Na Mwandishi Maalum,Dodoma
Kasi ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa inayoikabili Tanzania na Dunia kwa ujumla inawataka Mawakili wa Serikali na hususani vijana, kuwa tayari kwa kujiendeleza , kujijengea uwezo na umahili katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na kasi hiyo.
Hayo yameelezwa leo ( Jumatatu) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mawakili wa Serikali Vijana takribani 27 kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Dodoma.
AG Feleshi amewaambia Mawakili hao wa Serikali kwamba, ni kwa kujiendeleza na kujiongezea maarifa ndipo watakapoweza kuishauri vema na kwa weledi Serikali na kuedesha mashauri na mashtaka kwa ubora na viwango vya hali ya juu kama Mawakili wa Serikali.
“kwa muda mrefu nimekuwa nikitamani sana kukutana nanyi Mawakili wa Serikali Vijana, na leo imewezekana. Na kubwa ambalo nimependa tubadilishane mawazo ni hili la kujengeana uwezo na maarifa katika sehemu zetu za kazi ili kupitia maarifa hayo muweze kutekeleza majukumu yenu na katika viwango vinavyokubalika” akasema AG Feleshi
Amebainisha kwamba yeye binafsi ni muumini mzuri sana wa dhana ya kujiendeleza na kujiengea maarifa na umahili mahali pa kazi. “Nimelisimamia hili katika maeneo mbalimbali niliyofanya kazi baada ya kuona changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu nikiwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali na pia nikiwa Jaji kiongozi kwa sababu, niliona haja na umuhimu wa suala hilo na nimeona matokeo chanya ya dhana hiyo”.
Katika mazungumzo hayo na ambayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Mtumba, Dodoma . AG Feleshi amesema uwezeshwaji wa Mawakili wa Serikali waliopo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mataifa ya Mashtaka kunaweza kufanyika kwa kuweka utaratibu mzuri wa Mawakili Waandamizi wenye uzoefu na waliobobea kuwafundisha na kuwaelekeza Mawakili wa Serikali vijana ili nao waweze kuboresha utendaji wao wa kazi.
“Tutambue wazi kwamba, dunia inabadilika kwa kasi sana, nasi lazima tuenende na kasi hiyo, nitawapa mfano mdogo, vita vinayoendelea hivi sasa kati ya Urusi na Ukraini italeta changamoto nyingi na kubwa, mnasoma huko Ulaya wanavyojadiliana kuangalia namna na hatua za kukabiliana na changamoto zitakazotokana na vita hiyo zikiwamo za masuala ya gesi na mafuta. Kwa hiyo tunaweza kujikuta tunapokea wawekezaji wengi katika maeneo hayo je kama mawakili wa Serikali tunajipangaje” akaeleza AG Feleshi.
Akawataka Mawakili hao wa Serikali kutambua kwamba leo wao ni vijana lakini kesho watakuwa viongozi na huwezi kuwa kiongozi pasipo kuwa na nia, hamu, utashi na uthubutu wa kujiendeleza na kujijengea maarifa. Nyinyi mmesoma katika mazingira mazuri na bora kuliko sisi wa huko zamani, rai yangu kwenu zitumieni fursa hizi vizuri”.
Amebainisha kuwa ni lazima na muhimu kwa wakili wa serikali kuwa na ujuzi na maarifa mtambuka na kuweza kutekeleza majukumu mbalimbali kwa wakati mmoja.
“Usiridhike kwamba wewe ni mwendesha mashtaka basi ukaishia hapo, au wewe ni Muandishi wa Sheria ukaridhika hivyo au wewe ni Mpekuzi wa Mikataba ukaridhika na hali hiyo. Kama ni mwendesha mashtaka basi uwena uelewa pia wa kuedesha kesi za madai, ujue pia kuandika sheria, ujue pia kupekua mikataba, na hivyo hivyo kwa muandishi wa sheria, ama mpekuzi wa mikataba, uwe tayari kufanya kazi sehemu au katika taasisi yoyote”
Akitilia mkazo juu ya umuhimu wa Mawakili wa Serikali kujiendelea na kujengea uwezao na umahili sehemu za kazi. Mwanasheria Mkuu Feleshi hata muelewa wakili yoyote wa serikali wakiwamo viongozi watakaofanyia mzaha jambo hilo na kwamba watakuwa kama kama wahujumu wa maendeleo yao binafsi ya na Taifa.
Vile vile amewahimiza Mawakili wote wa Serikali, kujiamini, kujithamini na kujipambanua kwa sababu nafasi yao kama Mawakili wa Serikali ni kubwa na ya heshima sana.
Kwa upande wao Mawakili hao wa serikali pamoja na kumshukuru Mhe. Mwanasheria Mkuu kwa kukutana nao na kubadilishana mawazo wameahidi kuzingatia ushauri wake na pia wameomba kuandaliwa utaratibu wa namna ya kubadilishana uzoefu ikimo namna ya kwenda mahakamani kuendesha.
“Mhe. Tunakushuru kwa kukutana nasi, tutayazingatia haya na tunaomba utaratibu uaandaliwe ili tuweze kubadilishana uzoefu na kujifunza na pia kwenda mahakamani”. Akasema Dkt. Dalfina Ndumbalo Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...