 jijini Dar es Salaam.

Kwa kuwa na mimi nilikuwa miongoni mwa wanafunzi hao wakati huo na nami nainyanyua kalamu yangu kuandika yale ambayo nitajaliwa kuyakumbuka huku mengine nikiwasiliana na wenzangu tuliokuwa nao wakati huo ambapo nitayaandika katika matini mfululizo.

Kabla sijaingia katika mgogoro wenyewe wa siku hiyo naomba msomaji wa matini hii nadhani ni vizuri mno kuzifahamu vizuri shule hizi mbili Azania na Tambaza kihistoria. Tangu enzi zilikuwa ni shule za wavulana tu lakini baadaye Tambaza kidato cha tano na sita waliingizwa wasichana.

Azania walikuwa na urafiki na Jangwani, nashukuru hili hata Baba Askofu Mwamakula amelitaja, Tambaza walikuwa na urafiki na Zanaki. Bahati nzuri ya Azania walikuwa majirani mno na dada zao shule rafiki Jangwani, wakati Tambaza walikuwa mbali kidogo na dada zao rafiki shule ya Zanaki.

Ujirani wa Azania na Jangwani ulisaidia mno wanafunzi wa Azania kutokuwa watundu zaidi kwani mara zote walikuwa wakiwaona wanafunzi wa Jangwani na sketi zao za rangi chungwa ambazo ziliwavutia mno vijana wa Azania hata sie tuliokuwa tukisoma Tambaza wakati huo.

Nakumbuka hata bweni la wanafunzi wa A level wa Jangwani lilikuwa katika viwanja vya Azania wakati huo

Nikirudi nyuma zaidi kuanzia mwaka 1990 shule kadhaa za umma za kutwa za Dar es Salaam zilitakiwa kuwapokea wanafunzi wengi ili kutoa nafasi ya wanafunzi wengi zaidi wa mkoa huu kupata elimu ya sekondari, kwa hiyo wakati huo kukawa na wanafunzi wengi wa kidato cha kwanza na kukawa na makundi mawili yenye mikondo kumi na miwili na kila mkondo ulikuwa na wanafunzi 40 jumla kuu ilikuwani wanafunzi 480 kwa kidato cha kwanza tangu mwaka huo 1990.

Wanafunzi hawa 480 wa Azania na 480 wa Tambaza na shule zingine waliofaulu pamoja wakiwa msingi walisoma pamoja, walipofaulu walitenganishwa tu na shule hizo. Kama ukiwafuatilia tangu wadogo pengine mafundisho ya kipaimara kanisani, kupokea Kipaimara hicho walipokea pamoja, madrasa walisoma pamoja.

Wengine walikuwa ndugu wa damu, kaka alikuwa Tambaza na mdogo mtu alikuwa Azania. Hali hii ilikuwa hivyo hivyo kwa Zanaki , KIusutu , Kibasila , Forodhani na Jangwani.

Swali la kulijibu ilikuwaje hawa wanafunzi walisoma pamoja shule ya msingi, waliokuwa wakisoma pamoja kipaimara na walisoma pamoja madrasa wakaja kuwa maadui hadi wakipigana kwa kutumia mabomu ya petrol kama alivyosimulia Baba Askofu Mwamakula?

Kwa miaka mingi shule ya Tambaza ilikuwa ya wanafunzi watundu, wachangamfu, wapenda utani, wacheshi na vituko vya hapa na pale huku pia wakitazamwa kama magangwe wa mjini. Kwa kuwa walipokuwa waksoma Tambaza hawakuwa jirani na wasichana kama Azania, ndiyo maana vitendo hivyo vya utundu uliovuka mipaka uliongezeka.

Japokuwa walikuwa watundu hivyo walifanya vizuri kitaaluma lakini wapo wanafunzi ambao walivuka mipaka ya tabia hizo mbaya huku walimu wa shule na serikali wakijahidi kuyafanyia kazi.

Japokuwa shule hizi zilipokea wanafunzi wengi kwa upande wake serikali ilijitahidi kuwapatia chai na chakula cha mchana wanafunzi wote lakiai changamoto moja kubwa ilikuwa ni usafiri wa wanafunzi hapo ndipo shida ilipoanza.

Nakumbuka makondakta walikuwa vijana ambao walikuwa wamemaliza darasa la saba wengine kidato cha nne hawa walishindana mno kwenye usafiri na wanafunzi wa Tambaza wakati wakienda shule au kurudi nyumbani.

Wanafunzi wa Tambza wakiwa katika makundi kulingana na wanapotokea mathalani Mkaundi Magomeni, Tandika, Ubungo, Mwananyamala, Kijitonyama, Mwenge, Kawe na hata Mbagala na wakienda shuleni pamoja na kurudi pamoja.

Makondakta walikuwa wakitafuta faida ya biashara zao sasa linapokuja kundi la wanafunzi wa Tambaza wapande wote hiyo ni hasara kwao, hapo ndipo ngumi zilipotokea.

Kutoka na hilo CCM hasa hasa Umoja wa Vijana wa wakati huo ulijaribu kulitatua na kuja na mradi wa mabasi ya wanafunzi ambapo wanafunzi wote tulipewa makadi ya kuchangia mradi huo na mradi huo kuanza. Chini ya UVCCM ya John Guninita na akiwamo Wiliam Lukuvi japokuwa baadaye mradi huu ulikufa. Huku yakitumiwa mabasi ya mashirika ya umma kubeba wanafunzi kama kuokoa jahazi.

Yale mkundi ya kupambana na makondakta yaliwapa nafasi wanafunzi wengi wa Tambaza kujifunza michezo kadhaa ikiwamo kubeba vyuma karate, ngumi nakadhalika hili wawe magangwe wa kweli.

Kwa wale wanaozifahamu siasa za Tanzania wakatihuo wapigania uhuru wengi walikuwa hapa nchini na familia zao. Watoto wao wakisoma katika mifumo ya elimu ya Tanzania wengine walipata elimu hadi ya Chuo Kikuu.

Baadhi yao walisoma Tambaza kwa kidato cha Tano na cha Sita, kwa kuwa walikuwa wapigania uhuru waliambukiza zile mbinu za kivita za awali kama mabomu ya petrol na kutumia mawe kwa wanafunzi wenzao na palipokuwa panatokea vurugu mbalimbali kama ya Azania na Tambaza, Tambaza na JKT Mgulani, Tambaza na Kinondoni Muslimu na ugomvi Tambaza na Makondakta na hata Kuvunjwa kwa ukuta wa shule ya Msingi Muhimbili.

Ujuzi huu ulitumika katika ugomvi binafsi mathalani wa kuwagombania wasichana kama ulivyokuwa huu mgogoro wa Azania na Tambaza hadi kuumizana na kuharibu mali za umma.

Serikali ya wakati huo chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi haikukaa kimya bali walifuatilia mno jambo hilo chini ya Waziri wa Elimu wakati huo Profesa Philimon Sarungi , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Ditopile Mzuzuri na RPC Dar es Salaam Typhone Maji na hata baadaye RPC Mwinyi Dadi Ally.

Naomba kwa leo niishie hapo, matini ijayo nitaendelea zaidi kuusimulia mgogoro mmoja baada ya mwingine hadi shule hii kufungwa na baadaye kuwahamisha wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili pamoja na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu na cha nne.


Nakutakia siku njema

makwadeladius@ gmail.com

0717649257 



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...