************************

Benki ya NMB na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kupitia Wakala wa Serikali Mtandao ‘eGovernment Zanzibar’, wamesaini makubaliano ya ushirikiano, yatakayowezesha mifumo ya NMB kuingiliana na ZanMalipo, kusaidia taasisi kukusanya mapato kupitia matawi na mifumo ya kidijitali ya benki hiyo.

Makubaliano hayo yamefanyika leo visiwani Zanzibar, ambayo yatakuwa ni chachu ya ukuaji wa uchumi visiwani humo, endelevu na wenye manufaa kwa SMZ na taasisi zake lakini pia utakaoleta maendeleo chanya.

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, aliipongeza SMZ chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa mageuzi chanya ya kiuchumi yanayochakatwa na kusimamiwa na serikali yake kwa ustawi wa Taifa.

Zaipuna alibainisha kuwa makubaliano hayo ni chachu kwa taasisi yake kubuni suluhushi mbalimbali za Wazanzibari na Taifa ujumla, na kwamba maendeleo ya kidijitali kwa ulimwengu wa sasa hayaepukiki, hivyo ushirikiano wao huo utakuwa na mchango chanya katika kuharakisha ukuzaji uchumi na kurahisisha utendaji wa Serikali.

Makubaliano haya ni kielelezo tosha kuwa Serikali ya Zanzibar na NMB inakwenda kushirikiana kuboresha huduma za ukusanyaji mapato na malipo, sambamba na kuwezesha mifumo yetu kuingiliana na ile ya ZanMalipo, hivyo kuwezesha Taasisi za SMZ kukusanya mapato kupitia matawi ya NMB na mifumo ya kidijitali ya benki yetu.

Benki ya NMB na eGovenment Zanzibar, wanaenda kutengenezea Kituo cha Pamoja cha Malipo Kidijitali ‘One Stop Center,’ cha Shirika la Bandari Zanzibar, ambacho kitampa mlipaji wa huduma mbalimbali ‘control number’ moja kwa ajili ya kufanyia malipo mbalimbili bandarini, badala ya namba tofauti tofauti.

Suluhisho hizi mbili zinazooambatana na makubaliano haya, zinaenda kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, lakini pia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato na kuondoa kero ya muda mrefu wanaotumia wananchi kufanya huduma za malipo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB alibainisha kuwa, SMZ kupitia eGovenment na NMB, wanaenda kujenga ushirikiano utakaokuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na kwamba matarajio yao ni kuwa na ushirikiano endelevu, wa karibu zaidi, wenye manufaa kwa SMZ na taasisi zake, utakaoleta maendeleo chanya ya Serikali, Taifa na wananchi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa eGovernment Zanzibar, Said Seif Said, aliishukuru Benki ya NMB kwa kusaini makubaliano ya ushirikiano huo, ambao aliutaja kama muarobaini wa changamoto mbalimbali za kimalipo wanazokutana nazo wananchi wa Zanzibar, unaoenda pia kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.

Seif alisema kuwa eGovernment inaamini kwamba ushirikiano huu ni chanya, utakaobeba tija kwa Serikali, hususani hiyo ‘One Stop Center’ ambayo itajikita katika kurahisisha mifumo ya malipo bandarini ambako tutatumia mifumo ya kidijitali kuongeza ufanisi kwenye makusanyo mbalimbali.

Pia, alisisitiza kuwa huu ni mwanzo tu, wanategemea kufanya mengi makubwa kwa pamoja baina yao na NMB. Bandarini ni sehemu ambako kumekuwa na changamoto za muda mrefu katika masuala mazima ya makusanyo, lakini kupitia makubaliano haya wanaamini yataondoa na kumaliza changamoto zote hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...