Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika mkutano wa pembeni kwa njia ya mtandao katika Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania inaendelea kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi, kushiriki kwenye mipango ya matumizi ya ardhi iliyopo vijijini na utoaji wa maaamuzi kwenye changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo wakati akishiriki Mkutano wa pembeni ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea Jiji la New York  Marekani.

Dkt. Gwajima amesema,  Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mwanamke anapata fursa ya kumiliki ardhi hasa kwa wanawake wanaoishi vijijini kwani kumekuwa na changamoto katika kumiliki na kushirikishwa ngazi za  maamuzi ya matumizi ya ardhi hasa upande wa kilimo.

"Tumeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha Mwanamke na Mtoto wa Kike wanawezeshwa kumiliki ardhi na kushirikishwa kuamua matumizi bora ya ardhi na kunufaika nayo" alisema Waziri Dkt. Gwajima

Waziri Dkt. Gwajima aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amon Mpanju sambamba na baadhi ya Wataalam amesema, Mkutano wa Hali ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2022 unaongozwa na kauli mbiu ya "Kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na watoto wa kike kwa kupitia programu na sera yenye mtazamo wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira pamoja na upunguzaji wa athari za majanga"

Wakishiriki Mkutano huo kwa njia ya Masafa wakiwa jijini Dodoma wataalam  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Wadau   wamesema msukumo ajenda iliyojadiliwa katika mkutano huo ni muhimu kwa Mazingira ya sasa kwa Nchi zinazoendelea kwani Makundi ya Wanawake ndio wamekuwa wahanga.

Akizungumza kando ya Mkutano huo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Idara ya Maendeleo ya Jinsia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Rennie Gondwe amesema lengo la Mkutano huo wa pembeni ndani ya Mkutano wa 66 wa hali ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii na kuwa na usawa na haki katika kumiliki na kutumia ardhi na kutoa maamuzi.

Rennie ameongeza kuwa, Wizara kwa kushirikiana na wadau inatekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wenye maeneo manane ikiwemo eneo la Mila na Desturi ambapo unasaidia pia kutoa hamasa kwa jamii na wadau kutoa elimu ya kumuwezesha Mtoto wa kike na Mwanamke kumiliki na kunufaika na ardhi.

Akichangia kwenye Mkutano huo Mkurugenzi wa Landesa Tanzania Dkt. Monica Mhoja, amesema Shirika lake linashirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha mwanamke haachwi nyuma kunapo umiliki wa ardhi na kupata manufaa  hasa wakati wa uzalishaji na matumizi bora ya ardhi.

Ameongeza kuwa lengo la Shirika hilo ni kuangalia ni kwa namna gani makundi hayo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashirikishwa kwenye mpango wa matumizi ya ardhi hususan ni ngazi ya kaya ili ardhi hiyo iweze kuwanufaisha dhidi ya ustawi wao.

Afisa kutoka Shirika la Landesa Tanzania Khadija Mrisho akichangia katika mkutano wa pembeni kwa njia ya mtandao jijini Dodoma katika Mkutano wa 66 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.
picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...