Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi wa Halmashauri Ilemela walipofika kukagua mradi wa kupanga na kupima ardhi inayotekelezwa na Halmashauri hiyo jijini Mwanza.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ikiwa katika picha ya pamoja katika eneo la mradi wa kupanga na kupima ardhi unaotekelezwa na Halmashauri ya Ilemela jijini Mwanza.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ikiwa katika picha ya pamoja katika eneo la mradi wa kupanga na kupima ardhi unaotekelezwa na Halmashauri ya Ilemela jijini Mwanza.
……………………………………………….
Na Anthony Ishengoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Ally Makoa amezitaka Halmashauri zote Nchini kuiga juhudi za utekelezaji wa mpango wa program ya kupanga na kupima ardhi inayotekelezwa na Halmashauri ya Ilemela jijini Mwanza.
Halmashauri ya Ilemela inatekeleza mradi huo kufuatia mkopo unaotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuziwezesha Halmashauri nchini kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa lengo la kuongeza thamani, mapato na kuepukana na makazi holela.
Bw. Makoa alisema kamati yake imeona na kujiridhisha kwa kiasi kikubwa na mpango wa program ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi inayotekelezwa na Halmashauri ya Ilemela na kuongeza kuwa kama mpango huu utatekelezwa Nchi nzima kama ilivyofanyika Ilemela itakuwa ni mafanikio makubwa kwa maendeleo ya Taifa.
‘’Kama nchi nzima tutafanikiwa kuwa na mradi kama huu kwa hakika tutakuwa tumeitendea haki serikali ya sasa inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan’’. Aliongeza Bw. Ally Makoa Mwenekiti wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii na Mbunge wa jimbo la Kondoa mjini.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Babati Mkoani Manyara Bi. Asia Halamga akiongea na vyombo vya habari mara baada ya Kamati kutembelea eneo la mradi alisema pamoja na pongezi kwa utekelezaji wa mradi lakini pia mradi huo ni funzo kwa wakurugenzi wa Halmashauri ikiwemo maafisa ardhi kote Nchini.
Bi. Asia aliongeza kuwa, watumishi wa sekta ardhi wanafanya kazi nzuri kwa kuwashirikisha wananchi aliowaeleza kuwa wameonesha uelewa huku akiwataja wananchi wa Singida ambao walitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa kamati hiyo kuhusu matumizi bora ya ardhi baada ya kushiriki zoezi la upimaji.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula akiongea na Kamati hiyo katika eneo la Mradi la Halmashauri ya Manispaa ya Iemela alisema watumishi wa umma wakiwemo walimu na wauguzi ambao waliojiunga katika makundi tayari wamepatiwa viwanja vilivyopimwa kwa bei ndogo na kuongeza kuwa mwitikio wa watumishi hao tayari umeipatia mapato makubwa Hamashauri ya Ilemela.
Dkt. Mabula alisema, watumishi ambao walichelewa kujiunga na mpango huo hawatoafaidika na bei ya awali kwa kuwa thamani ya ardhi inapanda tofauti na awali ambapo walimu walinufaika kwa kupata kiwanja kwa kiasi cha M.1.6 na kuweka wazi kuwa wale watakao jiunga sasa viwanja hivyo vinaweza kufikia zaidi ya Milioni mbili.
Kwa mujibu wa Dkt.Mabula, makundi ya watumishi yaliyoanza kuwa ni walimu takribani 500 waliochanganyikana na wauguzi ambao tayari wamepatiwa hati pamoja na vibali vya ujenzi kwa gharama hiyo hiyo na sasa wanafikilia kuyashawishi makundi ya bodaboda kujiunga na mpango huo.
Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii iko katika ziara ya kikazi kutembelea program mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na tayari imefanya ziara kama hiyo katika Mkoa wa Singida ilipotembelea na kukagua mradi wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vya Ntondo na Nkwea ambavyo pia vinapitiwa na mradi wa bomba la mafuta.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...