WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amesema kuwa katika mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wamefanikiwa kuanza kujenga Mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) .
Mfumo huo ni kwaajili ya kuondokana na changamoto za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS, ambao haukuakisi hali halisi ya utendajikazi wa watumishi hali iliyoleta hisia za kupendeleana au kuoneana na kutokutumika kwa matokeo ya utendajikazi katika kufanya maamuzi ya kiutumishi.
Hayo aliyasema jana jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mwaka mmmoja wa Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan .
Alisea kuwa Mfumo mpya wa Public Employees Management Information System (PEPMIS) utakuwa ni wa kielektroniki na utaondokana na matumizi ya makaratasi.
“Pia utaongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji wa utendaji wa watumishi,lakini pia utaweka mifumo ya ufuatiliaji wa utendaji kazi wa watumishi kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa na yanayopimika”alisema Mhagama.
Pia alisema kuwa mfumo huu pia utahamasisha uwajibikaji wa hiari na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za utendaji kazi wa watumishi.
Wakati huo huo alisema kuwa katika kipindi hiki Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi Public Institutions Performance Management Information System (PIPMIS).
“Mfumo huu ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi ya Umma kuhusu malengo ambayo taasisi husika itayatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja”alisema.
Alisema kuwa makubaliano hayo yatakuwa kati ya viongozi wakuu wa taasisi na viongozi wao wanaowasimamia katika masuala ya kisera na utendaji wa kila siku.
“ Utekelezaji wa mfumo wa huu wa PIPMIS utaongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa sera, mikakati na vipaumbele vya taasisi, sekta na taifa kwa ujumla, kuimarisha utamaduni unaojali matokeo, na kuleta matumizi bora ya rasilimali za umma”alisema.
Wakati huo huo alisema kuwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imefanikiwa kujenga Mfumo wa Sema na Waziri wa UTUMISHI kwa lengo la kuwawezesha watumishi na wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu masuala mbalimbali ya Utumishi na Utawala.
Alisema mfumo huo unampa fursa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kufuatilia namna masuala ya utumishi na Utawala Bora yaliyowasilishwa na wananchi na watumishi wa Umma yalivyofanyiwa kazi na kumuwezesha Waziri kufuatilia hali ya uadilifu na uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kushughulikia masuala mbalimbali ya utumishi na utawala bora.
“Mfumo huu pia unamuwezesha Waziri wa Utumishi na Utawala Bora kuongea moja kwa moja na mlalamikaji ili kujua ni kwa namna gani tatizo lake limefanyiwa kazi na kuchukua hatua stahiki”alisema.
Wakati huo huo Mhagama alisema kuwa Rais aliwaelekeza kuwapandisha vyeo Watumishi 190,781 wenye sifa stahiki.
“ Rais aliamua tutumie jumla ya sh. bil 39,649,988, 204 na kazi inaendelea,kulipa madeni ya mishahara ya Watumishi wa Umma 65,394 yenye thamani ya sh. bil 91,087,826,006.34”alisema
Lakini pia kuwabadilisha kada Watumishi wa Umma 19,386 na kuwalipa mishahara mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 1,330,306,572,kutoa vibali12,336 vya ajira mpya na mbadala ambapo jumla ya sh. bil 7,761,869,809 zimelipwa na kuwapunguzia kodi watumishi wa umma kutoka asilimia 9 mpaka 8.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Jenista Mhagama akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...