Na Khadija Kalili, Chalinze
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza kuelekea zoezi la uhesabuji wa watu katika sensa ya watu na makazi ameagiza wazazi kuhakikisha watoto na vijana wenye ulemavu wawatoe wahesabiwe, kwani kuhesabiwa ni haki yao ya msingi ili serikali ijue namna ya kupanga mipango ya maendeleo ya kuihudumia jamii ya wananchi kulingana na aina ya wananchi waliopo nchini.
Amesema hayo wakati azindua mradi wa maji wa Mlandizi/ Mboga uliopo Chalinze mkoani Pwani uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni zaidi ya 18 ambao utahudumia Wilaya za Bagamoyo na Kibaha ulianza kujengwa tangu mwaka 2019 chini ya uongozi wa Rais Hayati John Pombe Magufuli.
Alisema kama kuna nyumba ina mtoto mwenye ulemavu wahesabiwe hivyo wazazi wasiwafiche watoto wala watu wote wenye ulemavu maana kulikuwa na baadhi ya watu kwenye jamii walikuwa wakiwaficha watoto wenye ulemavu na walemavu ili kusaidia serikali kujua idadi halisi ya wananchi waliopo nchini itakayosaidia kupanga maendeleo ya nchi kulingana na idadi na aina ya wananchi waliopo.
"Tunapokwenda kuhesabiwa tuhakikishe kama kuna mtoto mwenye ulemavu ahesabiwe kwasababu dira ya kitamataifa tunayoifuata inatutaka kuhakikisha hata mtoto mwenye ulemavu ahesabiwe kwani ataingizwa kwenye hesabu za maendeleo kwahiyo kila mmoja ahesabiwe" alisema Rais Samia.
Akizungumzia miradi huo wa Mlandizi Mboga Rais Samia ameagiza kutoa shilingi bilioni moja kwaajili ya kuharakisha usambazaji wa maji katika mradi wa maji huo kwa awamu mbili ilikuharakisha usambazaji wa huduma za maji kwa wananchi.
Rais Samia alisema kwa awamu ya kwanza ameagiza kutolewa shilingi milioni 500 ambapo baadae atangalia kuongeza tena shilingi milioni 500 fedha ambayo itarudishwa kutokana na ulipaji wa bili za maji wa wananchi wa Chalinze na kuwahimiza wananchi kulipa bili zao za maji kwani mradi huo sio Sadaka kwani jinsi wananchi wanavyolipa bili ndivyo huduma hiyo ya maji itaendelea kutolewa kwa wananchi.
Alisema uzinduzi wa mradi huu wa mradi wa maji umekwenda muafaka na ikiwa ni katika kukamilisha yale yote yaliyomo katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020.
"Tunafunga wiki ya maji ikiwa ni sherehe ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Waziri wa Maji Juma Aweso hivyo Mrisho Mpoto mwimbie wimbo"alisema Rais Samia Suluhu Hassan.
"Nakumbuka wakati wa kampeni nilijionea changamoto ya maji na hasa hapa katika Jimbo la Chalinze Mkoa wa Pwani safari ya kuleta maji Chalinze ilikuwa ndefu lakini leo tumemtua mama ndoo kichwani" alisema Rais Samia.
Pwani ni Mkoa wa viwanda tunakwenda kuzodi asilimia 85 na tutakapofika 2025 tutafikia asilimia 100 kwa kweli kazi kubwa imefanyika nimetembelea mradi nimeona hongera sana kwako Waziri pia hongera na DAWASA tutaanzia na kutoa Mil.500 Ili kazi ya usambazaji maji kwa wananchi iende haraka wekeni mfumo mzuri Ili maji yawafikie kwani huduma hii ni muhimu.
Natoa wito kwa wananchi wa Chalinze lindeni miundombinu Ili maji yaendelee kutoka na muendelee kupata maji hivyo lindeni miundombinu tuliyowaletea, alisema Mheshimiwa Rais Samia.
Maji haya siyo sadaka ya bure niwaombe sana jinsi mtakavyolipa bili zenu za maji Ili huduma iendelee kupatikana.
Nimefurahishwa kusikia kwamba mradi huu utasaidia kupatikana maji katika maeneo ya viwanda.
"Natambua changamoto mlizonazo wakaazi wa Chalinze hivyo naahidi kwamba nitakuja kuzitatua ikiwemo barabara, pia nawakumbusha kuwa kila mtanzania anahaki ya kuhesabiwa ikiwemo watoto walemavu Hawa wanayohaki na kila.mmoja anatakiwa ahesabiwe Ili tujue tunajipangaje
Mradi huo upo katika maeneo ya Mlandizi ,Mboga Chalinze ambapo huu utakuwa ukisafirisha maji kupitia Bomba lenye kipenyo cha inchi 16 (DN400) swa na umbali wa KM.59 kutoka Mlandizi (Mitambo ya Ruvu Juu) hadi Kijiji cha Mboga (Msoga) ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
Mradi huu wa bomba kuu unatarajiwa kusafirisha kiasi cha lita za ujazo Mil.9 (9,3000,000)kwa siku ambazo zitawezesha kuwahudumia wakazi wapatao 120,912 kwa siku, sambamba na ujenzi wa mradi huu, vituo viwili vya kusukuma maji (Boosting Stations) vimeshajengwa katika Vijiji vya Chamakweza na Msoga ambapo pampu sita(tatu kwa kila kituo) zimeshafungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakar Kunenge akitoa salamu za Mkoa alisema kuwa mbali ya wananchi kunufaika na mradi huo pia maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo ni pamoja na maeneo ya viwanda vya Twyford, KEDA, Kiwanda Cha ngozi, Bandari Kavu ya Vigwaza, Kiwanda Cha Juice -SAYONA , Stesheni ya Treni ya Mwendokasi-Vigwaza (Kwala),Kituo Cha Mizani -Vigwaza pamoja na maeneo tengefu yaliyoko katika mpango wa ujenzi wa viwanda.
RC Kunenge alisema kuwa mradi huu unatekelezwa kwa awamu huku akiwataka Mamlaka ya Maji safi na Majitaka (DAWASA) kuhakikisha wanayafikia maeneo yote yenye uhitaji wa maji yaliyobaki.
"Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Pwani natoa shukrani za dhati kwa ziara hii kwetu hili ni jambo la heshima kubwa kwetu sisi Pwani kwani ameonyesha kututhamini kwa kiwango cha hali ya juu kwa sababu miradi hii ya maji iko mingi nchini hivyo angeweza kwenda kuzindua katika Mkoa wowote lakini ametuheshimisha kwa kuja kuzindua mradi huu Kwetu Pwani tunamshukuru sana"alisema RC Kunenge.
RC alisema kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha Bil.18.
"Mradi huo umeanzia Mlandizi Wilaya ya Kibaha ambako kumewekwa vituo vidogo vya maji ikiwemo ,Chamakweza na Mboga zilizopo ndani ya Hamashauri ya Chalinze
Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Polisi Chalinze huku ukiwa umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Wizara ya Maji Juma Aweso, Generali Mstaafu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Davis Mwamunyange (SDF), Manaibu Waziri, Wabunge wote wa Mkoa wa Pwani, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Viongozi wa dini zote Wakurugenzi wa Halmashauri zote, Madiwani,Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi wa Mkoa wa Pwani.
Pia RC Kunenge amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufanya jitihada kubwa za ujenzi wa Barabara huku akiitaja Barabara ya Pangani Baobab ambayo itaunganisha kwenda Bagamoyo ikiwa imeshazinduliwa na ujenzi unaendelea kwani wakandarasi wanaendelea na kazi.
Akizungumzia kuhusu zoezi la chanjo ya Covid 19 Pwani inaendelea vizuri sanjari na kujipanga vema kwa zoezi la Sensa huku zoezi la uandikishwaji wa anuani za makazi unaendelea vizuri.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi Ridhiwani Kikwete amesema anamshukuru Mheshimiwa Rais na kuwa mtiifu kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,hii heshima kubwa uliyotupa mimi binafsi na kwa wana Chalinze
Amesema "Asante sana zaidi ya miaka 50 jimbo hili lilikua likikabilina na ukosefu wa maji lakini leo tumeandika historia katika kuibadilisha Chalinze hizi jitihada zako mama zinanekana, alisema Kikwete.
Mwisho nakushukuru sana kwa uzinduzi wa mradi huu mkubwa wa maji leo nina furaha sana kuona mradi huu wa maji umekamilika.
"Pia namshkuru Hayati Ris John Pombe Magufuli kwani yeye ndiye aliyeanzisha mradi huu Ili kuwakomboa na adha ya ukosefu wa maji wakaazi wa Chalinze Mungu amlaze mahali pema peponi" alisema Kikwete.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiondoa Kitambaa kuzindua mradi wa maji wa Mlandizi-Chalinze-Mboga katika tukio lililofanyika Chalinze mkoani Pwani leo tarehe 22 Machi 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Chalinze mkoani Pwani katika Mkutano uliofanyika Viwanja vya Polisi Chalinze Mkoani Pwani mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa Mlandizi-Chalinze-Mboga leo tarehe 22 Machi 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...